Kamati ya Bunge yapendekeza Hospitali ya Benjamini Mkapa iwe ya Taifa
Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi akiwaongoza Wabunge walipotembelea hospitali hiyo
Muktasari:
- Hii si mara ya kwanza kwa wabunge kuomba Benjamin Mkapa iwe Hospitali ya Taifa kutokana na huduma zinazotolewa hapo ikiwemo za kibingwa ambazo zimekuwa zikitolewa hapo.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imeiomba Serikali kufikiria uwezekano wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kuwa Hospitali ya Taifa, kutokana na kiwango cha huduma za kibingwa na bobezi zinazotolewa hospitalini hapo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Johannes Lukumay, amesema kamati imeridhishwa na maendeleo ya huduma katika hospitali hiyo, ikiwemo utoaji wa huduma 20 za ubingwa na 17 za ubingwa bobezi, pamoja na huduma za upandikizaji uloto kwa watoto wenye sikoseli na upandikizaji wa figo.
Amesema huduma hizo zinaonyesha uwezo wa hospitali hiyo kufikia hadhi ya kitaifa, huku akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu ya kibingwa kwa gharama kubwa.
Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi akiwaongoza Wabunge walipotembelea hospitali hiyo
Pia, Lukumay amesisitiza Serikali kuendeleza jitihada za kuboresha sekta ya afya, hususan utekelezaji wa bima ya afya kwa wote pamoja na kuimarisha viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama za matibabu nchini.
"Tunaipongeza Serikali, uelekeo katika sekta ya afya sasa ni kuanzisha viwanda vyetu vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi kutoka nchi za nje," amesisitiza Dk Lukumay.
Amesema utekelezaji wa bima ya afya kwa wote utalenga kuhakikisha makundi yote ya jamii yanapata uhakika wa huduma za afya, hususan matibabu ya magonjwa sugu na yenye gharama kubwa kama sikoseli, figo, moyo, kisukari na matatizo ya mifupa.
Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi akiwaongoza Wabunge walipotembelea hospitali hiyo
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, amesisitiza kuwa Wizara ya Afya itahakikisha mradi wa ujenzi wa kituo cha umahiri cha mafunzo na matibabu ya saratani unaojengwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa gharama ya Sh32 bilioni unakamilika kwa wakati.
Amesema hatua hiyo itaenda sambamba na uwekaji wa vifaa tiba ili kuwezesha huduma za kibingwa bobezi za saratani kupatikana katika kanda zote nchini.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani kwa ukaribu zaidi na wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema asilimia 60 ya huduma 20 za ubingwa na 17 za ubingwa bobezi tayari zimeanzishwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wateja.