Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kambi za matibabu zinavyoonyesha ombwe la uhitaji wa huduma bora za afya Tanzania

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akimpokea mtoto alipotembelea meli ya jeshi la China (Ark Peace) iliyopo katika bandari ya Dar es Salaam tangu Julai 16 kwa ajili ya kutoa huduma bure ya matatiba kwa wananchi.

Muktasari:

  • Fursa za matibabu ya bure nchini Tanzania, kama meli ya hospitali ya jeshi la China (Ark Peace), huvutia maelfu ya wananchi kutokana na gharama kubwa za matibabu.

Dar es Salaam. Kila inapotokea fursa ya matibabu ya bure nchini Tanzania, maelfu ya wananchi wamekuwa wakijitokeza wakati mwingine hata kwa kugombania, jambo linaloonyesha uhitaji wa matibabu ya kibingwa waliokuwa nao.

Baadhi ya wachambuzi wanadai hali hiyo inatokana na watu wengi kutokuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu. Pia urahisi wa kukutana na madaktari bingwa karibu na maeneo yao.

Miongoni mwa fursa za matibabu ya bure ya hivi karibuni ni meli ya hospitali ya jeshi la China (Ark Peace) ambayo ipo bandari ya Dar es Salaam tangu Julai 16, 2024 ikitoa matibabu bure kwa wananchi.

Baadhi ya wagonjwa hulazimika kulala nje ya bandari hiyo ili kujihakikishia fursa kutibiwa. Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu zaidi ya wagonjwa 5,000 wamepewa matibabu ya magonjwa mbalimbali katika siku tano za mwanzo za kambi za utoaji huduma wa Ark Peace.

Akizungumza jana Jumapili, Julai 21, 2024, Waziri Ummy alisema meli hiyo ni hospitali inayotembea ikiwa na vipimo vyote vinavyohitajika ikiwemo CT-Scan, Ultra sound pamoja na vyumba vinane vya upasuaji na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali yakiwamo ya ndani.

"Kwa kweli nimefurahi kuonana na mama aliyepata mtoto kwa kujifungua salama kwenye meli hii, hii inaonyesha mahusiano ya nchi hizi mbili yamegusa maisha ya watu na mtoto huyu amepewa jina la 'Peace of Ark'," alisema.

Kamanda anayeongoza meli hiyo mwaka huu, Ying Hongbo alisema kuzaliwa kwa mtoto katika meli hiyo ni hatua nyingine ya kuimarisha urafiki kati ya China na Tanzania. “Lengo letu ni  kuhudumia wagonjwa 600 kwa siku lakini tutajitahidi kuongeza idadi kadri inavyowezekana.”

Wakati Kamanda Hongbo akisema lengo lao ni kuhudumia wagonjwa 600 kwa siku, idadi hiyo imeshavuka kulingana na takwimu alizozitoa Waziri Ummy ni kuwa wanahudumia wastani wa wagonjwa 1,000 kwa siku.

Akizungumzia meli hiyo Balozi wa China nchini, Mingjian Chen alisema Ark Peace ndiyo meli ya kwanza ya matibabu ya rasmi ya Kichina ambayo imekuwa ikitoa huduma katika maeneo mbalimbali na kwa Tanzania hii ni mara ya tatu inakuja ambapo awali ilikuja mwaka  2010 na 2017.

“Hii inaifanya Tanzania kuwa nchi pekee Afrika ambayo imetembelewa na meli hii mara tatu. Tangu karne ya 15 na China imekuwa ikichukulia Tanzania kama rafiki wa karibu, tumekuwa na urafiki wa kitamaduni tangu zamani na umekuwa ukirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” alisema Chen.


Kilichotokea kambi ya Arusha

Ukiachilia mbali yanayojiri katika meli hiyo, zaidi ya watu 32,186 walihudumiwa katika kambi ya matibabu ya madaktari bingwa na wabobezi iliyofanyika kwa muda wa wiki moja Juni mwaka huu katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkombachepa alisema kati ya watu hao walikuwamo watoto 4,616 na wanawake 19,546.

Mkombachepa alisema wagonjwa waliokuwa wengi ni wa macho wakiwa  9,834 ikifuatiwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu waliokuwa 2,601.

Mwandaaji wa tukio hilo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alisema kwa idadi hiyo, inaonyesha watu wenye uhitaji ni wengi.


Gharama za matibabu changamoto

Kutokana na mafuriko ya watu katika huduma za bure msemaji wa sekta ya afya kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga amesema changamoto kubwa ni uwepo wa watu wengi wasioweza kumudu gharama za matibabu, hivyo kukimbilia huduma za bure.

Dk Elizabeth amesema hata hivyo zahanati na vituo vingi vya afya havina madaktari. “Majengo yapo, lakini madaktari ni changamoto.”

“Kambi ni nzuri lakini si suluhisho hata kama ukitibu watu 100,000 hawa watahitaji ufuatiliaji wa wataalamu wa afya, watawapata wapi? Cha kufanya Serikali iache kuwekeza sana kwenye masuala ya huduma za kibingwa ambazo watu hawawezi kuzifikia, wawekeze madaktari ngazi za chini ili kuwaibua wagonjwa katika hatua za awali kabla hawajahitaji mabingwa,” amesema.

Dk Elizabeth amefafanua bajeti kubwa ya Wizara ya Afya imewekezwa kwa madaktari bingwa na kuwasahau wananchi ambao ni asilimia 80 wanaotibiwa katika ngazi za chini.

Amesema nchi ikijikita kuwekeza katika ngazi za chini itasaidia kubaini wenye magonjwa sugu mapema kama ini, figo, moyo, kisukari na mengineyo.

“Lazima kuimarisha ngazi za chini, kubadilisha mfumo wa ugharamiaji wa sekta ya afya kwani kwa  sasa Serikali imejiweka pembeni, ni lazima iingie kumsaidia mwananchi katika huduma za afya kupitia mfumo tunaoupendekeza na pasiwe na matabaka na kila wanapoenda vituoni wapate huduma za afya kadri wanavyohitaji,” amesema Dk Elizabeth.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe amesema uhitaji wa huduma za afya nchini ni mkubwa hususani zilizo bora na wanaamini kwenda huko watakutana na wanaoweza kutoa huduma bora zaidi.

Ametaja kitu cha pili ni gharama za matibabu kuwa juu kwa kuwa Watanzania wengi hawana fedha, hivyo hutamani huduma za bure ndiyo maana zikitangazwa wanajazana.

“Ukiwa huna pesa utakimbilia au kutafuta kwenye unafuu, ndicho kinachotokea.”

“Hii inaashiria huduma zinahitajika zenye ubora, bobezi na zinazofikika. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha haya yote yanapatikana. Serikali yenyewe haitaweza tunahitaji usaidizi watu tuliopo kwenye sekta binafsi tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja,” amesema Dk Makwabe.

Amesema, “uwekezaji fedha unahitajika, Serikali haiwezi kutoa huduma bure, watashindwa kuendesha huduma kwa maana dawa, vifaa ni gharama watashindwa kumudu. Ikija bima ya afya kwa wote labda itakuwa nafuu watu wote waweze kuingia huko, japokuwa itachukua muda mrefu,”alisema.

Wasemacho wananchi

Baadhi ya wananchi waliofika katika bandari ya Dar es Salaam kupatiwa tiba, walisema wanakata tamaa kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kupata huduma, ilhali walio wengi ni wagonjwa na wana maumivu kutokana na maradhi waliyonayo.

Mkazi wa jijini la Dar es Salaam, Kennedy Gausi amesema: “Hali zetu zinajulikana tangu juzi tuko hapa mpaka sasa, kama walivyosema wanahudumiwa watu 600 lakini leo siku ya tatu hatujapata huduma,” amesema.

Mama aliyejifungulia katika hospitali hiyo,  Naza Fadhili amesema alikuwa akihudhuria kliniki katika Hospitali ya Lugalo na daktari aliyekuwa akimhudumia akamweleza kuwa kuna fursa ya kujifungulia kwenye meli na inatoa matibabu bure kama anahitaji, "Aliniambia naweza kwenda huko sababu hakuna gharama ya kujifungua, nikaenda na kulazwa na kesho yake alfajiri nikajifungua mtoto."