Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MKE WA BILIONEA MSUYA: Shahidi aeleza walivyowanasa watuhumiwa

Mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita

Dar es Salaam. Shahidi wa 22 katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya inayoendelea kusikilizwa, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam namna walivyowakamata washtakiwa, kutambuliwa na kile walichokisema baada ya kuhojiwa.

Amedai kuwa mmoja alikiri kuhusika na mauaji hayo na mwingine alikana.

Shahidi huyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi (SSP) David Paulo Mhanaya, alieleza hayo jana alipokuwa akitoa ushahidi wake kwa siku ya pili.

Itakumbukwa kuwa Aneth alikuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani eneo la Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam na mwili wake ulikutwa ndani ya nyumba yake ukiwa mtupu, huku nguo yake ya ndani ikiwa pembeni ya mwili wake.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103/2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki ni Miriam Steven Mrita, ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya, na mwenzake Revocatus Everist Muyalla.

Katika ushahidi wake juzi akiongozwa na mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, shahidi huyo aliieleza mahakama yale aliyoelezwa na aliyekuwa binti wa kazi wa marehemu Aneth, Getruda Peniel Mfuru kuhusu matukio kabla ya mauaji ya mwajiri wake.

Katika mwendelezo wa ushahidi wake, jana Mhanaya aliieleza mahakama jinsi walivyoyafanyia kazi maelezo ya binti huyo wa kazi mpaka wakawakamata washtakiwa jijini Arusha kwa nyakati tofauti.

Mhanaya alidai mshtakiwa wa kwanza, Miriam alikiri mbele ya askari polisi aliyemhoji na mbele ya Mlinzi wa Amani, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala Pangani, kutoa fedha ili kufanikisha mauaji hayo.

Pia alidai mshtakiwa wa pili, Muyella alipohojiwa na polisi alikana kuhusika na mauaji hayo, lakini alitambuliwa na binti wa kazi wa marehemu Aneth wakati wa gwaride la utambuzi.

Hivyo alieleza kuwa walimchukua mtuhumiwa sampuli ya mpanguso wa mate ukapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa uhusiano wa vinasaba na vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio ambavyo ni kisu, filimbi na nguo ya ndani ya marehemu.

Alisema matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwepo kwa uhusiano kati ya vinasaba vya kwenye mpanguso wa mate ya mshtakiwa huyo na vinasaba katika baadhi ya vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio.

Pia, alidai Julai 23,2016 Getruda akiwa nyumbani kwao Masama Moshi, alipigiwa simu na askari Sajenti Jumanne na Koplo Lenatha wakakubaliana wakutane na alifanya hivyo na wakaongozana hadi Moshi mjini.

Julai 24, 2016 Getruda alipelekwa kituo cha Polisi Chang'ombe, Temeke Dar es Salaam na Julai 25, 2016, Mhanaya akafanya naye mahojiano, baada ya uchambuzi aliona Getruda hastahili kuwa mshtakiwa, bali shahidi, hivyo alimueleza Ester amuandikie maelezo yake kama shahidi.

Agosti 4, 2016, Mhanaya alidai yeye na timu yake wakaanza safari kuelekea Arusha kufanya upelelezi kuhusu mtuhumiwa huyo aliyekuwa ametajwa na Getruda.

Alidai siku hiyo hiyo kati ya saa moja na saa 1:30 usiku walipata taarifa kuwa mtuhumiwa waliyekuwa wanamfuatilia alikuwa maeneo ya Tembo Club.

Hivyo alimtuma DC Ratifa Chiko, kwenda kumchukua na alipofika Mhanaya alijitambulisha kwake kwa cheo chake cha wakati huo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) na majina yake na alimfahamisha kuwa anatuhumiwa kwa mauaji katika jalada la kesi ya mauaji namba KGB/3849)2016 kosa la mauaji ya Aneth Elisaria Msuya.

Alimtaka mtuhumiwa pia ajitambulishe, naye akajitambulisha kwa jina la Miriam Steven Mrita.

Kisha SSP Mhanaya alimchukua mpaka ofisi ya RCO Arusha ambako walifika majira ya saa mbili usiku.

Mhanaya alimtaka mtuhumiwa awaongoze kwenda nyumbani kwake eneo la Sakina.

Alimtafuta mjumbe wa eneo hilo na shahidi huru wa upekuzi aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Sabore ambaye alimtaka amhakikishie kama walikuwa na kitabu cha upekuzi.

Alidai alifanya hivyo sambamba na kumueleza kusudio la kufanya upekuzi huo na walianza upekuzi saa 6 mpaka saa 8:41 usiku wa kuamkia Agosti 6, 2016.

Alidai katika upekuzi huo walipata nguo, suti za kike, mkufu wa dhahabu, kadi mbalimbali za magari, likiwamo lenye namba T429BYY Range Rover Ivok rangi ya Silver na simu tatu.

Kisha Mhanaya alimtaka mtuhumiwa Miriam awaonyeshe hayo magari, lakini alimwambia yameegeshwa kwenye hoteli ya SG anayoimiliki.

Wakaelekea huko na mtuhumiwa aliwaonyesha magari hayo, ikiwemo Range Rover Ivok na Suzuki Vitara (rangi nyekundu) isipokuwa gari aina ya Ford Ranger lenye rangi ya dark blue, ambalo mtuhumiwa alisema halikuwepo hapo kwa sababu lilikuwa bovu na limepelekwa CMC -Cooper Motors.

Baada ya hapo, Katabazi naye alifika hotelini hapo na kuelekeza kuwa yeye atasimamia suala la vielelezo vya magari na atavituma Dar es Salaam, hivyo akawataka Mhanaya na timu yake watangulie na mtuhumiwa.

Agosti 6, 2016 asubuhi, Mhanaya na timu yake sambamba na mtuhumiwa Miriam walianza safari ya kurejea Dar es Salaam.

Agosti 7, 2016 asubuhi, Mkuu wa Upelelezi Wilayani Temeke, SSP Mchomvu alimteua DC Mwajuma kumhoji mtuhumiwa (Miriam).

Asubuhi wapelelezi walikutana kupeana taarifa na wakaelezwa kwamba mtuhumiwa alihojiwa na akakiri kuhusika na tukio la mauaji kwa kutoa fedha Sh20 milioni ili mauaji hayo yaweze kutekelezwa na akamtaja mtu anaitwa Ray anayeishi Olasiti, Arusha kwamba ndiye aliyempa fedha hizo ili kutekeleza mauaji hayo.

Siku hiyo (Agosti 7, 2016) majira ya jioni mtuhumiwa Miriam Steven Mrita alifanyiwa gwaride la utambuzi na alitambuliwa na Getruda.

Agosti 10, 2016, mtuhumiwa alipelekwa kwa Mlinzi wa Amani Leonia Kajumlo, katika Mahakama ya Mwanzo Ilala, Pangani ambako mtuhumiwa alitoa maelezo yake ya ungamo kuhusu tukio hilo.

 Agosti 19, 2016, mtuhumiwa (mshtakiwa wa pili, Muyella) alikamatwa na siku hiyohiyo SSP Mhanaya na timu yake walikwenda kumchukua. Walifika Arusha kwenye saa 7 usiku.

Baada ya kukabidhiwa mtuhumiwa SSP Mhanaya alijitambulisha kwake, akamueleza dhumuni la kwenda hapo na akamtaka mtuhumiwa ajitambulishe, naye akajitambulisha kuwa anaitwa Revocatus Everist Muyella au Revoo au Ray.

SSP Mhanaya alipomhoji alibaini kuwa alikuwa hajapekuliwa, hivyo alilazimika kufanya upekuzi wa dharura. Alimtaka mtuhumiwa ampeleke nyumbani kwake Olasiti.

Huko alimtafuta na kupata mashahidi huru Ruth Katy na Boniface Mathew.

Katika upekuzi huo walipata vitu mbalimbali, ikiwemo bastola aina ya Canick briefcase na simu kadhaa.

Aliviorodhesha vitu hivyo kwenye hati ya dharura mbele ya mashahidi wote akasaini na kuwapa mashahidi hao ambao pia walisaini pamoja na mtuhumiwa.

Pia maelezo ya mashahidi walioshuhudia yaliandikwa palepale.

Walirudi kituoni na SSP Mhanaya alimuelekeza DC Hassan amhoji mtuhumiwa na DC Hassan alimueleza SSP Mhanaya kwamba mtuhumiwa amekanusha kuhusika na tukio la mauaji hayo.

Siku hiyohiyo wakiwa na mtuhumiwa Ray walianza safari kurejea Dar es Salaam.

Agosti 21, 2016 mtuhumiwa alifanyiwa gwaride la utambuzi na alitambuliwa na shahidi Getruda.

Katika kutafuta ushahidi zaidi mtuhumiwa huyo alichukuliwa sampuli ya mpanguso wa mate ambayo ilipelekwa kwa Mkemia wa Serikali ili kulinganisha na vielelezo vilivyopatikana aneo la tukio kuona kama anahusika au hahusiki.

Baadaye walipata matokeo kutoka Mkemia wa Serikali kwamba mtuhumiwa vinasaba vyake vilipatikana kwenye vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio.

Akisoma hati ya upekuzi aliyoijaza baada ya kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa (mshtakiwa Muyella) alisema kuwa miongoni mwa vitu vilivyopatikana ndani kwake ni pamoja na bastola, simu, briefcase na hati ya kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya madini ya marehemu Msuya (Bilionea Msuya).

Kesi hiyo inaendelea tena leo na shahidi huyo ataendelea kutoa ushahidi wake.