Jamii yatahadharishwa kuchanganya dini na siasa

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania, Seif Hassan (katikati) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkutano wao wa mwaka unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Mariam Mbwana
Muktasari:
- Wito huo umetolewa na Naibu Amiri wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Abdulrahman Ame wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Dar es Salaam. Jamii imetakiwa kuacha kuchanganya masuala ya siasa na dini kwa kuwa kuwa yanaweza kuleta athari ikiwamo uvunjifu wa amani.
Pia, masuala hayo yanaweza kusababisha mkanganyiko na kuzalisha mianya ya wanasiasa kuitumia dini vibaya au watu wa dini kutumia siasa vibaya kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
Wito huo umetolewa leo Jumanne, Septemba 24, 2024 na Naibu Amiri wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Abdulrahman Ame wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wao wa mwaka unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Ame amesema dini na siasa ni vitu viwili tofauti ambavyo haviingiliani na vinasimama kwenye nyanja tofauti katika maisha ya binadamu
“Dini ni njia ya maisha inayokusudia kumuongoza mtu kuelekea kwa Mungu wake huku siasa ikihusika na masuala ya utawala,” amesema.
Pia, amesema kutokana na kuona umuhimu wa watu katika jamii kuwa na uelewa huo, itakuwa ni moja kati ya mada itakayozungumzwa katika mkutano wa mwaka wa jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 27 na 29, 2024 katika Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Seif Hassan amesema mkutano huo ambao ni wa 53 tangu kuanza kufanyika unatarajiwa kuhudhuriwa na watu takribani 5000 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Pia, unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na jamii kwa jumla huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Mkutano huu unalenga kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu, kuepukana na maovu, kuchochea moyo wa huruma na upendo,”amesema.
Vilevile amebainisha baadhi ya mada zitazungumzwa katika mkutano huo ni maadili pamoja na malezi sahihi kwa watoto.
Naye, Amir wa jumuiya hiyo, Khawaja Ahmad amesema mkutano huo umelenga kuwakumbusha waumini wake kuendeleza tamaduni ya kuisaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwamo utoaji wa huduma za afya, elimu na misaada ya kibinadamu kwa wenye uhitaji bila ya kujali itakadi ya imani zao.
Pia, kuwaelimisha na kuwahimiza vijana kuwa na mienendo bora ya kimaisha na kuwa raia wawajibikaji kwa nchi yao na kuwa viongozi waadilifu katika jamii kwa mustakabali wa jamii na Taifa bora,” amesema.