Kampuni ya Jatu yamleta mshauri mwelekezi ili kuinusuru

Kaimu Mkurugenzi wa Jatu PLC, Mohamed Simbano
Muktasari:
- Kaimu Mkurugenzi wa Jatu PLC, Mohamed Simbano amemtambulisha mshauri huyo kuwa ni Ben Philipsen, raia wa Uholanzi ambaye atakuwepo nchini kwa kazi maalum ya kusaidia kampuni hiyo kutengeneza mpango kazi mpya wa biashara itakayoendana na dira na maoni ya kampuni.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (32) kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujipatia Sh5.1 bilioni kwa udanganyifu, kampuni hiyo imemleta mshauri mwelekezi kutoka Uholanzi kwa ajili ya kutengeneza mkakati na kuweka taswira nzuri kwa wawekezaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Jatu PLC, Mohamed Simbano amemtambulisha mshauri huyo kuwa ni Ben Philipsen ambaye atakuwepo nchini kwa kazi maalum ya kusaidia kampuni hiyo kutengeneza mpango kazi mpya wa biashara itakayoendana na dira na maoni ya kampuni.
Amesema mpango huo ni pamoja na kushauri namna ya kuboresha uongozi na kumaliza madeni yote wanayodaiwa na wadai kwa kukaa meza moja na wadai.
Simbano amesema hayo leo Jumanne, Januari 3, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malengo na mikakati ya kampuni hiyo pamoja na kumpokea mtaalamu huyo wa masuala ya biashara, fedha na uongozi kutoka nchini Uholanzi.
Amesema JATU imeamua kuleta mshauri huyo kwa ajili ya kutengeneza mpango mkakati na kurudisha taswira nzuri ya kampuni hiyo sambamba na kuhakikisha kuwa wale wote waliowekeza katika kampuni hiyo, mitaji yao haipotei.
“Mtaalamu huyo amekuja nchini jana na atakuwepo nchini kwa siku 14 na atashirikiana na taasisi ya PUM Netherlands pamoja wataalamu wa masuala ya fedha na mitaji ambao ni Luzane Financial na InterCapital Advisory Service kwa kushirikiana na SSC Capital ambao kwa sasa wanafanya kazi ya kukuza mtaji kwa ajili ya kumaliza madeni yote kampuni inayodaiwa na kuona namna ya kuendesha miradi,” amesema Simbayo na kuongeza:
“Pia, mshauri huyu atatoa ushauri namna ya kuendesha miradi iliyokuwepo awali na kuisimamia kwa weledi na ujuzi ili kuleta tija na hatimaye kumaliza changamoto zilizojitokeza,” amesema Simbano.
Amesema kampuni hiyo itashirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ambao ni wamahisa, wakulima, washauri, taasisi za Serikali na wahisani ili kukamilisha mchakato wa kuleta mabadiliko katika kampuni.
Pamoja na mambo mengine, amesema kampuni ya Jatu imefanya mabadiliko ya uongozi kuanzia Septemba mwaka huu kwa ajili ya kuongeza ufanisi.
“Lengo la uongozi mpya ni kuhakikisha kuwa maono na malengo la ya kuanzishwa kampuni yanatimia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wote waliowekeza mitaji yao haipotei, lakini pia kuiruidisha kampuni hii katika taswira nzuri na bora iliyotarajiwa na kila mwekezaji,” amesema Simbano.
Amesema kwa muda mfupi tangu uongozi huo mpya uingie madarakani Septemba 2022, wamesharudisha baadhi ya huduma za uzalishaji wa bidhaa ikiwemo unga wa dona na sembe ambapo hapo awali zilisitishwa na uongozi uliopita.
Simbano amesema uongozi mpya kwa kushirikiana na bodi, Serikali na wabia mbalimbali wameweka nguvu kubwa kwa sasa katika kilimo baada ya kubaini changamoto zilizokuwa zinaikabili kampuni hiyo ambazo ni madeni, uongozi wa kampuni na kuyumba kwa biashara.
Kwa upande wake, mshauri huyo mwelekezi, Ben Philipsen amesema amekuja nchini kwa ajili ya kuangalia namna gani atatumia uzoefu wake katika kuandaa mikakati itakayoinyanyua juu kampuni hiyo.
“Jatu inaingia kwenye mkakati mkubwa, mpya na wenye maono makubwa kwa sababu imeorodheshwa kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam,” amesema Philipsen.
Dk Zaipuna Yohan ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya JATU, amesema hakuna hela iliyowekezwa katika kampuni hiyo itakapoyotea kwani mpango mkakati wao kwa mwaka 2022/2023 ni kuongea juhudi katika kilimo ili kuongeza mapato zaidi na kuongeza spidi ya kupunguza madeni pamoja na kurudisha huduma za kiofisi za Jatu PLC.
“Pia, tunataka kujenga taswira mzuri kwa kampuni ili kuondoa changamoto ambazo tulizibaini na kupelekea kufanya mabadiliko ya uongozi mpya kwa lengo la kuiinua kampuni hii,” amesema Dk Yohan.