Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hoja NEMC kuwa mamlaka yawakosha wabunge

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni

Muktasari:

  • Wabunge wa Tanzania wamechangia marekebisho ya muswada madogo wa sheria ya Mazingira sura 191 wameitaka Serikali kupeleka muswada wa sheria ya kuanzisha Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka.

Dodoma. Katika kuhakikisha Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) linakuwa na meno zaidi ya kukabiliana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira, wabunge wameunga mkono lipandishwe hadhi ili kuwa mamlaka itakayokuwa na nguvu kubwa ya kisheria katika eneo hilo.  

Katika majadiliano, wabunge wamesema NEMC inapaswa kubadilishwa kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi Mazingira.

Mtazamo wa wabunge wameutoa leo Jumatano, Februari 12, 2025 wakati wakichangia muswada wa marekebisho madogo ya Sheria ya Mazingira sura 191 wameitaka Serikali kupeleka muswada wa sheria ya kuanzisha kwa mamlaka hiyo.

Awali, taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira imesema ni wakati mwafaka NEMC kuwa mamlaka ikizingatiwa kuwa nchi imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika suala la mazingira na uhifadhi wake.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Agness Hokololo amesema Serikali inatakiwa kupeleka bungeni muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili wapitishe sheria mpya.

"Sisi katika kamati moja ya mambo ambayo tunayatarajia ni kupata muswada mpya wa NEMC kuwa Nema pamoja na uchumi wa buluu," amesema mbunge huyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga amesema ni matamanio yao kumpatia Rais Samia Suluhu Hassan chombo chenye nguvu kitakachosimamia vyema mazingira ambayo yamekuwa yakiathiriwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

"Ni matamanio ya kamati kuona tunampatia Rais chombo chenye nguvu," amesema Kiswaga ambaye pia ni mbunge wa Kalenga.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya amesema mazingira inahitaji kuwa na chombo madhubuti kusimamia sekta hiyo akashauri Baraza la Mazingira lipandishwe kuwa na hadhi ya mamlaka itakayokuwa na uamuzi bora katika suala la mazingira wenye nguvu.

Mbunge wa Ngara, Profesa Shukran Elisha amesema ni muhimu Serikali ikawasilisha marekebisho makubwa ambayo yataboresha utendaji wa taasisi hiyo kuwa mamlaka itakayokuwa na nguvu za kiutendaji.

"Ni matarajio ya kamati katika Bunge lijalo uletwe muswada wa sheria kubadilisha Baraza la Taifa la Hifadhi Mazingira kuwa mamlaka," amesema Profesa Elisha akitaja baadhi ya changamoto inazopitia kwa sasa NEMC zinazoifanya ishindwe kusimamia vyema mazingira.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kuendelea kuwapo kwa matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilipigwa marufuku, utupaji taka katika fukwe za bahari na maziwa, uchimbaji wa madini usiozingatia uhifadhi wa mazingira, kelele hasa wakati wa usiku mitaani pamoja ujenzi katika vyanzo vya maji.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amesema ni wakati muafaka sasa kuwapo na mamlaka itakayokuwa na nguvu katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira.

Akitoa majumuisho ya michango ya wabunge, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni ameahidi Serikali itawasilisha muswada wa sheria ya usimamizi wa mazingira katika Bunge lijalo ambapo pamoja na mambo mengine ili kuipandisha hadhi NEMC kuwa mamlaka.