Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hakimu akerwa upelelezi kesi ya Zumaridi kuchelewa

Mshtakiwa pekee kwenye kesi ya Jinai namba 11/2022 Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi akiwa ndani ya mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza. Kwenye kesi hiyo Zumaridi anakabiliwa na shtaka la kufanya usafirishaji haramu wa binadamu.

Muktasari:

  • Hakimu akerwa upelelezi kesi ya Zumaridi kutokamilika, kauli ya Rais Samia kuhusu kukamatwa watuhumiwa kabla ya upelelezi kukamilika yaibuliwa mahakamani

Mwanza. Kesi namba 11/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi peke yake imegeuka kuwa kaa la moto kwa Serikali baada ya mawakili wa utetezi kuhoji kwa nini upelelezi wa kesi hiyo haukamiliki wakati ni miezi sita tangu mteja wao ashikiliwe.

 Hayo yamejitokeza leo Agosti 31, 2022 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Mwanza kwa hakimu anayesikiliza, Monica Ndyekobora huku mwendesha mashtaka wa serikali, Dorcas Akyoo akiieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

 Maelezo ya Akyoo yamepingwa vikali na jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Wakili, Steven Kitale, Erick Mutta na Linus Amri ambapo wakili Kitale amesema suala la upelelezi wa kesi kutokamilika linachelewesha mteja wao kupata haki.

 Kitale pia, amelitaka Jeshi la Polisi kuanza utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa hivi karibuni alipokuwa akifungua mafunzo kwa maofisa wa jeshi hilo mkoani Kilimanjaro ambapo alimtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai kukamilisha upelelezi kwanza ndiyo mtuhumiwa akamatwe.

 "Mheshimiwa hakimu naomba upande wa mashtaka wazingatie maelekezo ya mama yetu Rais Samia aliyotoa jana kwa Polisi. Ikiwezekana kesi ya Zumaridi iwe ya mfano kwa kumuachia ili wakafanye upelelezi wao wakatapokamilisha na ikabainika ana kosa ndiyo wamkamate," ameeleza Kitale

 Katika hatua nyingine, Kitale ameieleza mahakama hiyo kuwa Mei 24 mwaka huu alimuandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) barua yenye kumbukumbu namba ONL/MWZ/VOL 02/54/2022 akilalamikia ucheleweshwaji wa shauri hilo linalomkabili mteja wake kwa kile kinachotajwa kuwa ni kutokamilika kwa upelelezi.

 Kitale ameeleza kuwa katika aya ya pili ya barua hiyo alieleza wazi kwamba katika uendeshwaji wa kesi tajwa kumekuwepo na mahairisho mengi yasiyo na ukomo wala sababu zozote za msingi zaidi ya upande wa mashtaka kusema kuwa upelelezi haujakamilika.

 Pia, ameieleza mahakama hiyo kuwa Jana Agosti 30, 2022 jopo la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo walimuandikia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, John Kahyoza barua yenye kumbukumbu namba MAA/BR/CC.11/2022 likilalamikia shauri hilo kuahirishwa kwa zaidi ya miezi sita.

 Katika maelezo yake, Kitale ameieleza mahakama hiyo kuwa sababu kubwa inayotajwa kusababisha shauri hilo kuahirishwa kuwa ni upelelezi wake kutokamilika na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza wala kutoa uamuzi juu ya mashtaka yanayomkabili mteja wao.

 Kwenye barua hiyo pia, jopo la mawakili wa utetezi lilimuomba Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo kutumia mamlaka yake ya usimamizi kuliitisha jalada la kesi hiyo ili kulitolea maelekezo muhimu ikizingatiwa kwamba haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa.

 Kwa upande wake, Hakimu Monica amemgeukia mwendesha mashtaka wa serikali, Dorcas Akyoo akimuuliza iwapo amesikia malalamiko yaliyowasilishwa na mawakili wa utetezi kuhusiana upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika huku Akyoo akikiri kupokea malalamiko hayo bila kueleza hatua zilizochukuliwa na upande wa Jamhuri.

 Baada ya majibu ya Akyoo, Hakimu Monica ameeleza mahakamani hapo kuwa anakwenda kusoma sheria mbalimbali na kanuni ili kuona iwapo kuna kifungu kinachomruhusu kupeleka faili hilo katika ngazi ya juu.

 "Suala hili liliwahi kulalamikiwa na mshtakiwa mwenyewe hapa mahamakamani, nikakuagiza mwendesha mashtaka ukamilishe upelelezi haraka iwekezanavyo lakini haujanipatia taarifa yoyote," ameeleza hakimu Monica

 Ameongeza; "Sasa naenda kupitia sheria kama kuna kifungu kinaniruhusu kulipeleka ngazi ya juu nitafanya hivyo ili Septemba 9 mwaka huu tutakapokutana hapa nitoe maamuzi,"