Madereva masafa marefu na kati wajitosa kuchangia damu

Muktasari:
- Katika zoezi la utoaji damu salama madereva zaidi ya 380 wamechangia mikoa mbalimbali kama Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Tunduma katika benki ya damu salama.
Dar es Salaam. Madereva wa safari ndefu na kati hapa nchini wakiwemo wanaoendesha mabasi na malori wamejitosa kuchagia damu hatua walioitaja kama kurudisha kwa jamii.
Aidha wamesema mara nyingi ifikapo mwisho wa mwaka wamekuwa wakinyooshewa kidole kutokana na ajali nyingi zinazomwaga damu za Watanzania hivyo wamejitosa kuikoa jamii kupitia zoezi hilo.
Hayo yamejiri leo Novemba 25 ikiwa ni siku ya Dereva Tanzania waliyoianzisha mwaka huu iliyoenda sambamba na zoezi la uchangiaji damu kwenye kituo cha daladala cha Mbezi Dar es Salaam.
Akizungumzia Mwenyekiti wa Taasisi ya Madereva Hassan Dede, amesema katika kituo hicho pekee wamechangia damu uniti 138 kwaajili ya kuwasaidia Watanzania wenye mahitaji.
“Kila ikifika mwisho wa mwaka damu nyingi zinapotea zinazotokana na ajali za barabarani na sisi madereva ndio tunaulizwa kuhusu ajali hizo,” amesema.
“Kama walengwa tumeamua kuchangia ili kurudisha damu inayopotea ambayo itasaidia kuokoa maisha ya wenzetu,” ameongeza Dede.
Katika zoezi la utoaji damu salama madereva hao zaidi ya 380 wamechangia mikoa mbalimbali kama Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Tunduma.
Amesema madereva ni kiungo muhimu katika kujenga uchumi wa Tanzania hivyo wameamua kujitoa na kurudisha kwa jamii kutokana na umuhimu wao.
Akizungumza mmoja wa madereva hao Monica Boy amesema wameamua kuchangia damu kutokana na kuguswa kwao na Watanzania wenye mahitaji ya damu huku akisema wao kama madereva watafanya mengi zaidi.
Aidha amegusia changamoto zinazowakabili katika tasnia ya udereva huku akisema zinawafanya kupoteza madereva waaminifu na wenye nidhamu ya kazi huku wale wasio waaminifu kuchukua usukani.
Miongoni mwa changamoto walizoziwasilisha ni pamoja na kukosa mikataba ya ajira zao, mishahara, kuvamiwa na madereva wasio na weledi ‘makanjanja’ na mishahara kiduchu.
Changamoto nyingine inayowapasua vichwa ni ajira zisizo na mikataba, bima, kuzingatiwa usalama na afya kazini pamoja na ushindani wa waajiri wao kwa wawekezaji wa nje.
Amesema changamoto hizo zikitatuliwa watakuwa huru katika ufanyaji kazi huku akiiangukia Serikali.
Vilevile, madereva hao wameiomba Serikali kuboresha mazingira ya waajiri wazawa ili waendeshe biashara zao kwa faida kwaajili ya kuondoa migororo kati ya waajiri na wao.
Mgeni rasmi ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Jaffary Nyaigesha amewapongeza madereva hao kwa hatua walioichukua kuisaidia jamii.
Aidha amewaahidi kuzipokea changamoto walizonazo zikiwemo maegesho ya magari huku akisema atazifikisha kwa Mkuu wa Mkoa Wilaya na mamlaka husika kwaajii ya kuzitatua sambamba na kukutana nao kwaajili ya kuzungumza kwa kina.
“Wamenisomea risala na wameonekana wanachangamoto nyingi tutakutana nao kwaajili ya kuwatatulia yanayowakabili,” amesema.
“Aidha niwapongeze madereva wote kuja na wazo la kuchangia benki ya damu ili kuifanya kuwa na akiba,” amewashukuru Nyaigesha.