Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ludovick Utouh aeleza siri iliyomfanya aandike kitabu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh

Muktasari:

Hilo lilitokana na namna suala la uwajibikaji lilivyoachiwa taasisi hiyo pekee, ilhali jamii nzima inapaswa kuhakikisha dhana hiyo inatelezeka.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema kukatishwa tamaa alikokutana nako wakati wa uongozi wake kulimfanya ajione ameachwa peke yake na taasisi hiyo.

Hilo lilitokana na namna suala la uwajibikaji lilivyoachiwa taasisi hiyo pekee, ilhali jamii nzima inapaswa kuhakikisha dhana hiyo inatelezeka.

Ni sababu hiyo ndiyo imemsukuma Utouh kuandika kitabu kiitwacho ‘Uwajibikaji ndani ya kalamu isiyokuwa na wino’. Pia ukurasa wa 129 wa kitabu hicho, mkaguzi huyo mkuu wa mstaafu wa hesabu za Serikali ametoa mapendekezo ya uimarishaji wa uwajibikaji nchini.

“Kwa kipindi chote cha miaka minane cha mimi kuwa CAG, nimekuwa nikishauri Serikali, Bunge na Mahakaka kuhusu namna ya kuboresha na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, na njia bora ya matumizi yake,” alisema jana wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.

Alisema mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi ni pamoja na uimarishaji wa mifumo ya uwajibikaji na utawala bora.

Alisema inafaa kuimarisha mifumo ya ndani ya utendaji kazi na ulipwaji wa mishahara inayokidhi mahitaji muhimu ya mfanyakazi.

Vilevile lipo suala la malipo ya mishahara hewa na uimarishaji wa miundombinu nchini.

Ndani ya kitabu hicho ambacho dibaji imeandikwa na katibu mkuu kiongozi mstaafu, Ombeni Sefue na chenye kurasa 153, Utouh ameelezea mambo aliyokutana nayo katika kipindi cha miaka minane.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, alisema miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikimuumiza ni kutofuatwa kwa mapendekezo aliyokuwa akiyatoa kwa ajili ya kuleta maboresho.

Utoah ambaye kwa sasa ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, alisema pamoja na kumuumiza jambo hilo lilisababisha ajione mpweke.

Alisema,“wakati mwingine kama CAG nilikuwa najiona niko mwenyewe kwa sababu unakuja na pendekezo ambalo unaamini ndani ya moyo wako kuwa likitelekezwa litaisaidia Serikali, halafu halitekelezwi.

“Ni sababu hiyo ikanifanya niandike hiki kitabu ili kuelimisha kuhusu dhana ya uwajibikaji na kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hili suala ni letu sote. Najua fedha na nguvu niliyotumia kuandika kitabu hiki haitarudi kwa sababu Watanzania hawana utamaduni wa kusoma, ila binafsi nimesukumwa niandike kutoa elimu.”

Utoah alisema mambo kadhaa alikuwa akishauri, lakini hayakufanyiwa kazi hadi Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuyaangalia kwa jicho la tatu.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na sakata la watumishi hewa, Escrow, kutambulika kwa makao makuu ya Serikali na mgogoro wa kimasilahi unaotokana na wabunge kuingia kwenye bodi za mashirika ya umma.

Kuhusu suala la watumishi hewa, alisema kwa muda mrefu alikuwa akilitolea ushauri, lakini haukizingatiwa ila sasa baada ya hatua kuchukuliwa manufaa yameonekana kutokana na fedha nyingi kuokolewa.

Kwa upande wake, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo alisema Utoah alichangia kwa kiasi kikubwa kuifanya ofisi ya CAG kuwa taasisi imara na yenye heshima kubwa hapa nchini.

Cheyo alisisitiza kuwa uwajibikaji katika mali za Serikali ni jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa na taasisi na watumishi wote wa umma.

Alisema iliyokuwa kamati yake ilifanya kazi kwa karibu na Utouh kuifanya ofisi ya CAG kuwa chombo kinachojitegea na kusimama imara kwa ajili ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kama zilivyopitishwa na Bunge.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Asasi za Kiraia, Francis Kiwanga alisema kipindi ambacho Utoah alikuwa akiongoza ofisi hiyo kulikuwa na changamoto kubwa katika suala la uwajibikaji serikalini.