Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Giza nene mabinti waliotoweka Arusha, Polisi yasema...

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa familia, wasichana hao waliondoka Juni 20, 2025 wakielekea kwenye sherehe ya kupongezana baada ya kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza, lakini hawakuwahi kurejea nyumbani na hawajaonekana hadi sasa.



Arusha. Mwaka mmoja sasa umepita tangu wasichana wawili, Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu kama ‘Rahma’ (22), kutoweka katika mazingira ya kutatanisha mkoani Arusha, huku familia zao zikizidi kuomba msaada wa mashirika ya haki za binadamu ili kusaidia kupatikana kwa ndugu zao hao.

Wasichana hao wanadaiwa kutoweka Juni 20, 2025, baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kutokana na kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza chuoni.

Katika tukio hilo, mfanyabiashara Godwin Ndossi alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 22, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea.

“Upelelezi wa tukio si wa siku moja, hivyo mkiambiwa unaendelea muwe na subira. Kazi bado inaendelea,” amesema Kamanda Masejo.

Baba mdogo wa Nakivona, Kakai Daudi, naye akizungumza na Mwananchi, amesema familia zinaendelea kusubiri majibu kutoka Jeshi la Polisi kuhusu hatma ya tukio hilo.

“Swali hili lina sintofahamu kubwa, hatuna cha kufanya zaidi ya kusubiri majibu ya Polisi,” amesema.

Kwa upande wake, dada wa Kareen, Elizabeth Didas amesema familia bado ipo katika hali ya maumivu na wasiwasi, huku ikiiomba Serikali na mashirika ya haki za binadamu kusaidia kufuatilia suala hilo.

“Tuko njia panda, hatuoni chochote kutoka Polisi. Tunaomba wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya kimataifa yatusaidie,” amesema.

Ameongeza kuwa hali ya mama yao inazidi kuwa mbaya kiafya kutokana na mshtuko wa kutoweka kwa mtoto wake, hali iliyosababisha kupooza kwa mwili na kuendelea kudhoofika.

“Tumechoka kusubiri Polisi. Kila siku tunaambiwa upelelezi unaendelea lakini hakuna kinachoonekana,” ameongeza.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, tukio la kupotea kwa wasichana hao lilianza kujadiliwa mitandaoni Mei 2, 2026, ambapo ilielezwa kuwa walialikwa katika sherehe ya usiku na mfanyabiashara Godwin Ndossi.

Inadaiwa kuwa wasichana hao walihudhuria sherehe hiyo Juni 20, 2025 katika eneo la Shangarai, wilayani Arumeru, na tangu wakati huo hawajawahi kuonekana tena.

Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tengeru na kupewa jalada namba TEG/RB/342/2025.

Kareen alikuwa akiishi Shangarai, Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogo ndogo huku akisoma uhasibu kupitia Chuo Huria cha Tanzania (OUT) kwa njia ya mtandao. Kwa upande wa Nakivona, alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), akihitimisha mwaka wake wa kwanza wa masomo kabla ya kutoweka.