Latra yafungia mabasi 27

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu kusitishwa kwa leseni za usafirishaji wa abiria kwa mabasi 27 kwa kipindi cha mwezi Machi. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesitisha leseni za usafirishaji wa abiria kwa mabasi 27 kwa kipindi cha mwezi Machi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesitisha leseni za usafirishaji wa abiria kwa mabasi 27 kwa kipindi cha mwezi Machi kwa madai ya kuingilia vidhibiti mwendo.
Uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa sheria za Latra kifungu cha 5 (1) (b) sura ya 413 na kanuni ya 27(1) (c) na d ya kanuni za leseni za usafirishaji wa magari ya abiria za mwaka 2020.
Februari mwaka huu mamlaka hiyo ilisitisha leseni za usafirishaji kwa mabasi 22 kwa kipindi cha mwezi Januari kwa makosa hayo.
Akizungumza na leo Jumanne Aprili 11, 2023 Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema hatua hiyo inatoakana na vitendo vya kuingilia mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari (VTS) na kusababisha mfumo kutotuma taarifa au kutuma kwa kurukaruka.
"Kuna baadhi ya mabasi baada ya wataalamu wa Mamlaka kuafanya uchunguzi, waligindua betri za vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) zimeharibiwa na mifumi yake na mifumo ya umeme kubadilishwa.
"Mabasi mengine yamekutwa yakiwa na mfumo wenye swichi inayotumiwa na dereva kuzima na kuwasha kifaa hicho," amesema Suluo.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kibaya na zaidi wanebaini yapo mabasi yaliyobadilisha mfumo na kutuma taarifa za uongo kwenye kituo cha ufuatiliaji.
"Unakuta basi linasafiri hadi linafika kwa mwendo usiobadilika, ni muhimu wamiliki wa mabasi na madereva wafahamu mfumonwa VTS una uwezo wa kutoa taarifa kwa mamlaka iwapo utaingiliwa au kuharibiwa," amesema.
Amebainisha kuwa kitendo cha kuingilia mfumo wa VTS ni ukiukwaji wa kanuni ya 51(a) na b) ya kanuni za leseni za usafirishaji magari ya abiri za mwaka 2020.
Ameitaja pia kanuni ya 51(a) inayomtaka mmiliki mwenye leseni ahakikishe basi lake limefungwa kifaa cha kufuatilia gari na kiwe kinafanya kazi vyema na kufanyiwa marekebisho na hakichezewi.
Kwa upande wake Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP, Ramadhani Ng'anzi amesema Jeshi hilo lilishatoa angalizo kama kuna basi lolote linatatizo lisianze safari.
Amesema licha ya kufungwa vifaa vya ufwatiliaji sasa wanafanya utaratibu kwaajili ya kufunga vikata mafuta (speed governor).