Jaji Mutungi: Sikuwaita kuwanyooshea kidole, nataka tujenge nchi

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Muktasari:
- Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema dhamira ya kikao cha Baraza maalum la vyama vya siasa ni kujenga nchi moja na si kunyoosheana vidole.
Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amesema dhamira ya kikao cha Baraza maalum la Vyama vya Siasa si kunyooshea kidole chama kinachokosea, bali ni kuelimishana ili kufanya siasa za kuijenga nchi.
Kauli yake hiyo inatokana na kile alichoeleza kuwa, wapo wanaodhani wito wake kwa wadau wa siasa unalenga kutupiana maneno na kuvituhumu vyama fulani vya siasa, ilhali si hivyo.
Kikao cha baraza hilo, kimeitishwa siku chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuratibu mkutano uliohusisha viongozi wa dini.
Mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Bulyaga Temeke jijini hapa, ulilenga kujadili mambpo yanayohusiana mkataba wa uwekezaji, uboreshaji na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam, kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia DP World.
Kutokana na kuhusishwa kwa viongozi wa dini, Jaji Mutungi aliiandikia Chadema kuisihi isitishe mkutano huo, huku akiwaita viongozi wake, lakini waligoma kufanya vyote.
Baada ya hayo, Jaji Mutungi aliwahi kuiambia Mwananchi Digital kwamba, kutotekelezwa kwa barua yake, kunaonyesha haja ya kutoa elimu kwa wadau wote wa siasa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, leo Jumanne ya Agosti 1, 2023, Jaji Mutungi amesema wito huo haulengi matumbano na vyama vya siasa bali ni kuelimishana.
"Naomba niwaondoe hofu kwamba tumekuja hapa sio kurumbana kwamba kuna vyama vingapi vya siasa vinatumia viongozi wa dini, bali tumekuja hapa kuelimishana namna tunavyotakiwa kufanya siasa zetu.
"Nimelazimika kusema haya kwa sababu watu huko nje wanasubiri kwa hamu kwamba hili baraza litaisha kweli? Si watatumbuana macho?" Amesema.
Jaji Mutungi amesisitiza mkutano huo unalenga kufanya tafakuri ya lugha zinazopaswa kutumiwa katika siasa hasa kufuata sheria.
Katika ufuatiliaji wa mwenendo wa siasa nchini, amesema wameona haja ya kuitishwa mkutano huo ili kutoka na makubaliano ya muelekeo mzuri wa kisiasa.
Tamanio lake kupitia baraza hilo, amesema ni kuwepo taratibu zitakazofanya siasa zifanyike bila kulifikisha taifa kwenye mipasuko.
"Tunataka tuwekeane utaratibu kwamba ili isije kufika mahali tukaharibu mambo. Tunatarajia uzalendo na utu uzima kutoka kwenu," amesema.
Pamoja na hayo, Jaji Mutungi amevitaka vyama vya siasa visiiogope ofisi yake.
"Ofisi ya Msajili sio Kituo cha Polisi msiogope lakini Ofisi ya Msajili sio malaika kuna wakati tunakosea mnatakiwa mtueleze bwana mnakosea hapa," amesema.