Jokate awananga vijana wabebao mabegi ya wagombea

Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo akizungumza na vijana wakati alipofanya ziara yake mkoani Iringa.

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Jokate Mwegelo,  amewataka vijana wasikubali kutumika vibaya katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025 na badala yake, wajitokeze kugombea.

Iringa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Jokate Mwegelo amewataka vijana kutotumika vibaya kubeba mabegi ya watu wanaotaka kugombea katika nafasi mbalimbali,  kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Amesema badala ya kutumika vibaya, vijana hao wanapaswa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali na kwamba wapo tayari kuwatetea wale wenye uwezo.

Jokate amesema hayo Juni 21, 2024 wakati akizungumza na vijana kwenye ziara ya kikazi mkoani Iringa.

Kiongozi huyo wa UVCCM, amefanya ziara hiyo kwa lengo la kutembelea chuo cha UVCCM cha Ihemi wanakotarajia kuanza mafunzo kwa vijana.

“Vijana tusitumike vibaya kubeba mabegi ya watu wanaotaka kugombea kipindi hiki. Tusikubali watu watutumie vibaya, tutapoteza mwelekeo na tutapotea kabisa,” amesema Jokate.

Mwegelo amewataka vijana kujenga upendo miongoni mwao na kwamba ofisi ya umoja huo haipo tayari kupokea fitna, majungu na uchonganishi.

“Ofisi itatumika kusaidia vijana wafikie ndoto zao, ofisi hii ni kwa ajili ya kuunganisha vijana wote bila kuangalia dini wala hali zao za kiuchumi,” amesema Mwegelo.

“Kuliko kubeba mabegi kwanini tusigombee wenyewe,” amesema.

Kiongozi huyo wa UVCCM Taifa amesema vijana wajue wana kazi kubwa ya kusaka na kulinda kura,  na kazi hiyo hawawezi kuifanga ikiwa kutakuwa na migongano.

Amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni vijana na kwamba kijana mwenye sifa na uwezo wa kuongoza umoja huo watamtetea.

"Vijana tujiamini, Tanzania ilitengenezwa na vijana wakiongozwa na  Mwalimu Julius Nyerere na walitumia ujana wao vizuri ndio maana wametuachia urithi ambao ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jokate.

Amewataka vijana wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la kupiga kura na kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi kwenye chaguzi zote.

"Vijana tuna kazi ngumu mbele yetu, tusemee kazi za Rais (Samia Suluhu Hassan) na twende kwenye mitandao ya kijamii kule kuna wapotoshaji wengi, lazima tueleze kazi za Rais," amesema Jokate.

Awali, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Aggrey Tonga amesema changamoto nyingi za vijana zimekuwa zikifanyiwa kazi.

“Makundi mengi ya vijana changamoto zao zinafanyiwa kazi, mfano machinga wamejengewa soko na wametoka juani,” amesema Tonga.