Maiti yafukuliwa, yabainika kukatwa baadhi ya viungo

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu
Muktasari:
Selina alifariki Februari 2, katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Nyerere baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa Februari 3, mwaka huu kijijini hapo na Machi 22 ikiwa ni siku 20 walikuta kaburi limefukuliwa sehemu ya kichwani na miguuni. Hivyo kutoa taarifa polisi ili kupata kibali cha mahakama kufukua na kuhakiki kilichomo.
Serengeti. Taharuki imetanda kwa wakazi wa Kijiji cha Parknyigoti, Kata ya Ikoma, Wilaya ya Serengeti mkoani baada ya kufukua kaburi la Selina Jumapili na kukutwa sehemu mbalimbali za viungo vikiwa vimekatwa.
Selina alifariki Februari 2, katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Nyerere baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa Februari 3, mwaka huu kijijini hapo na Machi 22 ikiwa ni siku 20 walikuta kaburi limefukuliwa sehemu ya kichwani na miguuni. Hivyo kutoa taarifa polisi ili kupata kibali cha mahakama kufukua na kuhakiki kilichomo.
Ufukuaji huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Mtiro Marinya chini ya maelekezo ya wazee wa mila ya jamii ya Kiikoma. Zoezi hilo lilitawaliwa na usiri mkubwa baada ya kubaini sehemu za siri, vidole vya mguu na sikio la kushoto vimenyofolewa.
Katibu wa mila ya jamii ya Waikoma, Hussein Ramadhani mmoja wa waliohusika kwenye zoezi la ufukuaji alisema kwamba walipobaini vitendo visivyo vya kawaida kwa ushauri wa wazee walikubaliana kutokuwaambia wanawake ili kupunguza hofu lakini kilichofanywa kinahusishwa na imani za kishirikina.
“Vitendo hivi ni vya kishirikina maana kufukua kaburi na kukata viungo hivyo kisha kufukia haya ni mambo ya kishirikina zaidi...Hali kama hii ukiisema hadharani utazua hofu na ndiyo maana wanawake wameruhusiwa kuangalia kama ni yeye ama la walioweza wameona,” alisema.
Naye Mzee wa Mila, Nyarancha Kichembu kutoka Kijiji cha Bwitengi alisema, tukio hilo ni la kwanza kutokea na kuwa wanawake hawapaswi kuambiwa hali halisi na kuwa limewasikitisha na linawapa wakati mgumu kutafuta undani wa vitendo hivyo.
“Kama maiti isingelikutwa ndani angenyongwa kondoo jike na kutumbukizwa ndani na kuzikwa kisha taratibu za kimila zingefuata maana si mambo ya kawaida haya….lakini kwa hili lililojitokeza uchunguzi unaendelea ili kubaini wanaojihuisha na vitendo hivyo vinavyozidisha hofu kwa watu,” alisema.
Mama mzazi wa marehemu huyo Nyahande Kwimambo alisema “Kuna kitu kisicho cha kawaida kilitokea Machi 22 kwa kawaida tunaamka saa 12 alfajiri lakini siku hiyo tuliamka wote saa nne na kukuta kaburi limefukuliwa sehemu ya kichwa na miguuni, ikabidi nipige yowe,” alisema.
Alibainisha kuwa hofu yake ilikuwa ni kwamba mwanaye alichukuliwa, lakini baada ya kufukua ameona kuwa ni yeye roho yake imetulia, hata hivyo waliohusika na kufukua hawakumweleza walichobaini baada yake walimtaka athibitishe kama ndiye kisha wakazika.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Marinya Marwa alisema walifikia uamuzi wa kufukua baada ya hofu kutanda kijijini hapo na kuwa taratibu zote za kisheria zimefuatwa na hivyo walichoona watu, yeye hawezi kuyasemea zaidi mambo hayo na kuwa watatoa taarifa kwa vyombo husika.