Halmashauri Jiji la Arusha yakabidhi hundi Sh2.6 bilioni kwa vikundi 169

Arusha. Halmashauri ya jiji la Arusha imekabidhi hundi ya Sh2.6 bilioni kwa vikundi 169 vya wanawake, vijana na walemavu vilivyokidhi vigezo vya kikanuni kupata mikopo hiyo.
Akizungumza leo Machi 22, 2023 jijini Arusha Kaimu Mkurugenzi jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro amesema jumla ya vikundi 205 viliwasilisha maombi yao kwenye mfumo wa TPLMIS, ambapo uhakiki ulifanyika na kubaini kuwa vikundi saba vimejikita katika shughuli zenye mwelekeo wa uzalishaji kupitia vikundi vidogovidogo na usindikaji.
Aidha amesema vikundi 28 vinafanya miradi ya uzafirishaji 77 vinajihusisha na miradi ya kilimo na ufugaji na vikundi 93 vinajihusisha na biashara na ujasiriamali ambapo katika hivyo vikundi 169 ndivyo vilivyokidhi vigezo.
Aidha amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanzia Julai hadi sasa hivi walishatoa kiasi cha Sh3.9 bilioni kwa vikundi 339 hadi sasa hivi ambapo zimewawezesha kutengeneza ajira mbalimbali kwa makundi hayo.
Amesema kati ya vikundi hivyo jumla ya vikundi 127 ni vya wanawake huku vikundi vya vijana vikiwa 32 na watu wenye ulemavu vikiwa 10 .
"Haijawahi kutokea jiji la Arusha kupata mikopo ya fedha nyingi hivi, hivyo tunawaomba sana mnaopatiwa mikopo hii leo mkawe warejeshaji wazuri na mkarejeshe kwa wakati ili na wenzenu waweze kunufaika kupitia mikopo hiyo na kujikwamua kiuchumi," amesema Chitukuro
Naye Mkuu wa wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amepongeza jitihada hizo za jiji la Arusha kuhakikisha makundi hayo yanawezeshwa na kujikwamua kiuchumi na haijawahi kutokea halmashauri kutoa kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo.
Amesema mikopo hiyo ina nia mjema ya kuwakomboa wananchi wake kutoka kwenye hali duni zaidi ili waweze kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.
"Nawaomba sana mkafanye biashara zenye ubunifu ili muweze kurejesha kwa wakati na wenzenu wengine waweze kupata na hata kuiga mfano kutoka kwenu kwani itawasaidia kutoka sehemu moja kwenda nyingine," amesema Mtahengerwa.
Meya wa jiji la Arusha, Maximilian Iraghe amesema kwa mara ya kwanza jiji la Arusha limevunjuka rekodi ya kutoa pesa nyingi kupitia mapato ya fedha za ndani .
Amesema kuwa Arusha mapato yameongezeka kutoka Sh30.5 bilioni kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh60.6 kwa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 100 .
"Kupitia fedha hizi zilizotolewa leo tunatarajia kuwa na jiji la Arusha litabadilika na vijana kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali na hatimaye kuweza kutengeneza ajira kwa vijana wengine," amesema Iraghe.
Kwa upande wake Mjasiriamali kutoka kikundi cha Genevaglory kutoka Kaloleni, Neema Koya amesema kuwa mikopo hiyo itawasaidia sana kujikwamua kiuchumi na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali huku wakijitahidi kurejesha kwa wakati.