Kinana atua Katavi, awapa ujumbe wanawake, vijana

Muktasari:
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Abdulrahman Kinana leo Jumatatu ameanza ziara yake katika Mkoa wa Katavi kisha atakwenda Rukwa, Songwe na Mbeya.
Katavi. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Abdulrahman Kinana amewataka wanawake na vijana wa chama hicho kujitosa kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kukijenga chama hicho.
Kinana ameyasema hayo leo Jumatatu Julai 25, 2022 wakati akiwasilia wakazi wa Katavi baada ya kuzindua mradi wenye thamani ya Sh65 milioni wa vibanda 15 vya fremu za biashara vilivyojengwa na chama hicho ngazi ya mkoa.
Makamu huyo mwenyekiti amesema hayo katika siku ya kwanza ya ziara yake Katavi kisha atakwenda Rukwa, Songwe na kumalizia Mbeya.
Kinana amesema kundi hilo linategemewa kuleta mageuzi ya kimaendeleo hivyo linapaswa kuchukua fomu kuwania nafasi kila unapofika wakati wa uchaguzi badala ya kuendelea kuwaachia wazee kuwania nafasi hizo.
"Wakati huu ni wa uchaguzi, wagombea ni wengi na mimi nichukue fursa hii kuwaomba akina mama chukueni fomu pambaneni na hao wanaume na vijana, chukueni changamoto chukueni fomu mgombee," amesema

Amesema chama hicho mfumo wa uongozi si usulutani na uchaguzi umekuwa ukifanyaika ili kupata watu wapya wenye nguvu na Kasi ya kuendeleza uhai wa chama.
Uchaguzi wa chama hicho kwa sasa uko ngazi ya wilaya, mikoa na taifa kwa nafasi mbalimbali ambapo shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu utahitimishwa Agosti 10, 2022.