Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipato chatajwa changamoto kwa mawakili vijana

Wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa mawakili vijana (AYL), Denis Bwana (kulia) na Emmanuel Ukashu (kushoto) na wakitoa hoja zao katika mdahalo uliyofanyika jijiji Dar es Salaam leo Julai 20, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wasema Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimepoteza mwelekeo wake kutokana na kutotatua changamoto za wanachama wake wala kuishauri Serikali.
no

Dar es Salaam. Wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Mawakili Vijana chini ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), wamesema tatizo kubwa linalosumbua vijana mawakili ni ukosefu wa kipato na kukatwa holela kwenye shughuli zao na kukosa utetezi.

Kutokana na mambo hayo, wamesema TLS imepoteza uelekeo kwa kushindwa kutoa msaada kwa wanachama wake na kuishauri Serikali kwenye mambo yanayoonekana hayapo sawa.

Wagombea hao wawili, Denis Bwana na Emmanuel Ukashu wameainisha mambo hayo leo Julai 20, 2024 wakati wa mdahalo wa kueleza nini watakwenda kufanya kwa mawakili vijana endapo watachaguliwa kuwatumikia.

Akijinadi mbele ya wapiga kura, Bwana amesema vijana mawakili wanalazimika kugonga mihuri yao kwa wateja kwa Sh5, 000 badala ya Sh20, 000 kutokana na kipato duni.

"Mawakili vijana hawana fursa, vijana wanashindwa kutumia maarifa waliyonayo  kuwa fursa, madalali wanapata fedha nyingi kuliko mawakili ni lazima sisi viongozi tunaochaguliwa kusaidia mawakili vijana kukuza uchumi wao," amesema.

Bwana amesema TLS imewatelekeza wanachama wake kwani hata changamoto ya Mawakili vijana kukamatwa kiholela hakuna msaada wowote wanaoupata kwa TLS badala yake wanachama husaidiana wenyewe kwa wenyewe.

Hatua hiyo ndiyo anayoitafsiri Bwana kuwa TLS tayari imepoteza mvuto kwani haitekelezi majukumu yake kuishauri Serikali, kutetea jamii na wanachama wake hivyo kama kijana atakwenda kupigania TLS kurudi kwenye misingi yake.

"TLS haionekani ikifanya utetezi wananchi, kusimamia haki za watu ndio maana ni ngumu kutetea wanachama wake, naweza kusema TLS ipo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) yanapotokea matukio utaona mashirika binafsi yakitoa matamko kulaani lakini TLS haizungumzi kutokana na manufaa ya mtu binafsi" amesema.

Mgombea mwingine katika nafasi hiyo Emmanuel Ukashu naye amesema suala la uchumi wa mawakili vijana ndio jambo atakalolipa kipaumbele.

Amesema wapo zaidi ya vijana mawakili 8,000 ambao atahakikisha fursa zilizopo ndani na nje ya nchi wanachangamkia.

"Mawakili vijana hawaendi kwenye mafunzo kwa vitendo, urejeshwaji wa leseni ni changamoto kutokana na kipato hivyo suluhu kwenye haya lazima nisimamie," amesema.

Ukashu amesema kwa mawakili ambao hawatakwenda kufanya kazi mahakamani watawapa fursa ya kuwaingizia kipato ikiwamo utoaji wa msaada wa kisheria kwenye jamii, ufanyaji tafiti.

Kuhusu ukamataji wa mawakili, Ukashu amesema ni kero nyingine ambayo hawapati msaada TLS jambo linalowafanya mawakili vijana kutafuta msaada wenyewe akisema njia ya kutatua kero hiyo ni kuleta programu kusaidia mawakili vijana kwenye changamoto wanazopitia.

"Tatizo la ucheleweshaji wa mihuri kwa mawakili vijana tutaweka muda wa ukomo Wakili kupewa kitambulisho na muhuri wake, tutatengeneza mfumo ndani ya TLS utakaokuwa rafiki kwa vijana," amesema.

Mdahalo huo ni sehemu ya wagombea kunadi sera zao kuelekea uchaguzi Mkuu wa TLS utakaofanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma na awamu ya pili ya mdahalo wa vijana wagombea urais nao watanadi sera zao kwenye ngwe ya pili ya mdahalo huo.

Wagombea wa nafasi ya urais TLS ni waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, 2024, ni Ibrahim bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba.