KONA YA MSTAAFU: Ngoma za mstaafu zinapokaribia kupasuka!
“Kila mwenye ngoma zake acheze na zipasuke” ulikuwa msemo mmojawapo wa wahenga wetu waliokikuza Kiswahili chetu. Kwamba kila mtu ana haki ya kufanya jambo lake mradi tu hawabughudhi watu wengine.
Mstaafu wetu ana miaka sita sasa anapiga na kucheza ngoma yake ya “Kona ya Wastaafu” akiwa amefaulu kutoa ‘midundo’ mia tatu na... ya ‘ngoma’ yake hiyo aipigayo kila siku ya Ijumaa kuanzia mwaka 2021 mpaka leo 2026, akifaulu kutoa ‘midundo’ mia tatu na... pamoja na Ijumaa kadhaa kupita kimya kutokana na sababu hizi na zile, nyingi zikihusu maradhi yake ya uzee yaliyo na dalili za Kinondoni!
Mstaafu anapenda kuamini kuwa ‘midundo’ yake ya “Kona ya Wastaafu” ya kila siku ya Ijumaa haijapata kumbughudhi mtu, zaidi ya kumkumbusha kuwa anatakiwa afanye nini kwa ‘wacheza ngoma’, hususani wale wa kima cha chini ambao wametimiza miaka 40 ya maisha yao wakiwa kwenye ajira ya kuijenga na kuilinda nchi yetu hii kwa jasho na damu yao, huku wakikatwa mishahara yao kwa miaka 40. Duh...!
Mstaafu alianza kupiga ngoma zake miaka sita iliyopita wakati yeye na wastaafu wenzake walipokuwa wakipokea pensheni ya Shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi, waliyokuwa wakiipokea kwa karibu miaka 17 ya nyuma wakati kilo moja ya nyama ikiwa Shilingi mia saba na hamsini, kilo ya sukari ikiwa Shilingi mia nne na hamsini na maharage kilo Shilingi mia mbili na themanini. Ndiyo, sijakosea, ni mia si alfu! Bila shaka Ijumaa ya leo hii mnajua wenyewe bei za bidhaa hizo!
Miaka yote 17 tuliyokuwa tukipata pensheni ya Shilingi laki moja na elfu tano, si Siri-kali wala kibubu cha akiba ya wafanyakazi wala rundo la vyama visemekanavyo kuwa ni vya kuwatetea na kuwasemea wafanyakazi, hakuna ‘aliyekohoa’ japo kidogo tu kuwasemea wastaafu. Wahusika wote walijikausha kama shati la mtumba sokoni. Kimya!
Tukumbuke tu kuwa hawa wastaafu waliokatwa mishahara yao kuweka akiba ya uzeeni walikuwa sasa wakikiwezesha kibubu cha akiba zao kuwa na rundo la hela zilizokuwa zikiongezeka kila mwezi bila matumizi yoyote zaidi ya kuwangoja wastaafu wazeeke na kuanza kula matunda ya jasho lao, yaliyokuwa ni pesa ya miaka 40.
Ghafla baadhi ya wahusika wakapata wazo kuwa ile akiba ya wafanyakazi sasa imekuwa rundo hasa na limekaa tu likingoja wenyewe wazeeke. Wazo lililokuja kuwaumiza sana wastaafu likaanzia hapa, kwa wahusika kuona wanaweza kutumia rundo lile la hela ya wastaafu linalozidi kuwa rundo kila mwisho wa mwezi kufanyia kazi nyingine, kama kujenga maghorofa ya kupanga na kuuza, na hata kuikopesha Siri-kali inapokuwa na shida ya hela.
Wastaafu wenye akiba yao waliyokatwa kwa miaka 40 wakaishia kupata pensheni ya Shilingi elfu 50 na baadaye Shilingi laki moja na elfu tano na wakadumu nayo kwa miaka 17 huku kibubu kikiendelea kujenga maghorofa kwenye miji yetu nchini. Tukaanza kushuhudia sasa mstaafu akistaafu anaweza kukaa hata miezi mitatu kabla hajapata kile kilaki moja na elfu tano chake kwa mwezi, huku ‘vikwangua anga’ vikiendelea kushamiri mijini!
Hali hii ndiyo iliyofufua utashi wa mstaafu wetu wa kuamini kuwa ‘Kila mwenye ngoma zake acheze na zipasuke’ na ngoma yake kuwa ile ya ‘Kona ya Wastaafu’ ya kila Ijumaa kuwakumbusha wahusika kufanya kile wanachopaswa kufanya kwa wenye hela zao walizoaminishwa kuzitunza wakati wakiijenga na kuilinda nchi, ili ziwafae wakati wamestaafu.
Mstaafu anashukuru sana kwamba miaka mitatu tu baada ya kuanza kupiga ‘ngoma’ zake za ‘Kona ya Wastaafu’, Siri-kali iliamua kuboresha kiasi maisha ya wastaafu kwa kuwapa sasa pensheni ya Shilingi laki mbili na nusu kwa mwezi, pamoja na kuwa kuna wastaafu kadhaa bado hawaamini ‘ngoma’ ya mstaafu mwenzao imechangia sana katika hili la ‘kuboreshewa’ maisha yao! Nabii hafahamiki kwao.
“Mwenye ngoma zake acheze na zipasuke.” Mstaafu yeye baada ya miaka sita hazijapasuka, pamoja na maradhi ya wastaafu kumsibu. Zitapasuka ama kufifia kabisa pale mstaafu wa kima cha chini atakapopata pensheni ya kuboresha maisha yake kweli, na si blah blah!
Mstaafu alipwe anachostahili kweli cha pensheni ya Shilingi laki tano kwa mwezi kama si Shilingi milioni moja kwa mwezi, na apewe Shilingi milioni tano na laki tano akiwa hai, na si kibubu kingoje hadi akiwa amefariki na kuipa maiti yake pesa hiyo kana kwamba ndiyo iliyoijenga na kuilinda nchi na kukatwa mshahara...