Idris Sultan, wenzake waachiwa huru na mahakama

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia kesi na kumwachia huru msanii wa vichekesho, Idris Sultani na wenzake wawili baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia kesi na kumwachia huru msanii wa vichekesho, Idris Sultani na wenzake wawili baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Sultan na wenzake walikuwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na kibali.
Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo, umetolewa leo, Jumanne Agosti 17, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili wa Serikali, Neema Mosha, ameieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya Ushahidi, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Wakili Mosha, baada ya kueleza hayo, Hakimu Ruboroga, amesema kupitia kifungu hicho, Mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa wote na kuwaachia huru
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Doctor Ulimwengu(28)mkazi wa Mbezi Beach na Isihaka Mwinyimvua (22) mkazi wa Gongolamboto.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8, 2016 na Machi 13, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Loko Motion, walichapisha maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Imeandikwa na Hadija Jumanne na Robert Nole, Mwananchi [email protected]