Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hivi ndivyo ma-RC, DC walivyosweka watu ndani

Muktasari:

Baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakiweka watu ndani mara kwa mara katika matukio tofauti, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na viongozi mbalimbali.



Dar es Salaam. Baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakiweka watu ndani mara kwa mara katika matukio tofauti, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na viongozi mbalimbali.

Jumanne wiki hii, Rais John Magufuli alipigilia msumari akiwataka wateule wake hao kutafakari kabla ya kuchukua hatua kama hiyo. Rais alizungumzia vitendo hivyo ambavyo vimewahi pia kulalamikiwa na wananchi, asasi za kiraia, viongozi wa dini, mawaziri na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo baada ya kumaliza kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani, Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Sio haki, viongozi wengi wamezungumza kuhusu hili na mimi narudia. Kwa sababu kama una mamlaka ya kuweka watu ndani ni sawa,” alisema Rais Magufuli.

“Mkuu wa mkoa wako naye akiamua akaweka watu ndani itakuwa ni vurugu na kuna masuala mengine hayahitaji kuweka watu ndani ni kutoa maelekezo tu.”

Kufuatia kauli hiyo ya mkuu wa nchi, Mwananchi linakuletea baadhi ya matukio ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kuwaweka ndani wananchi, watendaji walio chini yao na wanasiasa.

Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli, ni miongoni mwa wakuu ambao waliongoza kwa kuwaweka mahabusu viongozi wa vijiji, watumishi wa halmashauri akiwamo katibu tawala wa wilaya hiyo, Yusuph Kasuka.

Mbali ya Mbogho, kuna baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao wamekuwa wakichukua hatua kama hiyo akiwamo mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ambaye hivi karibuni alimweka ndani diwani wa viti maalumu (Chadema), Edna Mbise akimtuhumu kuficha saruji ambayo alikuwa amechukua kwa mfanyabiashara mmoja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Mbali na Muro, pia mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akiwa ziarani wilayani Karatu mwaka jana, aliagiza kukamatwa kwa wajumbe 24 wa bodi ya kiwanda cha maziwa na Chama cha Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos) cha Ayalabe wilayani humo kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh607 milioni.

Baada ya kukamatwa watuhumiwa hao, baadhi yao walifikishwa mahakamani na hadi sasa wapo nje kwa dhamana.

Kutoka Manyara, mwaka jana, wakuu wa wilaya za Mbulu, Simanjiro na Hanang’ waliagiza baadhi ya viongozi akiwamo mbunge, madiwani na watumishi wa Serikali kukamatwa na polisi.

Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Sarah Msafiri ambaye amehamishiwa Kigamboni, Dar es Salaam aliagiza kuwekwa ndani kwa mbunge wa Hanang’ (CCM), Dk Mary Nagu; mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Mathew Darema na baadhi ya madiwani wa halmashauri kwa madai ya kufanya uchochezi.

Hata hivyo, mbunge huyo na mwenyekiti hawakulazwa mahabusu, lakini walifika Kituo cha Polisi Katesh walikohojiwa na kuachiwa bila kufikishwa mahakamani.

Pia, mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliagiza madiwani wanne wa halmashauri hiyo kupitia CCM kulazwa mahabusu kwa madai ya kufanya uchochezi.

Chaula aliagiza diwani wa Orkesumet, Sendeu Laizer akamatwe na polisi kwa kufanya uchochezi wa mradi wa maji akishirikiana na baadhi ya wananchi na kisha afikishwe mahakamani.

Pia, aliagiza madiwani Tipay Ngaidiko (Msitu wa Tembo), Christopher Ole Kuya (Emboreet) na diwani wa viti maalumu, Diana Barnot wakamatwe kwa tuhuma za uchochezi, lakini hawakufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga aliagiza diwani wa Uhuru (Chadema), Felis Manimo akamatwe kwa uchochezi, lakini hakufikishwa mahakamani.

Mofuga pia aliwahi kuagiza baadhi ya watendaji wa Serikali ambao hawakutimiza wajibu wao ipasavyo walazwe mahabusu kwa saa 24, lakini hawakupelekwa mahakamani.

Huko Tabora, mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa alimweka ndani mfanyabiashara Abdul Hersi kwa kukaidi agizo lililomtaka kufukia mtaro uliokuwa unapeleka maji machafu msikitini.

Pia, alimweka ndani mwenyekiti wa chama cha msingi, Ibrahim Kagete kutokana na ubadhirifu kwenye chama hicho.

Kiongozi huyo alituhumiwa na bodi ya chama chake cha msingi kufuja fedha za ushirika na baada ya kuwekwa mahabusu alifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.

Pia, mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alimweka mahabusu ofisa mifugo msaidizi, Cornellius Massawe baada ya kulalamikiwa na wananchi na wafugaji wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wiki iliyopita.

Katika malalamiko yao, wafugaji walidai ofisa huyo amekuwa akiwanyanyasa kwa kuwatoza viwango vikubwa vya fedha huku akiwapa stakabadhi tofauti na kiwango wanacholipa.

Mkoani Kigoma, mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga alimtupa mahabusu kwa saa 48 diwani wa Kibirizi (ACT Wazalendo), Yunus Ruhomvya kwa madai kuwa alikataa kiongozi huyo asitumie ofisi ya mtendaji wa kata kufanya kikao cha kumwondoa madarakani mmoja wa wenyeviti wa mitaa kutoka chama hicho.

Matukio mengine

Novemba 2015, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliwaweka ndani maofisa ardhi kadhaa kwa saa sita.

Makonda alifanya hivyo akidai kuwa maofisa hao walikaidi agizo lake la kuwataka wawahi katika eneo la mkutano kusikiliza migogoro ya ardhi uliofanyika eneo la Nakasangawe, Kata ya Wazo.

Septemba mwaka jana, mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alimweka ndani kwa saa 48 diwani wa viti maalumu (Chadema), Silestina Jonso akidaiwa kusababisha nyumba ya moja ya mkazi mkoani humo kubomolewa.

Mkoa wa Kilimanjaro nao hauko nyuma, kwani mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo aliwahi kuwaweka ndani mtendaji wa Kijiji cha Kitangara, Dorice Bichumla na ofisa ustawi wa jamii wa wilaya, Victor Ombaikwa kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za wananchi zaidi ya Sh2 milioni.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliwaweka ndani mwekezaji wa mashamba ya kahawa ya Nkwansira ambaye pia ni diwani wa Okaoni (CCM), Moris Makoi; wakili wa kujitegemea Patricia Erick; vigogo kadhaa wa kampuni ya Kadco na baadhi ya viongozi wa Saccos ya Uswaa kwa madai ya ubadhirifu wa Sh126 milioni.

Agosti, mwaka jana mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliamuru kukamatwa kwa wananchi wa Kijiji cha Ngole, Kata ya Ilungu kwa madai ya kuharibu chanzo cha maji cha Mshewe.

Vilevile, Oktoba mwaka huo, Chalamila aliamuru kukamatwa na kuwekwa rumande kwa saa 48 diwani wa Isanga (Chadema), Anyandwile Mwalwiba na ofisa mtendaji wa kata hiyo, Robin Nzowa kwa madai ya kutafuna Sh1.8 milioni za ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi Ilolo.

Tukio lingine ni la Oktoba lilitokana na ziara yake ya kila kata ambako alimweka mahabusu kwa saa 24 katibu wa CCM Kata ya Manga, Norasco Tibakawa baada ya kudaiwa kutumia Sh20,000 za rambirambi za wananchi.

Chalamila pia aliamuru kuwekwa ndani kwa saa 24 watu kadhaa wa mji wa Rujewa wilayani Mbarali kwa kuingilia msafara wa makatibu wakuu 10 wa wizara tofauti waliofika wilayani humo kwa ziara ya kikazi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika aliamuru kuwekwa ndani diwani wa Itezi (Chadema), Ibrahim Mwaipwani kwa madai ya kufunga ofisi ya kata baada kuibuka sintofahamu kati ya diwani na mtendaji wa kata.

Vilevile, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa kabla ya uteuzi wake kutenguliwa, aliwaweka ndani madiwani wa kata za Chalangwa na Kambikatoo kwa kushindwa kusimamia shughuli za maendeleo.

Huko Mwanza, mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Colonel Magembe pia amewasweka watu ndani kwa tuhuma tofauti.

Magembe aliyeteuliwa kushika wadhifa huo Agosti, 2018 tayari amewasweka mahabusu baadhi ya viongozi na watendaji wa halmashauri, wanasiasa na wananchi.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Girigol Kalala ndiye aliyekuwa wa kwanza kuonja joto baada ya Magembe kuagiza awekwe mahabusu Desemba 2018 kwa madai ya kushindwa kusimamia maelekezo ya kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za kata yake ya Bukindo.

Desemba 14, 2018, ofisa mfawidhi wa ulinzi wa rasilimali ndani ya Ziwa Victoria Ukerewe, Judith Mugaya aliswekwa mahabusu kwa agizo la mkuu huyo wa wilaya baada ya kudaiwa kukaidi agizo la kusitisha operesheni dhidi ya uvuvi haramu.

Kadhalika, kaimu mhandisi ujenzi wa halmashauri hiyo, Ronald Muhanzi aliwekwa mahabusu kwa madai ya kushindwa kuwajibika katika nafasi yake.

Baadhi ya viongozi wa Serikali za vijiji na wananchi wa kawaida nao walijikuta wakinasa mikononi mwa Magembe baada ya kuwekwa mahabusu wakidaiwa ama kushindwa kusimamia au kushiriki utekelezaji wa agizo la ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za maeneo yao.

Vijiji vilivyokumbwa na matukio ya viongozi na wananchi wake kuwekwa mahabusu ni pamoja na Hamkoko, Bugombe, Muriti, Nyamanga, Chifule, Mulutilima na Kamasi.

Mwingine mkoani Mwanza ni mkuu wa Wilaya Misungwi, Juma Sweda ambaye aliagiza kuwekwa mahabusu kwa ofisa mazingira wa wilaya hiyo, Richard John kwa madai ya kuchelewa kufika kwenye tukio la utatuzi wa mgogoro wa uchafuzi wa mazingira.

Mwingine aliyewekwa mahabusu ni diwani wa Ukiliguru, Madoshi Marambo aliyedaiwa kuzuia wananchi kushiriki michango ya miradi ya maendeleo.

Vilevile, maofisa ardhi na watendaji wa Kijiji cha Nyang’homango walikamatwa kwa madai ya kusimamia uuzwaji wa ardhi kwa kampuni moja kijijini hapo.

Rungu la Sweda pia halikuwaacha salama baadhi ya watendaji wa kata waliodaiwa kukusanya mapato bila kutoa stakabadhi za kielekroniki.