Hukumu anayedaiwa kuua, kuteketeza mwili wa mkewe leo

Mshtakiwa Hamis Luwongo anayedaiwa kumteketeza mke wake kwa magunia mawili ya mkaa.
Muktasari:
- Mshtakiwa anadaiwa kuuchoma mwili wa mkewe kwa magunia mawili ya mkaa na kwenda kuzika majivu na masalia ya mifupa shambani kisha akapanda migomba.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Februari 26, 2025 inatarajia kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Hamis Luwongo, anayedaiwa kumuua mkewe kisha kuteketeza mwili wake kwa moto.
Hukumu inatarajiwa kusomwa saa 8:00 mchana na Jaji Hamidu Mwanga aliyesikiliza shauri hilo. Siku ya hukumu aliipanga Desemba 11, 2024.
Novemba 25, 2024 Mahakama iliamuru pande zote kufikia Desemba 10, ziwe zimeshawasilisha majumuisho ya hoja kwa lengo la kuishawishi Mahakama kuwa mshtakiwa ana hatia au hana hatia, na ikapanga kesi hiyo itajwe Desemba 11 kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu.
Katika kesi ya jinai namba 44/2023 mfanyabiashara huyo mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa kumuua mkewe Naomi Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku. Inadaiwa masalia ya mwili na majivu alikwenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake.
Upande wa mashitaka ulifunga ushahidi Novemba 18, 2024 baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, huku upande wa utetezi ukiufunga Novemba 19, 2024 baada ya kumuita shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe, bila kuwasilisha kielelezo chochote.
Mshtakiwa katika utetezi alikana kumuua mkewe akidai hajafa bali alitoroka na kwamba, taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto mwili wake akazika majivu na masalia yake shambani hazikuwa za kweli.
Alidai aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliomtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.
Mshtakiwa alieleza hata masalia ya mifupa aliyowaonyesha Polisi shambani kwake si ya mkewe bali ni ya mzoga alioukuta wakati akisafisha shamba lake na mingine ilisalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba lingine alilonunua eneo la Mwongozo, Kigamboni.
Alidai mifupa iliyofukuliwa na mafundi waliokuwa wakichimba udongo kutengeneza msingi wa nyumba aliyokuwa akiijenga, aliichukua na kwenda nayo shambani akaiweka pamoja na ya mzoga kisha akaichoma pamoja na takataka nyingine.
Alidai ndiyo maana hata uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali matokeo yake hayakutoa uthibitisho kuwa ni ya mkewe Naomi.
Upande wa mashitaka baada ya mshtakiwa kumaliza utetezi, uliiomba Mahakama iamuru daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Sadiki Mandari aitwe.
Dk Mandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba ndiye aliyemfanyia mshtakiwa uchunguzi wa afya ya akili kwa amri ya Mahakama.
Katika ripoti ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha wakati wa tukio la mauaji anayodaiwa kutenda mshtakiwa alikuwa na tatizo la kiakili.
Upande wa mashitaka uliiomba Mahakama daktari huyo aitwe kizimbani kwa ajili ya kumfanyia mahojiano kuhusu ripoti hiyo. Jaji Mwanga alikubali ombi hilo na akuamuru afike mahakamani kuhojiwa Novemba 25.
Alipohojiwa na mawakili wa pande zote kuhusu ripoti hiyo, Dk Mandari aliikana akidai haitambui, akiwasilisha nyingine inayoeleza wakati mshtakiwa akitenda kosa hilo hakuwa na tatizo la kiakili bali alikuwa na akili timamu.
Jaji Mwanga alionyesha kukasirishwa na hilo akahoji kwa nini mtaalamu kama yeye awasilishe mahakamani ripoti mbili tofauti katika kesi nyeti kama hiyo inayohusu maisha ya watu. Mshtakiwa alidai daktari huyo ameiaibisha taasisi yake.
Dk Mandari alipobanwa kwa maswali alisema kuna mmoja wa ndugu wa mshtakiwa alimpigia aende aitetee ripoti iliyoko mahakamani.
Alipoulizwa na Jaji kama alimweleza huyo ndugu wa mshtakiwa kuwa anakwenda na ripoti nyingine alijibu hakumwambia, alipoulizwa huyo ndugu wa mshtakiwa alijuaje kama anakwenda na ripoti nyingine alijibu hajui.