KONA YA WASTAAFU: Mstaafu, nabii asiyeheshimika kwao!

Muktasari:
Kwenye ‘Kona ya Wastaafu’ ya Ijumaa mbili zilizopita, kulikuwa na ujumbe mmoja uliomsisimua mzee wetu mstaafu na kumfariji sana kwamba angalau bado kuna watu wa kizazi hiki wanautambua na kuuheshimu mchango wake katika kuijenga nchi hii na wanaumizwa na anavyoendelea kupokea pensheni njiwa ya ‘laki si pesa’ wakati sasa hali imekuwa ngumu kwa kila mtu!
Kwenye ‘Kona ya Wastaafu’ ya Ijumaa mbili zilizopita, kulikuwa na ujumbe mmoja uliomsisimua mzee wetu mstaafu na kumfariji sana kwamba angalau bado kuna watu wa kizazi hiki wanautambua na kuuheshimu mchango wake katika kuijenga nchi hii na wanaumizwa na anavyoendelea kupokea pensheni njiwa ya ‘laki si pesa’ wakati sasa hali imekuwa ngumu kwa kila mtu!
Ameandika mjukuu yule, na mzee wetu mstaafu ananukuu, ‘Serikali ijipapase na kuwaongeza wastaafu pensheni yao ya mwezi iwe laki moja unusu ama mbili. Kwa nini isiwaongeze? Wastaafu wenyewe wamebaki wangapi?’
Ameuliza mjukuu yule mwema kwenye ujumbe wake mfupi, wastaafu wenyewe wa zamani wamebaki wangapi hadi Serikali ione itapata hasara sana ikiwaongeza pensheni yao ya ‘laki si pesa’ ambayo mara ya mwisho imeongezwa miaka 16 iliyopita?
Ndiyo, wastaafu wenyewe wamebaki wangapi katika nchi hii ya watu milioni 60 na ushee, kiasi kwamba Serikali ikiwaongeza pensheni yao ya mwezi kutoka ‘laki si pesa’ iliyopo kwa miaka 16 sasa, hadi laki tatu kwa mwezi, itakuwa inapata hasara gani?
Hii hii Serikali ambayo inaweza kutenga shilingi nyingi sana bilioni 550 kwa mwaka ili kujinunulia magari mapya na mabilioni mengine ya watu kuhomola?
Ndiyo, ni wastaafu wetu hawa wazee walioipokea nchi kutoka kwa wakoloni na kwa jasho na damu yao wakapapasa gizani kuijenga na kuifikisha ilipo.
Ndiyo, walikuwa wanapapasa! Tulikuwa tumeachiwa nchi na wakoloni na hatukuwa na moja, lakini tukapapasa gizani kwa jasho na damu na tukaifikisha nchi mlipoikuta viongozi wetu.
Mbona mnatutaka tuendelee tena kupapasa gizani hata kupata nyongeza tu ya pensheni yetu? Miaka 16, pensheni ya ‘laki si pesa’ iko palepale inapiga makitaimu?
Mzee wetu mstaafu anasikitika kwamba yeye aliyeipokea nchi kutoka kwa wakoloni na kuifikisha ilipo ameishia kuwa hapo alipo, wakati kuna wastaafu wengine waliompokea kazi wakati anastaafu kazi nao wamestaafu majuzi tu lakini sasa wanapata pensheni iliyokwenda shule na pensheni yao ya mwezi mmoja ni sawa sawa na pensheni za miezi 10 za mstaafu mstaafu! Binadamu wote ni sawa? Acha utani!
Imefikia sasa kila mstaafu wetu anaposhika gazeti na kulipitishia macho yake ya kizee, anaishia kupata msongo wa mawazo akisoma kuhusu fedha za Serikali kwa mabilioni zinavyohomolwa kushoto, kulia na katikati na kuingia kwenye mifuko ya watu binafsi kama vile hazina mwenyewe badala ya kuingia kwenye mifuko ya mstaafu wa zamani kama nyongeza ya pensheni yake!
Kwamba hakuna hata anayesimamishwa kizimbani ama kupelekwa kule ‘wanakonaniliu’ kwenye debe, inaonyesha uzembe wetu katika kuzisimamia tozo tunazokamua hata wastaafu!
Naam, yaleyale ya mjukuu wetu akiiba kuku ili kupoza njaa tunamchoma moto, lakini kibaka akiiba mabilioni ya Serikali akiwa kavaa suti tunamuimbia pambio na kumpigia makofi pamoja na kwamba naye ni kibaka tu!
Mstaafu wetu mzee anaishia kusononeka sana kwamba hata Tanganyika yao njema waliyopokea na kuikuza kwa jasho na damu na mapenzi makubwa, sasa inaishia kuwa ‘Tozonia’. Nchi ambayo tozo imekuwa ndiyo njia pekee ya kupata kodi! Kibaya zaidi ni kwamba tozo hazijamuacha salama hata yeye mstaafu!
Mstaafu anaomba twende taratibu kidogo hapo. Anajua kuwa alikatwa kodi ya mshahara kwa miezi 480 iliyo katika miaka yake 40 ya ajira. Alipostaafu na kulipwa mafao yake, yakakatwa kodi. Pensheni yake ya ‘laki si pesa’ sasa inaletwa moja kwa moja kwenye akaunti yake ya benki ambayo inachukua tozo zake.
Mstaafu akiichukua hiyo pensheni yake kupitia simu yake, mtandao wa simu yake nao unachukua chake!
Mpaka akija kuitia mkononi pensheni yake ya ‘laki si pesa’ ambayo mafao yake yalikatwa kodi kwa mshahara ambao ulikatwa kodi kwa miezi 480 aliyokuwa mwajiriwa, shilingi kama 25,000 zinakuwa zimekwishaota mbawa kutokana na tozo mbalimbali pensheni yake ya ‘laki si pesa’ ilizokumbana nazo! Hivi nchi hii hakuna mheshimiwa mwenye huruma ya kuwasikiliza wastaafu hawa! Hakuna?
Hivi waheshmiwa wa ‘Tozonia’ hawana ubunifu wa kutafuta mahali pengine pa kupata kodi badala ya kuwabamiza wananchi na tozo zisizoisha? Yaani kwenye kukamua wananchi, na wastaafu wazee na tozo zisizoisha ndio mwisho wa ubunifu wao?
Mnatuumiza wastaafu. Tuliisha lipa kodi zote. Tuongezeni pensheni, tupumzike. Na hakuna hata mheshimiwa mmoja anayeweza kusema ‘wazee wetu wa kuanzia miaka 60 wasikamuliwe tozo’!
Hakuna? Au ndio yatakuwa yale maneno ya kanga ya ‘matibabu ya bure kwa wazee wa umri zaidi ya miaka 60?’ Wazee bado wanajiuliza yalikoishia, kabla hawajabamizwa na ‘Bima ya Afya’ inayokamua zaidi ‘laki si pesa’ yao!
Uso umeumbwa na haya. Hebu waheshimiwa wetu wazivike nyuso zao haya na wawasaidie wastaafu wetu hawa wa zamani! Bila wao kukubali kuyafanya waliyoyafanya, pengine msingekuwa kwenye hivyo vyeo vya kuwaamulia nyongeza ya pensheni yao leo! Uso umeumbwa na haya!
Tuone haya wastaafu wetu wanavyosononeka kwa miaka 16 pensheni yao ya ‘laki si pesa’ iongezwe. Hakuna kitu kibaya kama sononeko la mzee. Kama tozo tulishalipa za kutosha.
0754 340606/0784 340606