Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jela mwaka mmoja kwa kumuua mpenzi wake kisa kunyimwa penzi

Muktasari:

  • Humphrey Ngogo ambaye wakati anatenda kosa hilo alikuwa na umri wa miaka 17,alishtakiwa kwa kosa la kumuua Faraja Shabani, aliyekuwa mpenzi wake kwa kumpiga na shoka kichwani baada ya kukataa kufanya naye mapenzi.

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya, imemuhukumu adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, Hamphrey Ngogo, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mpenzi wake Faraja Shabani, bila kukusudia.

Katika kesi hiyo ya jinai ya mwaka 2023, hukumu yake imetolewa jana Machi 25,2025 na Jaji Mussa Pomo na nakala yake kupatikana kwenye mtandao wa mahakama.

Awali Ngogo alishtakiwa kwa kosa la mauaji alilolitenda kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.

Ngogo wakati anatenda kosa hilo Septemba 2, 2022 katika eneo la Mkuyu kata ya Iganzo, mkoani Mbeya alikuwa na miaka 17.

Upande wa mashitaka ulieleza kuwa  Ngogo alikiri kutenda kosa hilo na kuwa siku ya tukio alikwenda nyumbani kwa akina Faraja kwa lengo la kufanya naye mapenzi, ila marehemu hakuwa tayari ndipo alipomkaba shingo ili asipige kelele.

Ilielezwa kuwa licha ya kujaribu kumkaba marehemu aliendelea kupiga kelele, mshtakiwa akaenda kuchukua shoka na kumpiga nalo kichwani na baada ya kuona Faraja hazungumzi tena, alitoka nje na kukimbia.

Akitoa ushahidi mahakamani hapo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa huo, Justine Daiwelo alisema Septemba 2, 2022 alipigiwa simu na balozi wa nyumba 10 akimtaarifu kuhusu tukio hilo na alipofika eneo hilo alikuta watu wengi wamekusanyika.

Alisema alipoingia ndani ya chumba alichokuwa akilala binti huyo, aliona damu imetapakaa chini ya kitanda na zulia lililokuwa chini yake likiwa limelowa damu.

Alieleza kuwa baadaye alipokea simu kutoka kwa balozi wa nyumba 10 na kumfahamisha kwamba kulikuwa na mvulana mdogo akisema amemwona mshukiwa wa kosa hilo ambaye alikamatwa akiwa amejifungia ndani nyumbani kwao.

Sajenti David ambaye alichunguza tukio hilo, alisema alipofika nyumba lilipotokea tukio hilo aliona damu imetapakaa chini ya kitanda kwenye chumba ambacho msichana huyo alikuwa akilala, na kwenye korido ya nyumba hiyo aliona shoka likiwa na mpini wa chuma.

Alisema baada ya kumkamata mshtakiwa alipokuwa akimuhoji alikiri kuwa ndiye aliyetenda kosa hilo na alikwenda alipokuwa anaishi marehemu kwa lengo la kufanya naye mapenzi, lakini msichana huyo hakuwa tayari kufanya hivyo.

Aliongea mshtakiwa alieleza kuwa alilazimika kumkaba koo msichana huyo ili asipige kelele ila alipotoka na kupata shoka alimpiga nalo kichwani na kumwacha marehemu amelala chini, baada ya kuona hawezi kuzungumza.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulibaini mwili huo ulikuwa na jeraha kichwani na chanzo cha kifo hicho ni jeraha la kichwa kutokana na kupigwa na kitu kizito.

Shahidi wa tatu, David Edward ambaye pia alikuwa na umri chini ya miaka 18,kwa kutii matakwa ya kisheria yaliyowekwa chini ya Sheria ya Mtoto alitoa ushahidi wake mbele ya Ofisa Ustawi wa Jamii, Lydia Edson.

Alisema siku ya tukio akiwa kwenye bustani ya mboga iliyopo nyuma ya nyumba aliyokuwa akiishi marehemu alimuona akipika jikoni na kumuona mshtakiwa akimsogelea ila hakujua walizungumza nini.

Alifafanua baadaye hakuwaona hapo tena na walikuwa kwenye nyumba hiyo ila dalili zilionyesha kuwa wawili hao walikuwa katika aina fulani ya mapigano, na alipomaliza kumwagilia mboga aliondoka.

Aliongeza kuwa aliporudi baadaye nyumbani kwa akina Faraja akihitaji kurejeshewa kadi yake, ambayo Faraja alikuwa amemuazima alikuta mlango umefungwa na hata alipogonga hakufunguliwa.

Alisema aliamua kumsubiri nje ila baada ya muda alisikia mlango ukifunguliwa na mshtakiwa akitoka ndani ya nyumba akikimbia na kuruka uzio wa nyumba hiyo.

“Saa 11 jioni nilisikia habari zikienea kwamba Faraja ameuawa, ndipo alipomweleza mama yake kuhusu mtuhumiwa huyo, mama yake akatoa taarifa kwa balozi wa nyumba 10.”


Utetezi

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo  alisema  siku ya tukio alipokuwa akitoka masomoni, akiwa njiani kuelekea nyumbani alimuona Faraja akiwa amesimama na mwanamume mwingine aliyedai alikuwa na mahusiano naye ya kimapenzi.

Alisema Faraja hakumuona hivyo alikwenda nyumbani kwao ila baadaye aliamua kwenda kwa akina Faraja kutaka kujua kama amerejea nyumbani kwa nia ya kuthibitisha kama alikuwa na mpenzi mwingine.

Alieleza kuwa alipofika aligonga mlango na mpenzi wake akafungua na kukaribishwa ndani, wakaelekea chumbani kwa Faraja na alipomuuliza kama ana mahusiano na mwanamume aliyemuona amesimama naye barabarani Faraja alimjibu kuwa, kwa namna ulivyoona ndivyo mambo yalivyo.

Ngogo alisema kulizuka kutoelewana kati yao na kuanza kurushiana maneno makali na kutokana na hofu, walianza kusukumana, ambapo alikiri kumkaba shingo na kumsukuma.

Alisema, Faraja alianguka na kichwa kilijigonga chini ya jiwe lililokuwa limewekwa chini ya kitanda na  kuwa alimuacha akiwa hai kisha akaondoka hadi nyumbani kwao, lakini baadaye  alikuja kukamatwa na Polisi.

Aliieleza mahakama kuwa hakumuua Faraja kwa kukusudia.


Uamuzi Jaji

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili Jaji Pomo alianza kwa kueleza kuwa suala litakaloamuliwa ni iwapo Jamhuri imeweza kuthibitisha pasipo shaka yoyote.

Amesema  kutokana na kukiri kwa mtuhumiwa mwenyewe, basi hakuna ubishi kwamba ndiye aliyemuua marehemu na kuwa suala muhimu mahakama inayoangalia ni kubaini iwapo mtuhumiwa alichochewa na nia mbaya ya kumuua marehemu.

Amesema kwa bahati mbaya hakuna mtu ametoa ushahidi wa kuwaona au kuwasikia washtakiwa na marehemu kuhusiana na kile kilichotokea walipokuwa ndani ya chumba hicho.

“Kwa mtazamo wangu nilionao sina shaka mtuhumiwa alifanya mauaji hayo baada ya kutolewa maneno makali yaliyochochea kufanyika tukio la mauaji,”amesema.

Jaji amesema mahakama imemkuta Ngogo na hatia ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

Jaji Pomo amesema baada ya kuzingatia hoja ya utetezi ya kupunguza adhabu kwa kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza ambaye amekuwa mahabusu kwa miaka mitatu tangu 2022, anajuta kosa alilofanya na alitenda kosa hilo akiwa na umri wa miaka 17 ambaye kwa mujibu wa sheria ni mtoto, hakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya busara.

“Kwa  kuzingatia muda wa kutenda kosa hilo alikuwa mtoto mwenye umri wa miaka 17, namuhukumu kutumikia kifungo cha muda wa miezi 12 jela kwa kusababisha kifo cha Faraja Shabani,”amehitimisha Jaji