Kauli ya wadau haki za binadamu maafa Hanang

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu.
Arusha. Janga la maporomoko ya tope lililoua watu 69 wilayani Hanang Mkoa wa Manyara, limegusa wadau wa haki za binadamu ambao wameshauru kuwapo kwa uwekezaji zaidi katika kitengo cha maafa.
Mwenyekiti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji mstaafu Mathew Mwaimu na Mratibu Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa wamezungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Desemba 7, 2023 wametoa pole kwa walioathiriwa na janga hilo na kusema ni muhimu Serikali kuwekeza zaidi katika kitengo cha maafa, ili Taifa liwe na utayari wa kunguza maafa.
Jaji Mwaimu amesema THBUB inaungana na Watanzania kutoa pole na kuungana na Serikali katika hatua zinazoendelea za kuwasaidia waathirika.
"Tukio hili linagusa haki za binadamu kwa sababu kuna watu wamefariki dunia, wamejeruhiwa na mali nyingi zimeharibika, hivyo tunatoa pole na tunaomba majeruhi wapone haraka," amesema.
Kwa upande wake, Ole Ngurumwa amesema licha ya THRDC kutoa pole, inashauri Serikali na wadau wengine kuwekeza zaidi katika kitengo cha dharura na maafa.
"Ni muhimu kutolewa elimu ya maafa kwa Watanzania, kuwe na vitengo imara vya maafa katika halmashauri zote, ili kutoa huduma za haraka majanga yanapotokea," amesema.
Amesema ni muhimu Serikali na wadau kuendelea kuboresha sheria ikiwa ni pamoja na kuundwa kamati za maafa kwa kila wilaya na kujengewa uwezo.
"Muhimu tuwe na utayari kama Taifa wakati wote ili kupunguza athari za maafa, lazima wadau washirikishwe katika kupambana na maafa ikiwa ni pamoja na kutengwa fedha za kutosha," amesema.
Mvua iliyonyesha usiku wa Desemba 2, 2023 imesababisha kumeguka eneo la Mlima Hanang na kusababisha mafuriko ya tope katika Mji Mdogo wa Katesh, vitongoji vyake na Kijiji cha Gendabi.
Mbali ya vifo, maporomoko hayo yamejeruhi watu 116 na kuharibu miundombinu.