KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Asimulia mateso msituni akishinikizwa kukiri kosa

Miriam Steven Mrita, mjane marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; akiwa na Wakili wake Peter Kibatala
Muktasari:
- Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita, ametoa simulizi ya madai ya jinsi alivyokuwa akipelekwa msituni na kuteswa na askari Polisi waliomkamata wakimshinikiza akiri kosa la kumuua wifi yake.
Dar es Salaam. Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita, ametoa simulizi ya madai ya jinsi alivyokuwa akipelekwa msituni na kuteswa na askari Polisi waliomkamata wakimshinikiza akiri kosa la kumuua wifi yake.
Pia Miriam amekana madai ya kuwa na ugomvi na wifi yake huyo marehemu Aneth Elisaria Msuya, kuhusiana na wa mirathi ya marehemu mumewe Bilionea, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.
Badala yake amedai kuwa ingawa Aneth hakuwa mmoja wa wanufaika wa mirathi hiyo ambayo yeye (Miriam) ndio alikuwa msimamizi kabla hajabadilishwa, lakini aliamua kumgawia sehemu ya urithi huo kwa upendo tu.
Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.
Lakini Miriam amedai kuwa alipokamatwa na askari Polisi mkoani Arusha Agosti 6, 2016, aliletwa Dar es Salaam na kwamba akiwa katika kituo cha Polisi Airport, aliteswa sana na kisha akapelekwa msituni kwa nyakati tofauti ambako aliteswa na askari Polisi waliomkamata ili akiri kumuua wifi yake.
Ametoa madai hayo leo Alhamisi, Oktoba 26, 2023 katika mwendelezo wa utetezi wake katika siku ya tatu mfululizo, katika kesi ya mauaji ya wifi yake huyo, Aneth, inayomkabili yeye na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu kama Ray.
Amekuwa akijibu madai mbalimbali yaliyotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kuhusiana na tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Mateso msituni
Akiongozwa na Wakili wake, Peter Kibatala, Miriam amedai kuwa akiwa mahabusu kituo cha Airport, asubuhi ya Agosti 9, 2016, SSP Mhanaya alifika kituoni hapo akiongozana na Jumanne Malangahe na WP Ratifa Chiko na kwamba mchana walimchukua wakamuingiza ndani ya gari wakafunga kitambaa usoni kisha gari ikaanza kutembea.
Kwa mujibu wa Miriam, baada ya kutembea umbali fulani gari ilisima wakamshusha, ambapo WP Ratifa akafungua kitambaa, na akajikuta yuko katikati ya pori hivyo wakamhoji kwa nini nilimuua Aneth, huku wote wakiwa na bastola huku Mhanaya akiwa anamgongagonga kichwani kwa kitako cha bastola.
Kisha Mhanaya alimuuliza kama anapafahamu mahali hapo naye akasema hapafahamu na Mhanaya akasema sasa hapao hata wakimuua hakuna ndugu yake yeyote anayefahamu.
Baada ya kipigo hicho walimfunga tena kitambaa usoni wakamrudisha kwenye gari ikaanza safari na alifunguliwa kitambaa akiwa kituo cha Airport, ambapo walimshusha kwenye gari wakamuingiza mahabusu.
Kesho yake, Agosti 10 mchana Mhanaya, Malangahe na Ratifa Chiko, walimchukua wakaingia naye kwenye chumba kingine, ambako alianza kupigwa huku akiulizwa kwa nini alimuua Aneth lakini yeye akasema hajamuua.
Baadaye walimrudisha mahabusu na kesho yake tena Agosti 11, 2016, mchana walimchukua wakampeleka tena msituni wakaanza kumpiga na Mhanaya akauliza kama kuna chupa kwenye gari aingiziwe kwenye makalio huku Ratifa akisema au achomwe na bisibisi sehemu za siri ili akiri kwamba amemuua Aneth.
Baada ya kumpiga sana alipandishwa tena kwenye gari wakaenda mpaka maeneo ya Chalinze na muda huo ilikuwa ni usiku na baadaye wakamrudisha kituo cha Airport.
Magawo wa mirathi ya Bilionea Msuya.
Amedai kuwa akiwa msimamizi wa mirathi hiyo aliigawa kwa wanufaika wote mbele ya Wakili John Mseru, wa Kampuni ya uwakili ya Royal Attorneys, wa Arusha.
Amedai kuwa mgawanyo huo ulifanyika mbele ya mashuhuda mbalimbali ambao ni Elisaria Elia Msuya (baba wa marehemu), Ndeshukurwa Elisaria Msuya (mama wa marehemu), na dada wa marehemu ambao ni Happy, Natujwa, Ester, Joyce na yeye mwenyewe.
Miriam amewataja wanufaika wa mirathi ya Erasto Msuya kuwa walikuwa ni watoto wa marehemu Erasto Msuya, Glory, Kelvin, Maurine, Calvin; wazazi, Elisaria Elia Msuya na Ndeshukurwa Elisaria Msuya, pamoja na yeye Miriam Erasto Msuya.
Shahidi wa 22 wa upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha kwa sasa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Mhanaya ndiye aliyekuwa Kiongozi wa timu ya wapelelezi wa kesi hiyo.
Katika ushahidi wake pamoja na mambo mengine alidai kuwa Miriam alikula njama kumuua wifi yake Aneth kwa sababu ya mgogoro wa mirathi na kwamba mshtakiwa alidai kuwa Aneth alikuwa akimtumia ujumbe wa simu (sms) za kumkashifu kuhusiana na umbile lake.
Kutokana na ushahidi huyo Miriam ameulizwa na Wakili Kibatala kuwa kama ni hivyo kwa nini alikwenda kuwagawia urithi kina Aneth, ndipo akajibu kuwa ingawa hawakuwa wanufaika lakini aliwagawia kwa upendo, huku akikana kuwa na ugomvi naye.
Kuhusu kuondolewa katika usimamizi wa mirathi hiyo mwaka 2019 amedai kuwa mahakama katika uamuzi wake imesema kuwa aliondolewa kutokana na kuchelewa kuwasilisha mahakamani mrejesho wa mgawanyo wa mali.
Amedai kuwa sababu nyingine alisema kuwa mahakama ilisema kuwa ni kwa sababu alikuwa mahabusu (Segerea) asingeweza kutekeleza majukumu yake.
Hivyo amedai kuwa baada ya kuondolewa waliwekwa watoto wake Kelvin na Glory ambao waliendelea kuanzia mahali alipokuwa ameishia yeye na kwamba walikuta mali zote zikiwemo magari fedha na viwanja vikiwa sawa na Mahakama iliridhika.
Kuhusu meseji baina yake na marehemu Aneth, amedai kuwa hakuna shahidi yeyote wa Jamhuri ambaye ameleta ushahidi wa meseji walizokuwa wanajibizana na Aneth.
“Mheshimiwa Jaji simu zangu wanazo wao askari na kulikuwa na wapelelezi na kama kulikuwa na ukweli wa kutumiana meseji mashahidi wa upande wa mashtaka wangeuleta maana simu zangu wanazo na simu za Aneth wanazo, kwa hiyo ushahidi wao ni wa uwongo Mheshimiwa Jaji,” amesema Miriam na kuongeza;
“Hakuna shahidi yeyote kuanzia wa kwanza mpaka wanafunga shahidi wa 25, hakuna aliyeleta ushahidi kwamba mimi nilikuwa na ugomvi wowote na marehemu Aneth.”
Maelezo ya ungamo
Kuhusu maelezo yanayodaiwa kuwa ni yake yaliyoandikwa na shahidi wa kwanza upande wa mashtaka WP Mwajuma kwa maelekezo ya aliyekuwa RCO wa Temeke wakati huo SSP Richard Mchomvu Miriam amesema kuwa si ya kweli.
Amedai kuwa hata RCO Mchomvu mwenyewe alisema katika ushahidi wake kwamba hajawahi kutoa malekezo hayo kwa WP Mwajuma kuandika maelezo yake.
“Kwa hiyo hayo maelezo wanajua wenyewe walikoyatoa kwa sababu haiwezekani huyu aseme hivi huyu anakataa.”
Kuhusiana na madai ya kukiri katika maelezo hayo kubadilisha umiliki wa magari mbalimbali na viwanja, amekana akidai kuwa kama kweli alikiri, mpaka upande wa mashtaka wanafunga ushahidi hakuna mahali ambapo wameleta ushahidi kuthibitisha kukiri kubadilisha umiliki wa magari na viwanja.
Kuhusu maelezo ya kumpigia simu Getruda Mei 20, 2016 kwenda kupanga njama za mauaji hayo, amedai kuwa si kweli kwani katika ushahidi wake Getruda hakuna mahali ambako ametaja hiyo tarehe kwamba alikwenda Kigamboni.
Amedai kuwa hata Mhanaya (mpelelezi mkuu) katika ushahidi wake hakuongelea tarehe hiyo.
“Hivyo hizo taarifa wanajua wenyewe walikozitoa hao walioandika maelezo hayo”, amesema Miriam.
Kuhusu madai ya Getruda katika ushahidi wake kuwa alimtishia kwa bastola, amesema katika maelezo hayo yanayodaiwa kuwa ni yake, hajaona mahali ambako wameandika kuwa alikiri kumtishia kwa bastola Getruda.
Amesisitiza kuwa madai hayo ni ya uwongo kwani kama kweli angekuwa amemtishia angetoa taarifa hata kwa bosi wake ambaye walikuwa wanaishi vizuri kama alivyoeleza au mahali kote alikokuwa akizunguka hata baada ya tukio (mauaji ya mwajiri wake).
Miriam amedai kuwa maelezo ya Getruda na Mhanaya kwamba alikwenda Kibada kwa Aneth Mei 15, 2016, na gari lake akamuuliza na Getruda nyumbani kwa Aneth na kujitambulisha kwake kuwa ni ndugu yake na Aneth, si ya kweli kwani Getruda alishindwa kuthibitisha kuwa gari aliyokwenda nayo.
Badala yake amedai kuwa gari yake ni mbovu na iko gereji.
Pia alidai kuwa kama kweli alijitambulisha kuwa yeye ni ndugu yake na Aneth basi Getruda angemwambia Aneth kuwa amekutana na ndugu yake.
Kuhusu saini iliyoko katika maelezo hayo ambayo inadaiwa kuwa alisaini kuthibitisha maelezo hayo si yake na kwamba hakuna shahidi yeyote aliyeleta uthibitisho wa nyaraka au wa aina yoyote kuhusiana na hiyo saini kwamba ni yake.
Pia alidai kuwa hakuna shahidi aliyekuja kuthibitisha madai kuwa alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya mipango ya kumuua Aneth na kwamba alilala Frances Hotel Sinza.
Kesi hiyo itaendelea kesho ambapo Miriam ataendelea na ushahidi wake kabla ya kuhojiwa na mawakili wa upande wa mashtaka
Siri iliyojificha
Miriam ambaye ni Shahidi wa kwanza upande wa utetezi aliieleza mahakama kuna siri iliyojificha kuhusu upatikanaji wa aliyekuwa binti wa kazi wa marehemu Aneth, Getruda Peniel Mfuru, baada ya mauaji hayo kutokea.
Getruda ni Shahidi wa 25 na wa mwisho upande wa mashtaka, ambaye ndiye anaonekana kuwa Shahidi muhimu kwani ndiye aliyedai kuwa washtakiwa walimtaka aondoke nyumbani siku ya tukio ili watekeleze kazi yao na kumuahidi kumpa mabilioni ya pesa.
Miriam amedai kuwa ni jambo la kushangaza kwamba polisi Temeke ambalo ni Jeshi lenye nyenzo na teknolojia lilishindwa kumpata binti huyo kama aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Polisi (RCO) Temeke, Richard Mchomvu alivyosema katika ushahidi wake lakini mama wa marehemu Ndeshukurwa Msuya akiwa nyumbani ndio akampata.
"RCO Mchomvu alidai kuwa walimtafuta Getruda kwenye simu yake lakini hawakupata lakini Gatruda katika ushahidi wake alidai kuwa hakuwahi kubadilisha namna ya simu," amesema na kuongeza;
"Lakini upande wa mashtaka hawakumleta mama wa marehemu Ndeshukurwa mtu muhimu kama huyo ambaye aliwasaidia kumpata ili kueleza namna alivyoweza kumpata Getruda."