Madaktari kampeni ya Dk Samia wawafikia wananchi Katavi

Jopo la madaktari bingwa 25 waliowasili mkoani Katavi kuweka kambi ya siku tano kutoa huduma za kibingwa hospital zote za halmashauri, wilaya na mkoa. Picha na Idd Hassan
Muktasari:
- Ujio wa madaktari hao pia utasaidia kutoa mafunzo kwa baadhi ya madaktari waliopo katika hospitali na vituo vya afya vya halmashauri zote za Mkoa wa Katavi.
Katavi. Kutokana na upungufu wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali mkoani Katavi, madaktari bingwa 25 wamewasili mkoani hapa na watawahudumia wananchi katika halmashauri zote za mkoa huo kwa siku tano.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 10, 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Ezekiel Budem amaesema mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa madaktari bingwa.
Amesema hali hiyo inawafanya wananchi wasafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kutafuta matibabu ya kibingwa katika maeneo mengine.
Amesema ujio wa madaktari hao kupitia kampeni ya Dk Samia Mentorship, itasaidia pia kutoa mafunzo kwa baadhi ya madaktari waliopo katika hospitali na vituo vya afya vya halmashauri zote.
Pia, amesema kwa siku tano watakazokuwepo mkoani Katavi watatoa matibabu bure kwa wananchi wenye matatizo mbalimbali yanayohitaji uchunguzi wa madaktari bingwa.
"Madaktari hawa 25 watagawanywa katika hospitali za halmashauri zote, ili kusaidia upatikanaji wa huduma za kibingwa katika siku tano watakazokuwepo mkoani hapa," amesema Dk Budem.
Ameongeza kuwa madaktari hao wamebobea katika magonjwa mbalimbali, hivyo ni vyema wananchi katika kila wilaya na halmashauri kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa kibingwa na kupatiwa matibabu kwa magonjwa yanayowasumbua.
"Mkoa wetu wa Katavi una changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali. Tunashukuru Serikali kupitia kampeni ya Dk Samia Mentorship kwa kutuletea madaktari bingwa 25 ambao watasaidia kutoa huduma za kibingwa kwa magonjwa ya watoto, wanawake, magonjwa ya dharura na upasuaji," amesema Dk Budem.
Kwa upande wake, Dk Nyamasani Kisori, bingwa wa magonjwa ya watoto ambaye amewasili mkoani Katavi, amesema ujio wao utawanufaisha wananchi kwa huduma za kibingwa, hivyo ni vyema wakajitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.
"Tumefika mkoani Katavi kwa lengo la kutoa matibabu ya kibingwa kwa magonjwa mbalimbali ambayo yanawafanya wananchi wasafiri umbali mrefu kutafuta madaktari bingwa. Sasa tumefika hapa, kikubwa ni wajitokeze kwa wingi kupata huduma hii,” amesema Dk Kisori.
Abdallah Hamis, mkazi wa Kasisiwe, Manispaa ya Mpanda amesema ujio wa madaktari hao utasaidia hasa kundi la wazee ambao wanasumbuiwa na magonjwa mbalimbali yanayohitaji matibabu ya gharama kubwa.
"Tunashukuru Serikali kwa kutuletea madaktari bingwa katika mkoa wetu. Tumeteseka sana hasa sisi wazee tuna magonjwa mengi yanayohitaji madaktari bingwa," amesema mzee huyo.