Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA MSTAAFU: Mstaafu anapokumbuka 'sikukuu' ya Siku ya Bajeti

Miaka ilee ya sabini katikati akina sisi tuliokuwa tumemaliza kidato cha nne na akili zetu hazikutuhusu kwenda kidato cha tano, makampuni na mashirika ya umma na binafsi yalituajiri bila hata barua za kuomba, au kutafuta ajira kwa tochi, kama ilivyo sasa.

Unaambiwa tulikuwa na makampuni, mashirika na viwanda rundo, ambavyo kila mwaka viliandika barua kwa Wizara ya Elimu kutaka mamia ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne lakini akili zao hazikuhusu kwenda kidato cha tano na sita, waripoti haraka Bandari au Posta au benki au Bima au kwingineko wakaajiriwe fasta ili kuijenga nchi. 

Miezi sita au tisa tu baada ya kumaliza kidato cha nne na chuo cha shirika au kampuni husika tayari ukawa ofisa wa Shirika la Taifa la Usagishaji au wa benki na mshahara wako wa Shilingi mia… rudia hapo, Shilingi mia tatu themanini, uliokuwa ni bonge la mshahara ambao kama ulikuwa bahili uliweza kukutana na wa mwezi ujao. 

Tukashiriki kuijenga nchi kwa jasho na damu' yetu, siku yetu kubwa ikiwa Ile ya May Day ambayo Baba ya Taifa alikuwa na kawaida ya kutangaza nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi, potelea mbali kwamba ingeweza kuwa Shilingi mia moja na kumi au mia moja ishirini tu! Tuliridhika. Tulikuwa tunaijenga nchi.

Ninakumbuka Baba wa Taifa alilazimika kuacha kutangaza nyongeza ya mishahara mara mbili tatu tu Nnyakati zile za miaka ya mwishoni mwishoni ya 70 tulipokuwa kwenye vita ya kumtimua jirani yetu Nduli Iddi Amin Dada wa Uganda, ambaye alikuwa ameivamia nchi yetu na kudai kuwa sehemu kadhaa za mkoa wa Kagera zilikuwa ni zake. Hatukumkawiza.  Aliishia kukiona ‘Cha mtema kuni’.

Baba wa Taifa akatutaka wananchi tukaze mikanda ya suruali zetu vyema kwa miezi 18 ili kuijenga upya nchi. Tukaikaza kweli mikanda ya suruali zetu, mahati mbaya miezi 18 ikawa miaka 18 na zaidi iliyofuata. Utamaduni wa Raisi kutangaza nyongeza ya mshahara kwa waajiriwa wake sasa ukawepo kama haupo.

Sasa utaratibu umefikia hapa pa kumpa pole Mheshimiwa kwa kutotangaza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wake na sio kwa kutoa pole kwa waajiriwa waliokosa nyongeza za mishahara na kuishia kuambiwa jambo lao na Mheshimiwa litafanyika baadaye.

Hata Ile 'sikukuu' kubwa ya Siku ya Bajeti ambayo tuliokuwa wanamichezo miaka Ile ya kuijenga nchi, tulisimamisha hata mazoezi siku hiyo na kukaa kwenye vijiwe vyetu na redio zetu za mkulima za 177 na 277 za mbao, ili kumsikiliza mtoa bajeti mhusika aliyeingia bungeni kwa miguu na kibegi chake kilichoandikwa neno moja la 'Bajeti' tu akitufafanulia nani angepata nini. CAG alikuwa bado yupo Ssayari ya Pluto.

Tumestaafu na nyakati hizi tunaishia kuangalia kwa huzuni tu mhusika wa Bajeti akifika panapohusika na msururu wa magari ya bei mbaya kama Raisina yule CAG aliyekuwa Pluto enzi zile sasa ameishawasili duniani, na hasa yupo hapa nyumbani na kila mara akitueleza tunavyolazimika kukaza zaidi mikanda yetu huku wachache wetu wakilegeza yao kufiti matumbo yao.

'Sikukuu' ya Bajeti sasa imekuwa siku ya huzuni kwa mstaafu wa Kima cha Chini cha Shilingi laki mbili na hamsini kwa mwezi badala ya angalau Shilingi Laki Tano kwa mwezi, ambayo kwa utashi tu wa wanaopaswa kuhusika, inawezekana....

.... hujiuliza sana kwa nini isiwezekane kwa nchi hii aliyoijenga mwenyewe na kuifikisha mahali pa asemekanaye kuwa ni mwakilishi wa wananchi, akiwemo huyu kima cha chini mwenyewe,  apate mshahara wa shilingi milioni...mama wee… milioni 14 na marupurupu na marapurapu yake mengine kwa mwezi, wakati yeye wa kima cha chini aliyeijenga nchi hii kwa jasho na damu yake akiishia kupata Shilingi laki mbili unusu, bila hata marapurapu yoyote, kwa mwezi.

Msimshangae mstaafu wetu wa kima cha chini anapoamua kwenda kumfundisha  kucheza 'bao' mjukuu wake badala ya kusikiliza 'sikukuu' ya Bajeti kama zamani. Ni maumivu tu kwake.


0754 340606 / 0784 340606