Joto kufikia nyuzi 48 barani Ulaya kwa mara ya kwanza
Muktasari:
- Mtandao wa Dail Mail umeripoti leo Julai 14, 2023 kuwa upepo mkali wenye joto (Anticlones) umeshuhudiwa ukipuliza kutoka kaskazini mwa jangwa la Sahara kuelekea kusini mwa bara Ulaya katika siku za hivi karibuni ambapo umesababisha kuibuka kwa moto wa porini unaotishia maisha ya watu na wanyama huko nchini Croatia.
Mwanza. Wiki ijayo, baadhi ya maeneo barani Ulaya yanaweza kukumbwa na hali ya joto kali zaidi kuwahi kutokea barani humo.
Hali hii imebainishwa na wataalam wa hali ya hewa, ambapo wametahadharisha kuwa joto hilo linaweza kufikia hadi nyuzi joto 48 jambo linalotishia usalama wa watu, mifugo na mazao.
Mtandao wa Dail Mail umeripoti leo Julai 14, 2023 kuwa upepo mkali wenye joto (Anticlones) umeshuhudiwa ukipuliza kutoka kaskazini mwa jangwa la Sahara kuelekea kusini mwa bara Ulaya katika siku za hivi karibuni ambapo umesababisha kuibuka kwa moto wa porini unaotishia maisha ya watu na wanyama huko nchini Croatia.
Wakati watalii na wenyeji barani humo wakijitahidi kuivumilia hali hiyo, nchi za Hispania, Italia, Ugiriki na Uturuki, joto linatarajiwa kuongeza zaidi ya nyuzi 45 ifikapo mwishoni wa wiki ijayo.
Jana, maofisa wa vikosi vya uokoaji nchini Ugiriki, walilazimika kuwasafirisha watalii kwa kutumia magari ya wagonjwa (Ambulance) kutoka ngome ya Acropolis huko Athens kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuongezeka kwa joto.
Pia kuna ripoti za vifo vya watu watatu wakiwemo watoto wawili huko Manfredonia siku ya Jumanne sambamba na kifo cha mchoraji wa mwenye umri wa miaka 44 huko Lodi nchini Italia, wote wakidaiwa kuwa walikuwa wakiogelea kutafuta unafuu wa halijoto hiyo.
Wakati wataalam wanakionya juu ya hali hiyo ya joto kali wanaloliita 'Charon,' inaelezwa kuwa huenda hali hiyo ikavunja rekodi ya kuwa na joto la juu zaidi kuwahi kutokea barani Ulaya.