Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hifadhi ya jamii ni nini, inafanyaje kazi?

Muktasari:

Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imesema changamoto inayolalamikiwa na baadhi ya wastaafu haihitaji mabadiliko ya sheria wala kanuni bali wastaafu kuelewana na mifuko husika ili iwaongezee muda wa marejesho ya mkopo.

Dar es Salaam. Mjadala kuhusu fomula mpya inayotumiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kukokotoa mafao kwa wastaafu bado unaendelea. Kwa mujibu wa fomula hii, wastaafu wote sasa watapewa asilimia 25 ya mafao yao kwa mkupuo na asilimia 75 itakayobaki watakuwa wakipewa kwa kila mwezi mpaka kifo.

Hatua hii imelalamikiwa na baadhi ya wananchi wanaodai kuunganishwa kwa mifuko kumepunguza viwango vya pensheni. Serikali imekanusha madai haya ikisema kwamba kanuni inayotumika siyo mpya na kwamba vikokotoo hivyo vimeshaanza kutumika tangu mwaka 2014.

Serikali inasisitiza kuwa kanuni mpya ya hifadhi ya mfuko wa jamii ya 2018 imeondoa ‘ubaguzi’ kwa watumishi wa sekta binafsi na Serikali ambao sasa watatumia kikokotoo kinachofanana.

Katikati ya mvutano huu, ni suala lenyewe la hifadhi ya jamii ambayo faida yake na ufanyaji kazi wa mifuko kadhaa inayotoa huduma hiyo huwekwa pembeni bila kujadiliwa kwa kina. Hii huwanyima fursa wananchi kujionea picha kubwa ya jambo lenyewe hivyo kuminya uwezo wao wa kushiriki mijadala yake.

Hifadhi ya jamii ni nini?

Hifadhi ya jamii ni mpango uliobuniwa tangu enzi na enzi kutoa ulinzi wa kijamii miongoni mwa wanajamii husika.

Ni utaratibu wenye historia ndefu ikitajwa kuanza tangu zama zinazojulikana kwa kimombo kama Paleolithic, ambazo ni zama zilizohusisha utumiaji wa zana za mawe, takribani miaka milioni mbili iliyopita.

Katika zama hizo, wanahistoria wanaeleza kuwa binadamu walikuwa wakiishi katika makundi, ambayo kwa kimombo yalijulikana kama bands, yaliyoundwa kwa lengo la kutoa ulinzi wa kiuchumi na kijamii kwa wanachama wake.

Kutokana na changamoto zilizokuwa zinawakabili binadamu hawa wa kale katika kujitafutia maendeleo, wanachama wa makundi haya walikuwa wakisaidiana wao kwa wao kwa manufaa yao ya kimwili na kiuchumi.

Makundi haya ya wanajamii yaliendelea kuwepo zama nyingi zilizofuatia mpaka pale Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Desemba 10, 1948 ulipoasisi tamko lake mashuhuri la Azimio la Haki za Binadamu.

Sehemu ya 22 ya azimio hili lilihitaji kila mtu katika jamii apatiwe ulinzi, huku likisisitiza, “kila mwanachama wa jamii yoyote, ana haki ya hifadhi ya jamii kupitia juhudi za kitaifa na ushirikiano wa kimataifa (na) kulingana na mpangilio na rasilimali za kila nchi na hali za kisiasa na kiuchumi ya nchi husika.”

Kufuatia azimio hilo, Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) lilianzisha Sheria ya Hifadhi ya Jamii Namba 102 katika mkutano wake wa 35 mwaka 1952 na kubainisha walau mafao tisa yaweze kutolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii. Haya ni pamoja na mafao ya uzeeni, ulemavu, fao la warithi, majeruhi katika ajira, uzazi, afya, ugonjwa, kukosa ajira na kifo.

Vipi kuhusu Tanzania?

Hifadhi ya jamii nchini Tanzania inatajwa kuwepo hata kabla ya ujio wa wakoloni. Kabla ya wakoloni kuwasili nchini, wanahistoria wanabainisha kwamba tayari kulikuwepo na aina na miundo fulani ya ulinzi wa kijamii ambao ulikuwa ukiendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kimila na desturi za jamii husika.

Utaratibu huu usio rasmi na wa kimila ulijikita katika msaada wa kifamilia na kijamii.

Mfumo rasmi (wa sheria na mifuko) uliopo leo wa hifadhi ya jamii ni matokeo ya urithi wa wakoloni ambao walianzisha hifadhi ya jamii kukidhi matakwa ya Wazungu na Watanzania wachache waliokuwa wakifanya kazi katika Serikali ya kikoloni.

Inadaiwa kuwa Tanzania, Kenya na Uganda baada ya kupata uhuru hazikubadili sana miundo hii rasmi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa na wakoloni licha ya kuwa na mapungufu mengi sana. Wataalamu wengi wa masuala ya hifadhi ya jamii wamehusisha hatua hii na matatizo kadhaa yanayoigubika mifuko mingi ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa.

Inafanyaje kazi?

Mifuko ya hifadhi ya jamii ni maalumu kwa ajili ya kumsaidia mfanyakazi kumudu mahitaji ya uzeeni pindi anapostaafu au mengine yaliyotajwa hapo juu.

Sababu kubwa iliyosababisha kuwepo mifuko ya hifadhi ya jamii ni baada ya kubainika kuwa wakati wa ujana, wafanyakazi wengi hushindwa kujiwekea akiba ya kutosha kukidhi mahitaji ya uzeeni au kumudu gharama za maisha yao pindi itokeapo hali yoyote ya kutojiweza.

Tofauti na benki au taasisi nyingine za kifedha, mifuko ya hifadhi hii hutoa mafao kwa mteja wake pindi awapo na uhitaji wa kidharura (maradhi, ulemavu au hali nyingine ya kutojiweza) au kustaafu kazi kwa misingi ya uzee kwa mujibu wa sera za kazi na utumishi na si vinginevyo.

Kwa mantiki hiyo mteja wa mfuko husika hawezi kudai mafao yake kwa misingi yoyote ile tofauti na ile iliyowekwa na mfuko husika ( mfano kuhitaji pesa kwa ajili ya kuanzisha biashara, kununua vyombo vya starehe kama gari, pikipiki na vinginevyo).

Kwa hiyo, bila uhitaji wa namna hiyo mteja hawezi kulipwa mafao yake ya aina yoyote ile hadi atakapofikia umri wa kustaafu iwe kwa hiyari au lazima ambao kwa Tanzania ni miaka 55 hadi 60.

Mifuko hii ni kama ilivyo sera ya bima yaani mtu hulipwa anapopatwa na janga.

Kwa nini ni muhimu?

Kutokana na hali ya maisha kuwa duni, wafanyakazi wengi hujikuta wakiishi maisha magumu mara baada ya kumaliza muda wa utumishi (kustaafu).

Lakini pia hata kabla ya kustaafu, wafanyakazi hujikuta wakipitia hali ngumu za maisha kutokana na maradhi au ulemavu ambavyo huweza kusababisha kupungukiwa au kukosa kabisa kipato hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu na za kimaisha kwa ujumla.

Hiki ndicho kipindi ambacho umuhimu wa mifuko hii huonekana, kwani baada ya kuridhika kuwa mteja anastahili huduma kutoka kwenye mfuko husika, hupatiwa gharama za matibabu na matunzo kutoka katika mfuko huo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Huduma hizi hutolewa endapo tu kama zimetajwa kama manufaa ya mfuko husika kwa wateja wake.

Ingawa kumekuwa na changamoto katika upatikanaji mafao haya kutoka kwa wateja wa mifuko mbali mbali kitu ambacho kimekuwa kikiibua mijadala na malalamiko ya mara kwa mara, wadau wengi wanakubaliana kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni muhimu si kwa mwanachama tu bali kwa taifa na maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii pia.