Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya kusafirisha mijusi, Mahakama yaelezwa washtakiwa walivyokutana

Muktasari:

  • Januari 20, 2020, raia wa Czechoslovakia, Peter Neas alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Vienna Schwechat akiwa na vinyonga 68 na alipohojiwa alidai amevipata Tanzania.

Dar es Salaam. Katika kesi ya kusafirisha nyoka, mijusi na vinyonga 164 inayowakabili washtakiwa watatu, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu namna wawili kati ya washtakiwa walivyokutana.

Wawili hao ni Azizi Ndago ambaye alikutanishwa na Eric Ayo ili aweze kumtafutia vinyonga, nyoka na mijusi raia wa Czechoslovakia, Peter Neas.

Mbali na washtakiwa hao wawili mwingine ni Ally Ringo wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha nyoka, mijusi na vinyonga 164, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafulu ameeleza hayo wakati akiwasomea hoja za awali amedai washtakiwa hao walijihusisha na nyara za Serikali bila kibali tangu mwaka 2016.

Akisoma hoja za awali, Wakili Mafulu amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu yakiwamo ya  kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali na utakatishaji wa fedha

Mafulu amedai Januari 20, 2020, Neas ambaye ni raia wa Czechoslovakia alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Vienna Schwechat akiwa na vinyonga 68 na alipohojiwa alidai amevipata Tanzania.

Amedai uchunguzi ulifanyika ambapo ilibainika kwamba Januari 2020, Neas aliingia nchini kwa ndege ya Ethiopia na alitembelea uoto wa asili wa Amani uliopo mkoani Tanga.

Raia huyo alipotembelea uoto wa asili huo alikutana na mshtakiwa Ringo ambaye alimpa nyoka sita kisha kumtambulisha kwa Ayo Mkazi wa Arusha na kumtaka amsaidie raia huyo wa kigeni kupata nyara hizo za Serikali katika milima ya Uduzungwa, Mikumi, Meru, Uluguru na Mufundi.

Mshtakiwa Ringo alikuwa akijihusisha na biashara hiyo tangu mwaka 2016 na kuwauzia raia wa kigeni wakiwamo kutoka  Czechoslovakia.

Mafulu amedai kuwa upelelezi ulifanyika ambapo mshtakiwa Ringo alikamatwa na kuwataja wenzake.

Pia  uchunguzi huo ulibaini kuwa, Januari 26, 2021 benki ya CRDB tawi la  Msamvu, Morogoro, mshtakiwa Ayo alibadili Dola 400 za Marekani kuwa fedha za Tanzania sawa na Sh923,600 ambazo zilitokana na uuzaji wa vinyonga.

Baada ya kusomwa maelezo hayo, washtakiwa wote waliyakana mashtaka yanayowakabili isipokuwa majina yao na pia walikubali kukamatwa na polisi.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 11, 2023 kwa ajili ya usikilizwaji huku mshtakiwa Ayo akirudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana,  wenzake Ndago na Ringo wakiwa nje kwa dhamana.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Desemba mosi 2020 na Januari Mosi, 2021 mkoani Morogoro, Tanga na Dar es Salaam ambapo kwa pamoja wanadaiwa kupanga na kuongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

Katika shtaka lingine la kukutwa na nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Desemba mosi, 2020 na Januari Mosi, 2021 katika maeneo ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakikusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vinyonga 164, mijusi 20 na nyoka 6, wote wakiwa na thamani ya Sh20 milioni, mali ya Serikali, huku wakiwa hawana kibali kutoka mamlaka husika, pamoja na dola za Marekani 9000.

Shtaka la mwisho la utakatishaji wa edha linalomkabili mshtakiwa Ayo inadaiwa Januari 26, 2021 katika benki ya CRBD iliyopo Msamvu, Morogoro ambapo kwa makusudi alibadilisha dola za Marekani 400 na kupata Sh923,600, wakati akijua, fedha hizo zilikuwa zimetokana na uuzaji wa nyara za Serikali.