Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maabara ya tehama sekondari ya Igogwe itakavyowanufaisha wanafunzi

Mwalimu wa Tehama katika Shule ya Sekondari Igogwe wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Felister Paul akiwafundisha wanafunzi wa kidato cha tatu matumizi ya Kompyuta. 

Muktasari:

  • Maabara hiyo imezinduliwa Mei 29, 2025 ikiwa na kompyuta 26 na vifaa vingine kikiwemo kifaa maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa data, kifaa cha kuonesha picha au video kwenye skrini na Luninga vilivyogharimu zaidi ya Sh30 milioni.

Mwanza. Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igogwe, iliyopo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wamesema sasa wana nafasi kubwa ya kuongeza maarifa ya kiteknolojia baada ya shule hiyo kupokea msaada wa kompyuta 26 na vifaa vingine kwa ajili ya maabara ya Tehama.

Msaada huo umetolewa na taasisi ya Camara Education Tanzania kwa kushirikiana na Helios Towers ambapo pamoja na vifaa hivyo, walimu pia watapatiwa mafunzo ya Tehama, mradi uliogharimu zaidi ya Sh30 milioni.

Wakizungumza mara baada ya uzinduzi wa maabara hiyo leo Alhamisi Mei 29, 2025, wanafunzi wa shule hiyo wamesema kompyuta hizo zimekuwa mkombozi kwani sasa wanaweza kufanya utafiti wa kielimu, kujifunza masomo ya sayansi kwa njia ya mtandao na kutumia programu mbalimbali zinazowawezesha kuelewa kwa urahisi zaidi.

Wanafunzi wa shule ya Igogwe iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wakiendelea kujifunza kompyuta kwenye maabara ya Tehama iliyozinduliwa shuleni hapo

Isaya Jumanne, mwanafunzi wa kidato cha tatu, amesema awali alikumbana na changamoto ya kupata vitabu vya kujisomea, lakini ujio wa kompyuta hizo umemrahisishia upatikanaji wa maarifa muhimu kwa ndoto yake ya kuwa mhandisi.

“Mimi nilikuwa napata changamoto sana hasa kwenye vitabu, lakini sasa tunaweza kutafuta mada muhimu kwenye kompyuta na kujifunza vizuri zaidi. Hii imerahisisha hata jinsi ya kufanya mazoezi ya maswali ya sayansi,” amesema Isaya.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Marryangel Frank amesema matumizi ya kompyuta hizo yameongeza ari ya kujifunza kwa kina na kuomba wadau wengine waige mfano wa wadau hao wa elimu kusaidia shule nyingine.

“Tunashukuru sana kwa kutuletea vifaa hivi vya teknolojia, imetuwezesha kusoma vizuri zaidi. Tunaomba juhudi hizi zisiishie hapa, bali zifike pia shule nyingine,” amesema Marryangel.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa maabara hiyo, Mkurugenzi wa Camara Education Tanzania, Dayani Mbowe, amesema lengo la mradi huo ni kusaidia wanafunzi kuendana na mabadiliko ya kisera katika elimu yanayolenga kutoa ujuzi wa moja kwa moja kwa soko la ajira.

“Tehama ni moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali. Sisi kama Camara tunaamini wanafunzi wakipewa nyenzo sahihi, wanaweza kuwa sehemu ya nguvu kazi yenye maarifa ya kisasa,” amesema Mbowe.

Uzinduzi wa chumba cha Tehama katika shule ya sekondari Igogwe iliyopo Wilaya ya Ilemela, Mwanza chenye kompyuta 26 zilizotolewa na taasisi ya Camara Education Tanzania kwa kushirikiana na Helios Towers Tanzania

Mkurugenzi Mkuu wa Helios Towers Tanzania, David Dziaba amewataka wanafunzi hao kutumia vizuri, kuzitunza na kutumia fursa ya kuvumbua maarifa mapya kupitia kompyuta hizo akidai ulimwengu wa sasa upo kwenye zama za dijitali.

Ofisa Tarafa wa Ilemela, James Chuwa, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, ameshukuru vifaa hivyo kupelekwa kwenye shule hiyo akiwataka wadau wengine waige mfano huo hasa wanaotekeleza miradi mbalimbali kwa kutoa kwa jamii inayowazunguka.

Amesema Serikali imejenga miundombinu ya shule hiyo kwa zaidi ya Sh1 bilioni ili kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Igogwe, Atanas Manyika, amesema maabara hiyo imewezesha somo la Tehama kufundishwa rasmi shuleni hapo, na kwamba walimu na wanafunzi tayari wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

Amesema kuwa shule hiyo iliyoanzishwa Julai 2022, kwa sasa ina wanafunzi 785, wakiwemo wasichana 413 na wavulana 372, huku ikiwa na walimu 28.