Keysha: Mama Asimwe anahitaji matibabu ya kisaikolojia

Mbunge Keisha akiweka shada la kumbukumbu kwenye Kaburi la Asimwe Novath (2) nyumbani kwao Kamachumu Muleba.
Muktasari:
- Keysha ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) amesema, Judith Richard (20) mama wa mtoto mwenye ualbino aliyeuawa, Asimwe Novath, anahitaji matibabu ya kisaikolojia na afya ya akili baada ya tukio hilo lililomfika mwanawe.
Muleba. Mbunge wa Viti Maalumu kundi la watu wenye ulemavu, Khadija Taya maarufu Keysha, ameiomba Serikali kumsaidia matibabu ya kisaikolojia, Judith Richard (20), mama wa mtoto aliyekuwa na ualbino, Asimwe Novath aliyeuawa kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake hivi karibuni.
Mei 30, 2024 saa 2:30 usiku, Asimwe (2) aliporwa mikononi mwa mama yake akiwa amekaa ndani ya nyumba yake katika Kijiji cha Bulamula wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.
Ilipofika Juni 17, 2024 kiroba cha sandarusi chenye mabaki ya viungo vyake, kilipatikana kikiwa kimetelekezwa chini ya karavati Barabara ya Ruhanga Makongora na kuzikwa nyumbani kwao Juni 18, 2024.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Julai Mosi, 2024 baada ya kufika nyumbani kwa mama huyo kwa ajili ya kutoa pole, Keysha amesema hayupo sawa na anahitaji msaada wa kisaikolojia.
"Naomba Mama Samia (Suluhu Hassan), Rais wangu, msaidie mama Asimwe hayuko sawa kisaikolojia, kwa kipindi hiki anahitaji matibabu ya afya ya akili. Naomba Wizara ya afya imsaidie mama huyu anaumia, ana mawazo sana,”amesema Keysha.
Aidha, amemshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kauli aliyoitoa Juni 2024, 2024 bungeni.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwa niaba ya Serikali anaviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya upelelezi wa kina na kuwabaini wahusika wa mauaji hayo ili hatua za sheria zichukuliwe dhidi yao.
Majaliwa pia alitaja mikakati ya Serikali ya kukabiliana na matukio ya ukatili hasa kwa watu wenye ulemavu ikiwemo Polisi Kata kutembelea mara kwa mara maeneo wanayoishi watu hao kwa lengo la kupata taarifa zao na kutambua mapema viashiria vya kihalifu sambamba na kuwapa elimu ya kuwabaini wenye nia ovu dhidi yao.
Hata hivyo, watuhumiwa tisa wa mauaji ya mtoto huyo akiwemo baba yake mzazi, Novath Venant tayari wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutekeleza mauaji hayo.
“Naishukuru sana Serikali yangu kwa namna ilivyotuunga mkono kwenye suala hili, ila hawa viumbe ni wa ajabu, kila mara wanatufanyia ukatili huu, hasa pale unapokaribia uchaguzi ili kudai wanasiasa ndio wanahusika na jambo hilo la kutunyofoa viungo, jambo mbalo siyo sawa,” amesema Keysha.
Akizungumza huku akilia kwa uchungu, mama yake marehemu Asimwe, ameishukuru Kampuni ya Mwananchi inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa namna ilivyoripoti tukio hilo tangu siku ya kwanza na kuufanya umma ufahamu kilichotokea.
“Ndugu zangu na watu mbalimbali walikuwa wananiambia Mwananchi limeandika kutekwa kwa mwanangu, kila habari ikitoka walikuwa wananiambia na kunipa moyo Asimwe tutampata, tumempata lakini marehemu,” amesema Judith huku akibubujikwa machozi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Erasto Sima ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba amesema Serikali itaendelea kumsaidia Judith mpaka itakapoona ametengaa.
“Tunajua huyu mama anapitia wakati mgumu sana, tuzidi kumuombea Mungu amjaalie kulishinda hili, na sisi Serikali tunamhakikishia tuko naye pamoja tutaendelea kumsaidia,” amesema Sima.