Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hivi hapa viini, tiba migongano wateule wa Rais

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wakati akifunga mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa katika chuo cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani. Picha na Ikulu

Dar/Moshi. Migogoro na minyukano isiyokoma baina ya wakuu wa mikoa na wilaya dhidi ya makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri kwenye maeneo yao imewaibua baadhi watendaji wastaafu kwenye nafasi hizo wakibainisha kiini na kupendekeza suluhusho la hali hiyo.

Wameeleza hayo ikiwa ni mwezi mmoja tangu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki alipokemea hali hiyo akisema anatoa onyo la mwisho.

Kairuki alitoa onyo hilo Julai 4 mwaka huu, wakati semina ya makatibu tawala wa wilaya zote nchini iliyofunguliwa na Waziri Mkuu, Kassima Majaliwa.

Alisema uvumilivu na kuwanyamazia umefika mwisho na kwamba kuanzia sasa watakaobainika, watapelekwa kwa mamlaka ya uteuzi kwa uamuzi.

Kauli hiyo ya Kairuki, ilikuja baada ya ile ya, Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa Februari mwaka huu ameachana na mtindo wa kuwapangua badala yake atawaengua.

“Sipendi sana, nataka niwaambie, hii itakuwa mara ya mwisho kutumia sababu hii kupangua wizara, likijitokeza tena maana yake hamwezani na hamuwezi kufanya kazi, wote wawili mtakwenda,” alisema.

Ilifika hatua baadhi yao wakatumia madaraka yao kuwaweka wenzao ndani, na miongoni mwa walioonja shubiri hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga, Zefrin Lubuva na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Yusuph Kasuka ambao waliwekwa mahabusu na mkuu wa wilaya, Aaron Mbogho mwaka 2021.

Kiini cha mitifuano

Sababu zinazotajwa wa waliowahi kushika nyadhifa hizo mojawapo ni wakuu wa wilaya kukosa mafungu ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zao na hivyo ofisi zao kutegemea halmashauri kwenye masuala kadhaa.

Sababu nyingine ni kukosekana kwa semina elekezi kwa wateule wa Rais kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo wateule hao walipigwa msasa kujua wajibu na mipaka yao.

Mbali na sababu hizo, masilahi binafsi na rushwa vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu za mitifuano hiyo kwa baadhi yao na sababu nyingine ikiwa ni changamoto za kimuundo na kimamlaka, mwingiliano wa majukumu kati ya DED na DC na baadhi ya wateule kutafuta umaarufu binafsi wa kisiasa.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, Mkuu wa wilaya mstaafu, Raymond Mushi alisema masilahi binafsi na ujuaji ni miongoni mwa sababu za chanzo cha migogoro kwa baadhi ya viongozi wanaoteuliwa na mamlaka za juu.

Mushi ambaye alihudumu katika wilaya mbalimbali kwa miaka 23, anasema kiongozi asiye na misingi ya maadili ni kichocheo cha kutoelewana na viongozi wengine katika kutekeleza majukumu, kutokana na fikra na mitazamo tofauti.

“Kunaweza kukawa na misimamo tofauti kutokana na sababu mbalimbali, wakati mwingine ni tabia za watu tu haziendani kati ya hao wawili; kuna mmoja ambaye anafikiri kwamba hamuitaji mwenzake na kwamba peke yake anatosha,” alisema.

“Wote wanatakiwa watambue kuna DED na DC, ni lazima mkurugenzi atambue kuna umuhimu wa kushirikiana na mkuu wa wilaya na mkuu wa wilaya atambue kuna umuhimu wa kushirikiana na mkurugenzi wake,” alisisitiza.

Eneo lingine ni misimamo tofauti kuhusu masuala mbalimbali, kwamba huyu anasema hivi na yule anasema vile na wote wanatambua kila mmoja ni muhimu lakini huyu ana msimamo huu na yule ana msimamo mwingine kuhusu jambo hilohilo.

“DC na DED inapotokea hawaelewani wanatengeneza mwanya mkubwa sana na matokeo hasi ni mengi. Katika kazi mambo yao binafsi yasiingiliane na kazi, watu wengi ambao hawaelewani mambo yao yanaingia hadi kwenye kazi,” anasema.

DC huyo mstaafu anasema, “kwa hiyo kama kiongozi lazima umsome (mwenzako), umjue na ujue ni namna gani ya kummudu kwenda naye, sasa kama mwenye hiyo nafasi hana uzoefu mkubwa wa mambo mengi au hana uelewa wa mambo mengi.

“Tatizo linakuwa kubwa zaidi, kwasababu ule ujuzi wa kumudu mambo haufundishwi shuleni, watu wanajifunza kadri wanavyoishi na kadri wanavyofanya kazi ndio wanajifunza.”

Kwa upande wake, Aaron Mbogho pia aliyewahi kuwa DC, alisema kinachosababisha migogoro kati ya wateule hao ni kuwa na mitizamo tofauti na hasa wakuu wa mikoa na wilaya wanapokuwa wanataaluma, huwa hawapendi kudanganywa.

“Kwa mtizamo wangu mimi, migogoro ni mitizamo tofauti, mnapokutana kwenye jambo moja. Kwa mfano Ma-DC na Ma-RC ni wawakilishi wa Rais si watendaji. Wao wana sheria yao inayotumika kusimamia utendaji kazi wao,” alisema.

“Inapokuja hawa Ma-RAS au Ma-DED hawa ni watendaji na hawa ni wataalamu na wanakuwa na taaluma zao kuliko wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa. Unapokuwa ni DC au RC halafu una utaalamu fulani, hapo hutakubali kirahisi,” anasema,

“Anapokuja RAS au DAS akafanya ndivyo sivyo na wewe unajua kitaalamu si hivyo, kusema ukweli unakosa uvulimivu na uvumilivu. Ni gharama sana kuvumilia kwa sababu unajikana ili kuendana na msimamo ambao si wa kwako.

“Sasa unapokutana na hali kama hiyo na mara nyingi hiyo migogoro inaonekana inalipukia kwa Ma-RC na Ma-DC kuliko Ma-DED au Ma-RAS au DAS ambao ni watendaji kwa sababu wanasiasa hao kiutawala wao wako juu ya hao watendaji,” alisema.

Mikoa isimamie wilaya

Kutokana na kukithiri kwa hali hiyo, moja wa viongozi aliyewahi kuwa katibu tawala wa mkoa (RAS) amesema mwarobaini wa tatizo hilo ni kurudisha mifumo ya madaraka mikoani uliokuwepo nchini mwaka 1974.

RAS huyo mstaafu aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema viongozi kugombana unatokana na changamoto ya kimuundo, kwa sababu viongozi wa mikoa na wilaya wote wanaripoti Tamisemi kulingana na sheria ilivyo.

“Ili kuondoa hii changamoto, inapaswa viongozi wa mikoa wawe ni mamlaka ya kinidhamu ya wilaya na ikifanyika hiyo hautakuja kuona migogoro ya viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa,” alisema.

“Turudishe mifumo ya madaraka mikoani uliokuwepo mwaka 1974 uliofutwa, ambao kwao mkoa ni mamlaka ya nidhamu kwa ngazi ya wilaya, itaongeza ufanisi kwani wote hawatakwenda kulalamikia wizarani,” alisisitiza

Mstaafu huyo alisema ni vigumu Tamisemi kuendesha mamlaka 185 zote kutoka Dodoma, “kuna baadhi ya halmashauri ni kubwa kuliko hata wizara, chukulia Kinondoni ya Dar es Salaam ina bajeti kubwa kuliko hata baadhi ya wizara,” alisema.

Alisema mikoa ikishapewa mamlaka kuziongoza wilaya, wizara iongoze mikoa na iwe mamlaka ya rufaa ya halmashauri, hii itarahisisha usimamizi na itaongeza ufanisi kwa halmashauri.

“Utaratibu wa sasa hivi, unaweza kukuta mkurugenzi au mkuu wa wilaya anakuwa na nguvu kuliko RAS na au mkuu wa mkoa na hii kwa sababu unakuta huyo DED au DC ana watu Tamisemi, hivyo anaona wewe RC au RAS utamfanya nini,” alibainisha.

“Ushauri huu umekuwa ukitolewa kwa muda mrefu na Tamisemi hawaukubali kwa sababu ya masilahi na watendaji wenyewe wa Tamisemi kwenye halmashauri na wilaya.

Mikoa iko karibu na halmashauri na wilaya, inawaona wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwa ukaribu zaidi, wanajua kila kinachoendelea, lakini sasa kukiwa na tatizo upeleke tuhuma au malalamiko Dodoma, mwisho mtaishia kubishana tu na mambo yanaendelea yaleyale.”