Halotel yazindua huduma kuimrisha usalama wa wateja wake

Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara kutoka Kampuni ya Halotel, Abdallah Salum, akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma mpya itakatosaidia mteja kujihudumia kwa kutoa taarifa, inajulikanayo kama Miss Halo.
Dar es Salaam. Katika kukabiliana na wizi wa fedha mtandaoni pamoja na utapeli unaofanywa na watu wasio waaminifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Kampuni ya Mawasiliano ya Halotel imezindua huduma mpya inayolenga kutatua changamoto hiyo.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Halotel, Abdallah Salum, amesema huduma hiyo mpya inajulikana kama Miss Halo, mfumo wa chatbot unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na kuwasaidia kujihudumia kwa haraka na kwa urahisi.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Halotel, Roxana Kadio akizunguma wakati wa uzinduzi wa huduma mpya inayojulikana kama Miss Halo.
Akizungumza leo Machi 20, 2025, wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Salum alisema kuwa Miss Halo inamuwezesha mteja wa Halotel kutoa taarifa za mashaka juu ya miamala au mawasiliano yasiyo salama ili kupunguza visa vya utapeli mtandaoni.
"Sekta ya mawasiliano inashuhudia mageuzi makubwa, hivyo ni muhimu kuwa na ubunifu na ufanisi ili kuhakikisha wateja wanapata msaada wa haraka na wa kuaminika," amesema Salum.
Ameongeza kuwa hapo awali wateja walilazimika kupiga simu kwa namba 100 au kufika ofisini kueleza shida zao, lakini kupitia Miss Halo, wateja sasa wanaweza kujihudumia kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp kwa namba 0620100100.
Salum amesema kuwa Halotel imezingatia viwango vya juu vya usalama wa taarifa za wateja katika huduma hiyo mpya ili kuhakikisha faragha yao inalindwa.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Wateja kutoka Halotel, Shaban Said akizunguma wakati wa uzinduzi wa huduma mpya inayojulikana kama Miss Halo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Halotel, Shaban Said, alisema huduma hiyo pia inawawezesha wateja kuangalia salio, kununua vifurushi na kupata huduma nyingine kwa urahisi.
"Huduma hii itaendelea kutatua matatizo ya kawaida na kutoa majibu moja kwa moja, hivyo kupunguza muda wa kusubiri. Tumerahisisha matumizi yake kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza," amesema Said.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Halotel, Roxana Kadio, alisema kuwa kampuni hiyo inaendelea kuimarisha sifa yake kama chapa inayojali wateja wake kwa kutoa si tu huduma bora za mawasiliano, bali pia uzoefu unaoboresha maisha ya watumiaji wake.
"Tunawahimiza wateja wetu kutumia huduma hii kwani ni rahisi, ya haraka na yenye usalama wa hali ya juu," amesema Kadio.