Madiwani Iringa waomba wananchi waongezewe kondomu

Muktasari:

  • Wakati Mkoa wa Iringa ukishika nafasi ya pili kwa maambukizi ya Ukimwi, hoja ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wameiomba Serikali iongeze kondomu kwenye vilabu vya pombe za kienyeji hasa ulanzi, ili kupunguza maambukizi hayo.

Iringa. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wameomba Serikali iongeze kondomu kwenye vilabu vya pombe za kienyeji hasa ulanzi, ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Kauli ya madiwani hao imekuja wakati ambao Mkoa wa Iringa ukishika nafasi ya pili kwa maambukizi ya Ukimwi, ambayo ni asilimia 11.2 huku ulevi kupindukia hasa kipindi cha ongezeko la pombe aina ya ulanzi ukitajwa kuwa chanzo cha ngono zembe.

Hata hivyo, hoja hiyo madiwani imezua mjadala mitandaoni huku baadhi ya wananchi wakisema kipaumbele cha wananchi kwa sasa ni uhaba wa sukari na mahitaji mengine muhimu.

Wametoa hoja hiyo juzi Februari 27, 2024 walipokuwa kwenye  kikao cha kamati ya Ukimwi ya Baraza la Madiwani ambacho ajenda yake ni moja, Ukimwi.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 29, 2024 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephane Mhapa amesema upo uhusiano mkubwa baina ya ulanzi na kasi ya maambukizi ya Ukimwi.

"Kwenye mabaraza yote ya madiwani nchi nzima kuna wajumbe wa kamati ya Ukimwi ambao wakifika kwenye kikao cha kila robo mwaka wanajadili masuala ya athari za Ukimwi na ajenda ni hiyo tu hakuna nyingine.”

"Kwenye mabaraza ya madiwani kuna kamati nyingine na moja ya kamati hizo ni kamati inayoitwa kamati ya huduma za jamii hiyo ndio inazungumzia pia hali mbaya ya upatikanaji wa sukari na mambo mengine," amesema Mhapa.

 Amesema hoja ya janga la Ukimwi wasilishwa na kamati ikaonekana kuwa pia kuna uhaba wa kondomu ambayo ni kinga inayoweza kupunguza maambukizi hasa kwenye ngono zembe.

"Tuache kudanganyana Ukimwi upo na hauna dawa na  unaua," amesema Mhapa.

Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoloki Iringa (Rucu), Mafanikio Kinemelo amesema ni kweli ulevi kupindukia hasa kipindi cha ulanzi ni hatari kwa maambukizi ya Ukimwi.

"Nafanya utafiti hasa kujua nje ya ulevi kwa nini Iringa Ukimwi unatajwa zaidi, ni hoja muhimu kujadili na tusiipuuze. Afya ni mtaji," amesema Kinemelo.

Kwa upande wake Fadhiri Ngajiro amekiri suala la ulevi kupitiliza kama moja ya chanzo cha mkoa huo kuwa kinara wa ukimwi.

"Unywaji pombe kupitiliza na ngono zembe, kurithi wajane, hamjagundua kuwa watu wengi hawajishughulishi na mambo ya Mungu. Watu wakikosa hofu ya Mungu ni rahisi kuambukiza wenzao bila hofu na huruma. Haya ni mambo ya kujadili," amesema Ngajiro.

Hata hivyo, Innocent Mbwilo amekosoa hoja hiyo akisema madiwani hao walipaswa kujadili uhaba wa sukari na kutafuta ufumbuzi na sio kujadili kondomu, hata kama Ukimwi unatajwa sana Iringa.

"Mahitaji yetu ni sukari sio kondomu, kweli tunakunywa ulanzi na wengine wakilewa wanafanya ngono zembe, lakini tuongelee hili hitaji letu la sukari," amesema.