Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lori la mafuta lalipuka laua, lajeruhi 19 Dar

Wakazi wa Mbagala Charambe.Dar es salaam wakitazama lori la mafuta ambalo lilipata ajari na kuteketea kwa moto ambao pia uiunguza nyumba kadhaa usiku wa kuamkia juzi.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Alisema dereva wa lori hilo aliteremka salama na kuwaonya madereva wa bodaboda kuwa wasiguse chochote kwa sababu gari hilo lilikuwa limebeba petroli ambayo ni hatari.

Dar es Salaam. Moto mkubwa umeua mtu mmoja na kujeruhi wengine 19 waliokuwa wanachota mafuta ya petroli yaliyomwagika baada ya lori kupinduka.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 5.15 usiku wakati lori hilo liliposhindwa kukata kona kwenye mzunguko wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam na kuanguka kwenye mtaro.

Kaimu Kamanda wa Polisi Temeke, Nyigesa Wankyo alimtaja aliyekufa katika tukio hilo kuwa ni Masoud Masoud mkazi wa Mbagala Charambe.

Alisema baadhi ya majeruhi wa moto huo wamelazwa katika Hospitali ya Temeke na wengine Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Mlipuko wa tanki hilo ulisababisha taharuki kwa wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani ambao walidhani ni mlio wa bomu, kutokana na kumbukumbu ya milipuko ya mabomu katika kambi ya jeshi iliyotokea Aprili 29 mwaka 2009.

Fatma Mburalala mkazi wa Nzasa alisema juzi usiku saa 5.30 usiku ulisikika mlio unaofanana na bomu uliokuwa ukijirudiarudia.

“Wakazi wa mtaa wetu wote walitoka nje na familia zao wakidhani kwamba ni mabomu. Tuliingia ndani saa 9.00 usiku baada ya kupata taarifa kwamba ni lori limelipuka moto,” alisema.

Alisema wakazi wengi walikaa nje ya nyumba zao usiku kutokana na mlipuko huo wakidhani kuwa ni mabomu.

Kamanda Wankyo alisema mlipuko huo umesababishwa na watu waliokuwa wakiiba mafuta.

“Wezi waliiba mafuta na kwenda kuficha kwenye nyumba za jirani na ulipotokea mlipuko huo moto ukafuata mafuta yalipo na kuleta madhara,” alisema.

Wankyo alisema polisi haijafahamu thamani ya mali zote zilizoteketea kwa moto na kwamba linafanya tathmini kwa kushirikiana na wamiliki.

Alizitaja mali zilizoungua ni baa, nyumba ya kulala wageni, pikipiki saba na maduka.

Alisema dereva wa lori hilo alikimbia baada ya tukio hilo na hajapatikana na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi kutokana na ajali hiyo.

Ajali hiyo haina tofauti na ile iliyotokea mwaka 2000, na watu 42 waliungua wakati wakiiba mafuta kwenye lori lililoanguka katika Kijiji cha Idweli, wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Watu hao walizikwa katika kaburi la pamoja baada ya miili yao kuharibika zaidi na kushindwa kutambuliwa.

 

Ajali ilivyotokea juzi

Mmoja wa wakazi wa Mbagala Rangitatu, Rashid Athuman ambaye alikuwapo eneo la tukio wakati ajali hiyo inatokea alisema baada ya gari hilo kuanguka, waendesha bodaboda kwa haraka walikusanyika katika eneo hilo.

Alisema dereva wa lori hilo aliteremka salama na kuwaonya madereva wa bodaboda kuwa wasiguse chochote kwa sababu gari hilo lilikuwa limebeba petroli ambayo ni hatari.

Athuman alisema madereva hao wa bodaboda walianza kufungua betri za lori na wengine wakikinga mafuta ambayo yalikuwa yakivuja.

Alisema madereva hao walikuwa wakihamisha madumu ya petroli na kwenda kuficha kwenye nyumba za jirani na eneo hilo.

“Baada ya dakika kama 15, lori hilo lililipuka kwa mshindo mkali unaolingana na bomu.”

Alisema mlipuko huo ulisababisha lori hilo kuwaka moto na nyumba zilizopo jirani zikaanza kuungua.

Alisema wakati moto huo unashika kasi ya kuwaka, vijana hao nao walikuwa wakikimbia huku na kule wakiwa wanawaka moto, wakiomba msaada.

“Ilikuwa kama vile sinema kuwaona vijana zaidi wa kumi wakiwa wanakimbia huku na kule wakiwaka moto, wengine walijidondosha kwenye mchanga ili kuzima moto bila mafanikio,” alisema.

Shuhuda huyo alisema, “Wako vijana waliojindosha kwenye mtaro wa maji machafu ili kuzima moto, kwa ujumla hali ilikuwa mbaya jana usiku.”

Alisema vijana hao waliokolewa na polisi waliowahi kufika katika eneo hilo huku wakiziacha bodoboda zao zikiwa zinaungua kwa moto.

Walioshuhudia walisema lori hilo lilipoanguka halikuleta madhara yoyote lakini moto uliosababishwa na wezi wa mafuta ulipowaka ndipo ukaunguza nyumba mbili.

Kati ya nyumba zilizoteketea kwa moto, moja ina maduka saba na nyingine ina baa na nyumba ya kulala wageni.

Mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo mwenye duka la vipuri vya magari, Salum Mtima alisema vipuri vyote vilivyokuwamo katika duka hilo vinavyokadiliwa kuwa na thamani ya Sh70 milioni viliungua kwa moto.

“Kama unavyoona duka lote limegeuka majivu, sijakuta kitu chochote kikiwa salama,” alisema.

Mmiliki wa baa na nyumba ya kulala wageni yenye jina la United States Bar and Guest House, Deus Kasigwa alisema vitu vyote vilivyokuwa kwenye baa na kwenye nyumba ya wageni viliteketea kwa moto.

“Hakuna kilichosalimika vifaa vyote vikiwamo majokofu, viti, meza, vitanda na magodoro yaliteketea kwa moto,” alisema.

Alisema bado hajafanya tathmini ili kufahamu gharama halisi za mali iliyoteketea kwa moto.

Hospitali ya Temeke

Mganga wa zamu wa Hospitali ya Temeke, Rolester Kinunda alisema juzi saa 5:50 usiku uongozi wa hospitali hiyo ulipokea watu 20 waliojeruhiwa kwa moto na mmoja alifariki muda mfupi baadaye.

Alisema majeruhi 15 walihamishiwa Muhimbili baada ya kuwa wameungua vibaya na wanne wakiendelea kutibiwa katika hospitali hiyo.