Kondomu za kike zapewa kisogo

Muktasari:
- Wakizungumza na gazeti hili jana, wataalamu hao walieleza kuwa mbali na changamoto hizo, gharama ya kondomu hizo imewafanya wengi kutozitumia badala yake kuwaacha wanaume kuvaa za kwa.
Miaka 19 tangu kuwapo nchini kwa kondomu za kike, wataalamu wa masuala ya uzazi wameeleza kuwa kuna changamoto ya uelewa na matumizi yake.
Wakizungumza na gazeti hili jana, wataalamu hao walieleza kuwa mbali na changamoto hizo, gharama ya kondomu hizo imewafanya wengi kutozitumia badala yake kuwaacha wanaume kuvaa za kwa.
Mtaalamu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma, Dk Wilson Lugano alisema kondomu za kike zinauzwa Sh5,000 huku za kiume ni kuanzia Sh500.
Dk Lugano alisema matumizi ya kondomu za kike na namna ya uvaaji ni changamoto na kwamba, hakuna msukumo wa kuzitangaza kwa jamii ili kuleta uelewa na matumizi, badala yake za kiume zipewa kipaumbele.
Mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na viungo vya uzazi kutoka Hospitali ya Al-Rahm Zanzibar, Dk Hafnia Makhrouk alisema nchi nyingi zimekuwa zikitoa elimu kwa jamii na kusambaza kondomu za kike kwa bei rahisi.
Dk Makhrouk alitoa mfano wa Zimbabwe ambako wanawake na taasisi za afya walifanya kampeni wakitaka zipelekwe na Serikali ilitekeleza.
Utafiti uliofanywa kujua uelewa, mtazamo na matumizi ya kondomu za kike kwa wanafunzi wanaosoma shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ulibaini zaidi ya asilimia 96 wanajua uwapo wake, lakini waliowahi kuzitumia ni asilimia nne tu.