Mahakama ya Kisutu yatishia kuifuta kesi ya Idris Sultani

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa ahirisho la mwisho katika kesi ya kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inayomkabili msanii wa vichekesho, Idris Sultani na wenzake wawili.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa ahirisho la mwisho katika kesi ya kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inayomkabili msanii wa vichekesho, Idris Sultani na wenzake wawili.
Hatua hiyo imetokana na upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani kwa miezi mitano mfululizo, tangu Desemba 8, 2020 kesi hiyo ilipotakiwa ianze kusikiliza ushahidi.
Uamuzi huo umetolewa leo, Alhamisi Mei 27, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea.
Hakimu Ruboroga amesema tarehe ijayo kama upande wa mashtaka hawatapeleka shahidi mahakamani hapo ataifuta kesi hiyo.
" Kesi ya hii haijaendelea kwa muda mrefu na nikiangalia jalada hapa, kesi hii tangu Desemba 8, 2020 haijaendelea na ushahidi, hivyo leo natoa ahirisho la mwisho, terehe ijayo kama upande wa mashtaka hamtaleta shahidi mahakamani, kesi hii nitaifuta" amesema Hakimu Ruboroga.
Sultan na wenzake wawili wanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na kibali.
Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka hawana shahidi, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza ushahidi.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Doctor Ulimwengu (28)mkazi wa Mbezi Beach na Isihaka Mwinyimvua (22) mkazi wa Gongolamboto.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8, 2016 na Machi 13, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Loko Motion, walichapisha maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mbali na kesi hiyo, Idris alikuwa na kesi nyingine ya kushindwa kufanya usajili wa laini ya simu ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, iliyokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo tangu Februari mwaka huu.
Hakimu Chaungu aliifuta kesi hiyo Mei 15, 2021 na kumwachia huru chini ya kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai( CPA).
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Idris kuachiwa na Mahakama, alikamatwa tena na askari polisi waliokuwepo Mahakamani hapo na kupelekwa kituo cha Polisi cha Oysterbay.