Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanisa Katoliki lamsimamisha padri anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe

Padri Elipidius Rwegoshora (picha kubwa) aliyesimamishwa uchungaji kwa tuhuma za mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novati (picha ndogo).

Muktasari:

  • Taarifa ya Polisi imesema Padri Rwegoshora anatuhumiwa kumshawishi baba mzazi wa marehemu Asimwe Novart, kufanya biashara ya viungo vya binadamu na kwamba ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.

Dar es Salaam. Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji, Padri Elipidius Rwegoshora kutokana na tuhuma zinazomkabili za kuhusishwa katika mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath.

Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jovitus Mwijage, ametangaza uamuzi huo kupitia gazeti la Kiongozi linalotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), toleo la Juni 21 -27, 2024.

Gazeti hilo limemnukuu Askofu Mwijage akikiri mtuhumiwa ni padri wa jimbo hilo na amemsimamisha kutoa huduma zote za kichungaji mpaka hapo suala lake litakaposhughulikiwa na vyombo vya sheria.

“Tunahuzunishwa na taarifa ya mauaji ya Asimwe, kwani sisi kama Kanisa Katoliki ni walinzi wa kwanza wa uhai wa wanadamu. Tunaiombea familia yake na kuiombea roho yake ipate pumziko la amani mbinguni.

“Hata hivyo, tumesikia taarifa ya watuhumiwa na mmojawapo akiwa ni Padri Rwegoshora. Ni kweli padri huyo ni wa Jimbo Katoliki Bukoba na tumechukua uamuzi wa kumsimamisha kutoa huduma zote za kichungaji mpaka hapo suala lake litakaposhughulikiwa na vyombo vya sheria,” amekaririwa na gazeti hilo.

“Baada ya vyombo vya sheria kumaliza kazi yake, ndipo taratibu nyingine za kanisa zitafuata,” alisema Askofu Mwijage.

Asimwe, aliyekuwa na miaka miwili na nusu alinyakuliwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Muleba mkoani Kagera.

Mwili wa mtoto huyo ulipatikana Juni 17, 2024 akiwa ameuawa kikatili kwa kukatwa baadhi ya viungo vyake, kisha kutupwa kwenye kalavati katika barabara itokayo Luhanga kwenda Makongora, wilayani Muleba.

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi nchini kupitia Msemaji wake, David Misime iliyotolewa Juni 19, 2024 iliwataja watuhumiwa tisa wa mauaji hayo, akiwamo Padri Rwegoshora aliyetajwa kuwa ni paroko msaidizi wa Parokia ya Bugandika.

Watuhumiwa wengine ni baba wa mtoto huyo, Novart Venant, mganga wa jadi Desdeli Evarist, mkazi wa Nyakahama, Faswiru Athuman, Gozibert Alkadi, Rwenyagira Burkadi, wote wakazi wa Nyakahama.

Wengine ni Selemani Selestine na Nurdin Hamada, wakazi wa Kamachumu na Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara.

Taarifa ya Polisi ilisema Padri Rwegoshora anatuhumiwa kumshawishi baba mzazi wa marehemu kufanya biashara ya viungo vya binadamu na kwamba, yeye ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.

Akizungumzia tukio hilo, kupitia televisheni ya UTV juzi, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba, Kashozi, Jimbo Katoliki la Bukoba, Padri Samuel Muchunguzi, alisema taarifa zaidi za mtuhumiwa anazo askofu wa jimbo hilo.

“Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu anayeelewa na kutambua na zaidi sana aliyelelewa vizuri, ni tukio ovu na hakuna mtu anayeweza kuliunga mkono,” alisema.

“Kile ni kitendo cha kinyama, hakipaswi kufanywa kwa mtu yeyote yule, huyo alikuwa mtoto mdogo, aina yoyote ya kuondoa uhai wa mtu au kuathiri maisha ya mtu. Hata kama wangekuwa hawajamuua wamemkata tu mkono,” alisema.

Mpaka sasa haijajulikana watuhumiwa watafikishwa lini mahakamani.

Juhudi za kumpata Misime kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, alipopigiwa simu hakupokea wala kujibu ujumbe aliotumiwa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda alipoulizwa alimtaka mwandishi kurudi kwa Misime ambaye ndiye msemaji wa Jeshi hilo.

“Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini ndiye mtoa taarifa lini watafikishwa mahakamni na sisi tuliwakamata na tunaendelea kuwahifadhi watuhumiwa mpaka taratibu za kisheria zitakapokamilika,” alisema Chatanda.


Maombi ya mama Asimwe

Judith Richard (20), mama yake na Asimwe ameomba familia ikubali awezeshwe kumudu maisha na kuendelea na masomo ya fani ya ushonaji aliyokatisha baada ya kupata ujauzito.

Judith anasema kabla ya kuwa na uhusiano na Novath (24) baba wa Asimwe, alikuwa mwanafunzi wa chuo cha ufundi Veta Ndorage, kilichopo wilayani Muleba mkoani Kagera.

Akizungumza na Mwananchi jana, alisema kutokana na janga kubwa la kumpoteza mpendwa wake, familia haikubali aendelee kuishi alipokuwa akiishi awali, hivyo anaomba jamii na Watanzania kwa ujumla kumsaidia kumudu maisha na kuendelea na mafunzo ya ushonaji.

Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Kagera (UVCCM), Juni 19, 2024 ulifika nyumbani kwa kina Judith, Kijiji cha Bulamulana kutoa ahadi ya kuijengea nyumba familia ya vyumba viwili na sebule kwa ajili ya kumbukumbu ya Asimwe.

Baada ya ahadi hiyo, anasema familia ilikaa kikao cha ukoo na kuomba nyumba isijengwe kwa baba wa mtoto huyo, bali itafutwe sehemu nyingine ajengewe, ikielezwa mila haziruhusu mtoto wa kike kujenga nyumbani kwao.

Mwenyekiti wa UVCCM Kagera, Faris Buruhan alisema jana kuwa baada ya mazungumzo ya pande zote, wamekubaliana litafutwe eneo ajengewe nyumba na kufunguliwa akaunti benki ili watakaokuwa tayari kumsaidia wafanye hivyo.

Mkazi wa Kamachumu, Odina Richard, mama mzazi wa Judith alisema familia imekubali UVCCM kumsaidia mtoto wake.

“Tumekaa kikao cha ukoo, pia tumekutana na viongozi wa UVCCM tumekubali kijana wetu asaidiwe kwa kutafuta eneo rafiki la kumjengea nyumba japo bado anahitaji kuendeleza fani yake aliyokatishwa kipindi yupo chuoni, alikuwa anasoma ufundi wa kufuma na kushona nguo,” alisema.

Mkazi wa Kata ya Kamachumu, Mugisha Venant, ambaye ni kaka wa Novath ambaye ni baba wa Asimwe alisema wanakubaliana na uamuzi wa upande wa pili wa ukoo wa Judith kutojengewa nyumba alikoporwa mtoto.

“Sisi hatuoni kama kuna tatizo kwa sababu mdogo wangu alifanya kosa na isitoshe huyo bado ni binti mdogo, anahitaji msaada wa kijamii na kisaikolojia. Tunaomba jamii iendelee kumsaidia,” alisema.