Magufuli acharuka wanaokwamisha uwekezaji

Muktasari:
Rais John Magufuli amesema baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa vichwa ngumu kama samaki aina ya kamongo na kuwataka kuachana na vikwazo vinavyokwamisha shughuli za uwekezaji nchini
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa vichwa ngumu, akiwafananisha na samaki aina ya kamongo.
Amesema kuna baadhi ya watendaji hawataki kuelewa na wamekuwa wakimuona mwekezaji kama adui badala ya kumwona rafik na kuwataka kubadilika haraka.
Amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha majani ya chai katika kijiji cha Kabambe mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa mbalimbali.
“Kuna matatizo ya uwekezaji katika nchi yetu, saa nyingine inakuwa inakatisha tamaa kuja kuwekeza, mtu anapotaka kuja kuwekeza saa nyingine anapata shida, masharti ni ya ajabu ajabu, baadhi ya watendaji wetu wamekuwa ni matatizo katika uwekezaji.”
“Ninawaomba watendaji ndani ya serikali wabadilike, mtu anataka kuja kujenga kiwanda unamzungusha mpaka mwaka mzima. Yeye ana pesa zake anataka kujenga kiwanda hata mabati na ajira zitapatikana hapa, lakini watu wamekuwa na vichwa vigumu sana, nafuu vichwa vya kamongo. Hawataki kuelewa, wapo wawekezaji wamekuja hapa wamewekewa mikwara mpaka wakaamua kwenda nchi za jirani,” amesema.
Amesema baadhi wamekuwa wakiombwa rushwana kulitupia lawama Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwamba nalo limekuwa likihusika kukwamishaji shughuli za uwekezaji.
“Wengine wamekuwa wakiomba rushwa, mara Nemc waseme kwamba mazingira ya hapa hayafai mpaka tukupime, wewe ardhi umeikuta hapa imeimbwa na Mungu halafu unasema mazingira ya namna gani, mara sijui kuna OSHA , sijui unaosha macho, vimasharti vya hovyo vimekuwa vingi, lakini tunajichelewesha wenyewe,” amesema.
Rais Magufuli amesema wawekezaji wanapenda kuja Tanzania kutokana na vivutio vilivyopo, lakini tatizo ni wahusika katika maeneo ya uwekezaji.
“TIC (kituo cha uwekezaji) ilikuwa wizara ya viwanda na biashara niliona mambo hayaendi vizuri sasa nimeamua kuirudisha ofisi ya waziri mkuu, nikiona mambo hayaendi nitairudisha kwangu,” amesema.