Mahakama yamruhusu mhasibu kupinga Rais kuridhia kufukuzwa utumishi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam imeridhia maombi ya aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Pere Muganda kufungua shauri la kupinga uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi kuridhia kuachishwa kwake kazi.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Abdi Kagomba baada ya kujiridhisha kuwa amekidhi vigezo vya kisheria, katika maombi yake hayo ambayo pia yaliungwa mkono na wakili wa Serikali aliyeiwakilisha Serikali wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo.
“Kwa kuzingatia sababu hizo hapo juu, nimeridhika kuwa maombi (shauri) yamekidhi viwango vya kisheria kupewa ruhusa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio”, amesema Jaji Kagomba kwa tafsiri isiyo rasmi, baada ya kujadili hoja za pande zote na kuhitimisha:
“Kwa hiyo ninatoa kibali kwa mwombaji (Muganda) kuomba amri (za mahakama) kama alivyoomba.”
Muganda alifukuzwa utumishi wa umma na Tume ya Utumishi wa Umm kwa tuhuma za kupoteza pesa za umma, uamuzi ulioungwa mkono na Katibu Mkuu Kiongozi na kuidhinishwa na Rais, Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo Muganda hakuridhika na uamuzi huo, hivyo alifungua shauri la maombi dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Halmashauri ya Wilaya ya Siha na Mwanasheria Mkuu.
Katika shauri hilo la maombi namba 40/2023, Muganda ambaye aliwakilishwa na wakili Isaac Muganda, aliomba ridhaa ya kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama (Judicial Review).
Aliomba aruhusiwe kufungua shauri hilo ili mahakama iupitie uamuzi huo na kutoa amri ya kuutengua, kuwaamuru wajibu maombi kutenda kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na kuwazuia kuingilia ajira yake bila kufuata sheria na taratibu.
Wakati wa shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza, wakili wa Serikali Doreen Mhina aliieleza mahakama dhahiri kuwa baada ya kudurusu maombi hayo wajibu maombi waliridhika kwamba mwombaji amekidhi matakwa ya kisheria kupata idhini kufungua shauri hilo.
Hivyo aliunga mkono maombi hayo na wakili wa mwombaji, Tasinga naye bila kusita aliafiki maombi na maelezo ya wakili Doreen.
Jaji Kagomba katika uamuzi wake amesema baada ya kusoma hati ya maombi ya mwombaji, kiapo chake pamoja na hati ya maelezo yake amekidhi viwango vya kisheria kupewa ruhusa hiyo.
Amevijata vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kuwa na maslahi katika shauri hilo, yaani kufukuzwa katika ajira yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha na kwamba ndiye muathirika wa uamuzi huo kwa madai ya kupoteza fedha za umma.
Pia Jaji Kagomba amesema kuwa Muganda ameibua hoja zinazotakiwa kuamuriwa kwa kuwa andai kuwa uamuzi wa kuondolewa katika utumishi wa umma na hatimaye kuthibitishwa na Rais haukuzingatia kanuni za haki ya asili inayofungamana na kusikilizwa kwa usawa.
Vilevile Jaji Kagomba amesema kuwa Muganda amebainisha kuwa hakupewa taarifa kwa muda wa kutosha kusikilizwa katika kamati ya nidhamu, kukataliwa fursa ya kutumia nyaraka muhimu na kunyimwa muda wa kutosha kuandaa utetezi wake.
Jaji Kagomba amerejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika rufaa ya madai ya David Mushi dhidi ya Abdallah Msham Kitwanga, rufaa namba 286/2016 kuwa usawa katika kusikilizwa ni haki msingi inayohifadhiwa chini ya Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya Nchi.
“HIvyo madai ya kunyimwa haki ya kusikilizwa kwa usawa ni mazito na mahakama sharti iwe katika tahadhari. Itoshe kusema kwamba mwombaji amekidhi vigezo vya kuwa na hoja za kesi. Hii ni bila kujali kama madai hayo hatimaye yatathibitika au la,” amesema Jaji Kagomba.
Amehitimisha kwa kusema kuwa pia alithibiitisha kuwa alifungua shauri ndani ya muda wa miezi sita kwani licha ya uamuzi huo kuthibitishwa na Rais Machi Mosi, 2023, aliuupokea Machi 13, 2023 na alifungua shauri hilo Septemba Mosi 2023, ndani ya miezi Sita.