Madhara ya kamari kidini na kidunia
Muktasari:
- Katika nyakati za leo, aina za kamari zimeongezeka sana, kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia, vyombo vya habari, na mtandao wa intaneti.
Hakika miongoni mwa rehema za Allah kwa waja wake ni kuwaridhia dini ya Uislamu kuwa sharia yao—dini iliyoleta kila jambo lenye manufaa kwa binadamu katika maisha ya dunia na Akhera.
Allah Mtukufu amesema: “Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimetimizia neema Yangu juu yenu, na nimeridhia Uislamu uwe dini yenu..” [5:3]. Mafundisho ya Uislamu aliyoyaweka Allah hayahusiani na ibada za kiroho tu, bali pia ni mambo yanayohusu maisha yote ya mwanadamu hapa duniani, ikiwemo miamala baina ya mtu na mwenzake, na baina ya mtu na Mola wake.
Ukizitafakari Sharia hizi za mbinguni, utakuta kuwa zimekusanya maslahi yote ya wanadamu na sababu za ustawi wao. Wanaposhishikamana nazo kikamilifu hupata ushindi, nguvu na utukufu.
Lakini wanapoanza kuzipuuza na kuzembea katika kuzitekeleza au kuacha baadhi yake, hapo ndipo unyonge, udhalili na mateso ya maadui wao huwapata—na hii ndiyo Kanuni ya Allah ya Kimaumbile kwa viumbe Wake.
Wanafalsafa husema: “ Haifai kulitolea hukumu jambo lolote ila baada ya kulifahamu”Wanazuoni wa Uislamuwa mwanzo na wa sasa wameilezea kamari kwa matamshi tofauti lakini yenye maaana moja. Mwanazuoni Az-Zuhr Allah amrehemu ameilezea kamari:
Ni kutupa mishale ya bahati nasibu juu ya mali au mazao” Naye mwanazuoni wa sasa Sheikh Qardhaw- Allah amrehemu- ameileza kamari: : Ni kila mchezo ambao mshiriki haepuki moja ya mambo mawili kupata faida au hasara.
Katika nyakati za leo, aina za kamari zimeongezeka sana, kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia, vyombo vya habari, na mtandao wa intaneti. Miongoni mwa aina hizo ni kubashiri michezo ya mpira na mashindano mbalimbali, kubeti kupitia ujumbe mfupi wa simu, kwenye luninga na redio kwa kutuma gharama za kushiriki.Ingawa hupewa majina mazuri na yakuvutia, kama vile majina ya “zawadi”, “bahati nasibu”, au “ “mkwanja”. Majina hayo hayabadilishi uhalisia wake kuwa kamari ni haramu.
Allah Mtukufu amesema: “Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika vyote viwili kuna madhara makubwa ….” (2:19). Kadhalika Allah Mtukufu amesema: “Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? (5: 90–91). Kwa hivyo, pombe na kamari zini madhara makubwa ambayo Uislamu ulikuwa wa kwanza kupambana nayo ili kuilinda familia, jamii na taifa zima.
Fedha au au mali inayopatikana kwa njia ya kamari ni haramu na haiwezi kukubaliwa na Allah kama sadaka, zaka, au hata kujenga misikiti au kuitoa wakfu. Hata dua ya anayecheza kamari haikubaliwi na Allah Mtukufu: Mtume wa Allah (rehema na amani ziwe juu yake) amesema “Hakika Allah ni mwema, hakubali isipokuwa kilichokuwa chema….”
Kama ambavyo kamari ina madhara yanayohusiana na dini ya mtu na humuweka katika hatari ya kupata ghadhabu ya Allah na adhabu ya Siku ya Kiyama, vivyo hivyo ina madhara mengine yanayohusiana na maisha ya dunia, ambayo huharibu utulivu na kuondoa ladha ya maisha.
Baadhi ya madhara haya yametajwa katika Qur’an, na mengine yanaonekana wazi katika maisha ya kila siku ya wanaojishughulisha na michezo ya kamari. Kamari husababisha uadui na chuki kati ya watu wanaocheza kamari kwa aina zake zote.
Kamari inachangia kuenea kwa uhalifu, kama wizi, anayetazama mchezo wa kamari huona jinsi mtu mmoja anavyopoteza mali yake kwa haraka na mwingine kupata kwa sekunde chache. Hii humvutia mtazamaji na kumpa tamaa ya kujaribu.
Mara nyingi hutumia njia haramu kama wizi ili kuridhisha hamu hiyo. Kamari husababisha mauaji, mara nyingine mchezaji huchukizwa na kupotea kwa mali aliyohangaika kuipata kwa muda mrefu. Hasira humshinda, na anaweza kujidhuru mwenyewe (kujiua), au kumuua mwenzake kwa lengo la kurejesha kile alichopoteza.
Haya ndiyo matokeo ya kawaida ya wanaoshinda na wanaoshindwa katika kamari Kwa sababu hii, sehemu nyingi za kamari huwa ni maskani ya ufuska, ulevi, dawa za kulevya na maovu mengine.
Kamari imeziparaganyisha familia nyingi, kuna wazazi ambao kamari imewapeleka kwenye msiba wa kuharibu maisha ya familia zao baada ya kuishi katika neema, imesababisha familia hizo kutawanyika na watoto kuwa mitaani bila msaada wala uangalizi. Kamari ni njia ya mapato yasiyokuwa halali, kwani msingi wake ni bahati tu, si kazi wala jitihada.
Hivyo kamari haizai manufaa yoyote kwa jamii ila hasara, umaskini, na vurugu. Mtu anapozama kwenye michezo ya kamari, hupoteza utulivu wa akili na hisia na haoni madhara ya pesa zinazotoweka mikononi mwake. Anakubali apoteze chochote alicho nacho kwa tamaa ya kutaka kupata kingi zaidi.
0712 690811