Kesi ya Dk Slaa kutajwa leo Mahakama ya Kisutu

Muktasari:
- Dk Slaa alipandishwa Kisutu kwa mara ya kwanza Januari 10, 2025 na kusomewa shtaka moja la moja la kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X zamani Twitter na mpaka sasa yupo rumande baada ya dhamana yake kuzuiliwa.
Dar es Salaam. Kesi ya kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X inayomkabili mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Willibrod Slaa (76) itatajwa leo Jumatano, Februari 19, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Dk Slaa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, imeitwa leo Jumatano, Februari 19, 2025 katika Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa na kuangaliwa iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au la.
Hata hivyo, Hakimu Nyaki kwa sasa yupo likizo, hivyo kesi hiyo itatajwa kwa hakimu mwingine.
Vilevile, wakati kesi hiyo inaitwa kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo, tayari Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania amewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo pamoja na mambo mengine.
Notisi hiyo ya kupinga uamuzi huo iliwasilishwa Mahakama ya Rufani na kusajiliwa katika mfumo Januari 30, 2025 na sasa inasubiriwa kupangiwa jaji kwa ajili ya usikilizwaji.
Kutokana na DPP kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sasa haitaweza kuendelea na kesi ya msingi hadi hapo Mahakama ya Rufaa itakaposikiliza rufaa iliyokatwa na DPP na kuitolewa uamuzi, ndipo kesi ya msingi itaendelea Mahakama ya Kisutu.
Kwa hali hiyo, kwa kuwa mshtakiwa yupo rumande kutokana na upande wa mashtaka kuweka zuio la dhamana dhidi yake, kesi hiyo itakuwa inatajwa kila baada ya siku 14 katika Mahakama ya Kisutu kama sheria inavyoelekeza kwa washtakiwa ambao hawana dhamana, kesi zao zinatakiwa kutajwa mahakamani kila baada ya siku 14.
Kesi ya msingi:
Dk Slaa anakabiliwa na kesi ya Jinai namba 993 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao ya kijamii wa X, zamani ukijulikana kama Twitter.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Mwanasiasa huyo mkongwe anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka kama ifuatavyo.
"Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung'unya,...na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahili atatoa pesa...hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake."
Pia, aliandika katika akaunti maneno yalisomeka kama:"Samia toka muda mrefu haangaikii tena Maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe" wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.