Mahakama yatupilia mbali kesi ya mke wa Mdude

Wakili Boniface Mwabukusi akitoa msimamo wao baada ya Mahakama kutupilia mbali shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Uamuzi huo umetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya, Said Kalunde leo Jumatano Julai 9,2025.
Mbeya. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imetupilia mbali shauri lililofunguliwa na mke wa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mwanaharakati, Said Nyagali, maarufu Mdude, Sije Mbughi dhidi ya wajibu maombi sita, akiwapo Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP).
Uamuzi huo wa Mahakama umetolewa leo Jumatano Julai 9, 2025 na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Said Kalunde baada ya upande wa mlalamikaji kutothibitisha mwathirika wa shauri hilo kushikiliwa na wajibu maombi.
Awali, imeelezwa mleta maombi Sije Mbughi ambaye ni mke wa Mdude, aliwasilisha ombi la kuomba mahakama kuamuru wajibu maombi sita akiwamo IGP na Mkuu wa Upelelezi, kumuachia Mdude au kufikishwa mahakamani.
Wengine ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (OCD), Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Shaaban Charo ambaye alidaiwa kumdhuru Mdude Mei 2, 2025.
Shauri hilo namba la mwaka 2025 lilianza kusikilizwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 30 mwaka huu, huku mleta maombi akiwasilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Boniface Mwabukusi, Hekima Mwasipu na Solomon Kamunyu.
Kwa upande wa Serikali wa wajibu maombi uliwakilishwa na mawakili wawili ambao ni Dominick Mushi na Adalbert Zegge.
Awali, kabla ya kutupilia mbali shauri hilo, Jaji Kalunde alitoa hoja kadhaa walizobaini ikiwamo Mahakama kutothibitisha mwathirika kwenye shauri hilo kushikiliwa na wajibu maombi
Hoja nyingine ni pamoja kiapo cha mleta maombi hakuonyesha maelezo ya kumtambua Shaban anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo Mei 2, 2025.
Jaji Kalunde amesema kuwa kiapo cha ushahidi ndio misingi ya mahakama kufanya uamuzi wa ombi lililowasilishwa.
Inadaiwa, Mdude Nyagali ambaye ni mwanaharakati alivamiwa nyumbani kwake Mei 2,2025 na watu wasio julikana ambao walikuwa na silaha na nyundo na kisha kumjeruhi na kutoweka naye kusikojulikana.
Inadaiwa kuwa watu hao walivunja mlango na kuingia ndani na kisha kujitambulisha kuwa ni askari Polisi ambapo walimshambulia kumjeruhi na kisha kuondoka naye.
Kauli ya Mwabukusi
nje ya Mahakama
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa mleta maombi, Boniface Mwabukusi amesema bado wataendelea kutafuta haki ya Mdude kwa sababu kitendo cha kuchukuliwa ni tusi na dhihaka kwake.
Amesema kwa sasa watakaa na wanasheria wenziye kuangalia namna ya kufanya ili haki ipatikane.
Katika hatua nyingine, Mwabukusi amesema mwenendo wa shauri hilo haujaenda kama walivyotarajia, lakini wamepiga hatua na kusisitiza anayecheza na Mdude amecheza na usalama wao.
Kauli za wanachama
Mmoja wa makada wa chama hicho, Asha Landa amesema hawajaridhishwa na uamuzi wa mahakama na kuomba mawakili wa upande wa mleta maombi kukata rufaa kwa sababu wapo tayari kuendelea kuchangia kesi hiyo.