Joto kuongezeka duniani kwa wastani wa nyuzi 1.50C ifikapo 2030
Muktasari:
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, Dk Agnes Kijazi amesema wastani wa ongezeko la joto duniani utapanda kutoka nyuzi joto 1.10C kwa mwaka na kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2030.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, Dk Agnes Kijazi amesema wastani wa ongezeko la joto duniani utapanda kutoka nyuzi joto 1.10C kwa mwaka na kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2030.
Dk Kijazi ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 23, 2021 alipokuwa kwenye uzinduzi wa kitabu kinachoelezea mabadiliko madogo ya hali ya Hewa kilichoandikwa na Mkurugenzi wa masuala ya Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Dk Ladislaus Chang'a.
Amesema tathmini iliyofanywa na Jopo la kidunia la masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa (IPPC) imeonyesha kuwa, kasi ya ongezeko la joto duniani ni kubwa.
“Inaonesha kuwa joto limeendelea kuongezeka, ambapo kwa mwaka 2020 na 2021, joto limeongezeka kwa wastani wa nyuzi joto 1.10C kwa mwaka.
“Kasi ya ongezeko la joto ni kubwa na tathmini iliyofanywa na IPCC inaonesha kuwa ongezeko la joto linaweza kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2030,” amesema Dk Kijazi.
Amesema ongezeko la joto Duniani huambatana na kuongezeka Kwa matukio ya Hali mbaya ya Hewa ikiwemo kuongezeka Kwa matukio ya ukame,mvua kubwa,mafuriko na upepo mkali.
"Matukio haya yanasababisha athari kubwa katika sekta zote za kiuchumi na kijamii hivyo kitabu hiki cha Klimatolojia na Mwendo na athari za matukio ya Hali mbaya ya Hewa kimekuja wakati muafaka," amesema DK Kijazi.
Kuhusu kitabu hicho, Dk Kijazi amesema kitakuwa na mchango mkubwa wa kuongeza uelewa wa changamoto za hali ya hewa kwa watu wote hasa wanafunzi wa elimu ya vyuo vya elimu ya juu pamoja na Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma.
Amewataja wanufaika wengine kuwa ni pamoja na watafiti, makandarasi na watunga sera.
“Nampongeza sana DK Chang'a kwa kazi nzuri na juhudi kubwa anazofanya za kufanya Tafiti, Kufundisha na kuwahamasisha vijana hapa nchini,” amesema.
Naye mwandishi wakitabu hicho, ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Dak Ladislaus Chang'a amesema sababu ya kutunga kitabu hicho baada ya kuulizwa maswali mara kwa mara na wanafunzi anaowafundisha wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Dk Chang'a amesema kitabu hicho kimekuja muda mwafaka hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa baada ya nchi kukabiliwa na changamoto ikiwemo ya ukame,mafuriko na Hali ya hewa mbaya.
"Niligundua katika nchi yetu hakuna kitabu cha aina hii cha kufundishia pale chuoni ndiyo maana nikaamua kutunga kulingana na maswali niliyokuwa nikiulizwa na wanafunzi wa Chuo kikuu," amesema DK Chang'a.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara aliyekuwa mgeni rasmi, amesema serikali inatambua changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan, aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa COP 26 uliofanyika Glasgow, Scotland Novemba 2021 ambako alielezea jitihada za Tanzania katika kuhimili na kukabiliana na changamoto hizo.
"Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii na kuwaandaa na kuwataka wataalamu kutoa mchango chanya wa kusaidia kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya tafiti na kuelimisha Jamii," amesema Waitara.