Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA WASTAAFU: Utengano unapokuwa udhaifu wa wastaafu

KONA YA WASTAAFU: Utengano unapokuwa udhaifu wa wastaafu

Muktasari:

  • Upo mfano mmoja rahisi sana aliopata kutoa babu mmoja kwa mjukuu wake kuhusu methali ya Umoja ni Nguvu uliopata kuandikwa enzi hizo shule zilipokuwa shule kweli na riwaya zilipokuwa riwaya kweli.

Upo mfano mmoja rahisi sana aliopata kutoa babu mmoja kwa mjukuu wake kuhusu methali ya Umoja ni Nguvu uliopata kuandikwa enzi hizo shule zilipokuwa shule kweli na riwaya zilipokuwa riwaya kweli.

Nyakati hizo wengi wa wastaafu tulionao sasa ndio walikuwa wanasoma na ambao sasa kwa bahati mbaya ama kutokana na mengi waliyonayo kichwani, wameusahau. Nitawakumbusha.

Babu alichukua kijiti kimoja na kumpa mjukuu wake na kumtaka akivunje. Mjukuu akafanya hivyo kirahisi tu. Kisha babu akachukua na kuvifunga pamoja vijiti kumi vya namna hiyohiyo kama kile cha mwanzo, na kumtaka mjukuu wake avivunje. Mjukuu akakukuruka kwa nguvu zake zote lakini akashindwa kuvivunja vijiti vile na funzo la babu likawa limekamilika.

Akamueleza mjukuu wake jinsi ilivyokuwa rahisi kuvikata vijiti vile vilipokuwa kimojakimoja, lakini jinsi ilivyokuwa ngumu kuvikata vijiti vile viliposimama pamoja, kama mjukuu mwenyewe alivyothibitisha. Somo la babu la ‘Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu’ likawa limemuingia mjukuu kwa mfano hai kabisa.

Unapoangalia vilio, masononeko na maombolezo ya wastaafu wetu wa nyakati hizi ambao wengi wao, kama si wote, waliusoma mfano huo na wakauelewa vizuri nyakati hizo ambapo hadithi ilipokwisha mwalimu lazima akuulize, “hadithi hii inatufundisha nini’ na uliposhindwa kujibu sawasawa fito na makwenzi ya mwalimu vilikuhusu!

Ni bahati mbaya sana sasa kwamba wastaafu wetu wanaelekea kuwa wameshausahau mfano mwema huu alioutoa babu kwa mjukuu wake kwamba ‘Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu’!

Inashangaza si kidogo kwamba malalamiko, maumivu na masononeko ya wastaafu ni yaleyale miaka yote, lakini hayajawahi kupatiwa ufumbuzi wa kueleweka na wahusika na kibaya zaidi, hata wastaafu wenyewe.

Ukiacha hili kubwa la kucheleweshewa mafao yao baada ya kustaafu, ambalo sasa limekuwa la kawaida kiasi cha kustahili msemo wa ‘kawaida ni kama sheria’. Naam, wastaafu kucheleweshewa mafao yao sasa imekuwa kama sheria ya nchi.

Unaliangalia hili jingine ambalo pia sasa limekuwa kama ‘sheria’ ya nchi kutokana na kujirudia mara kwa mara la mstaafu kufikia wakati wake wa kustaafu, anafanya hivyo kwa amani lakini anapokwenda kupokea mafao yake kule kwa watunza vibubu vya wastaafu anaambiwa kirahisi rahisi tu kuwa mafao yake hayapo, maana muajiri wake alikuwa hayawasilishi kibubuni! Inaishia hapo. Na inakuwa maumivu kwa mstaafu huku mwajiri husika akiendelea kula mema ya nchi kwa raha zake. Mzee wetu hajapata kufahamu ni kwa nini inapogundulika tu kuwa mwajiri hakuwakilisha michango ya mwajiriwa wake na hivyo kumfanya akose mafao yake kwa wakati na hivyo kumsababishia maumivu yanayomharakisha makaburini, ni kwa nini huwa hakufanyiki moja kati ya haya mawili tu?

Ama mali za mwajiri zikamatwe na kupigwa bei ili mstaafu apate chake si zaidi ya wiki mbili au mwajiri apelekwe Keko akananihii kwenye ndoo hadi wenzake ofisini watie akili kumtafutia chap na kumlipa mstaafu chake!

Huwa hakuna linalotendeka kati ya haya mawili kwa mpango wa dharura ili kumuondolea maumivu mstaafu ambaye anaishia kwenye malalamiko, maombolezo na maumivu na sana sana udhaifu wa kijiti kimoja wa kukatwa tu na kutupiliwa mbali huko…na sana sana kuzidi kunogesha tu usemi wa ‘Kawaida ni kama Sheria’!

Mstaafu wetu anasema ndipo hapa yeye na wenzake wanapokosea. Matatizo haya yanajitokeza mara nyingi tu. Serikali inatuaminisha kwamba imeshindwa kuyapatia ufumbuzi wa kudumu, sawa, wastaafu wenyewe je, watalialia hadi lini wakingoja huruma ya mtu ili kumaliziwa shida zao? Lini, ili waajiri watie akili na kujua kuwa linapokuja suala la mstaafu, ‘chezea pengine’? Lini?

Wakati umefika sasa wastaafu kusimama pamoja kama vile vijiti kumi vya mfano wa babu na kusema kwa pamoja ‘imetosha’! Kwa Amani. Ni wakati sasa wa wastaafu kujikusanya na kuunda umoja wao wa kuwasilisha shida zao kwa pamoja kama vile vijiti 10 vya babu badala ya kila moja kupuyanga kivyake kwenye kutafuta haki zake na matokeo yake ni kuishia ‘kukatwa’ tu kama kile kijiti kimoja cha babu !

Hivi kuna kitu gani kinachozuia kuwepo kwa ‘Baraza la Wastaafu’ litakalokuwa na kazi moja tu ya kusimamia na kupambania haki za wastaafu kwa pamoja?

Kuna mabaraza mengi tu nchini. Tunaamini kwamba yote hayo yasingekuwepo iwapo wastaafu wetu wangekuwa wameweka utaratibu na kanuni njema za kuyaunda na kuyaendesha. Ni imani ya mstaafu wetu kwamba itakapofika wakati wa kuunda ‘Baraza la Wastaafu’ haitaleta shida, kwa vile litakuwa na kazi moja tu ya kupambana na changamoto zinazowakabili wastaafu likiwa kama vijiti kumi vya babu vyenye nguvu inayotokana na umoja na si kuwa kijiti kimoja cha kuvunjwa vunjwa ovyo? Wastaafu himizaneni ili muwe vile vijiti kumi vyenye nguvu kwa kuunda umoja wetu wa kusimamia masilahi yetu pamoja badala ya kila mtu kupuyanga kivyake na kuishia maumivu tu yanayomharakisha mstaafu kufikishwa Kinondoni (makaburini)!

Ni kwa Umoja na Nguvu hii ya vijiti kumi ndipo tu tutaweza hata kusimama na kudai kuwa iwe kwa Katiba Mpya ama kwa kuwekwa kiraka ile iliyopo kwamba wastaafu wanahitaji si tu Viti Maalumu bungeni kutokana na ustaafu wao, bali pia hata kanuni ya kwamba katika vile viti 15 vya ubunge wa kuteuliwa vya mkuu wa nchi, alazimike kuteua wastaafu wawili, mwanamke na mwanamume kuingia Bungeni kusimamia masilahi ya wastaafu.

Tusomane Ijumaa.