Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbunge aliyependekeza bodaboda kutozwa Sh1,000 afafanua tena

Muktasari:

  • Msimamo wa sasa wa Mwalunenge hakupendekeza bodaboda wakatwe au wachangishwe Sh1,000 kwa ajili ya kujenga barabara; isipokuwa mfano wake ulikuwa wa kuonesha uwezo wao wa kujikusanyia mitaji na kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo

Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Patrick Mwalunenge ameibuka na kutoa ufafanuzi baada ya kutoa kauli bungeni kuhusu bodaboda, bajaji na machinga kuchangia Sh1,000 kujenga barabara kuzua mjadala mtandaoni.

Katika utetezi wake alioutoa Juni 20,2026 jimboni kwake kwenye kikao na madereva bodaboda na bajaji, amedai baadhi ya watu mitandaoni wameipotosha kauli yake na kuifanya ionekane kana kwamba mbunge anataka kundi hilo wachangishwe Sh1,000 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Amesema yeye alimaanisha Serikali isiyadharau makundi hayo, bali iyarasimishe, yatambulike na yaheshimike kwa kazi wanazofanya.

“Mtu anatoka kwa masilahi yake na kusambaza taarifa kwamba bodaboda wachangie Sh1,000 kujenga barabara. Kazi ya kujenga barabara ni ya Serikali, ambayo hujenga barabara kwa kutumia mapato yanayotokana na sekta mbalimbali, ikiwamo mafuta mnayonunua,” alisema Mwalunenge Jana.

Akichangia mjadala katika kikao cha 53 cha Bunge Juni 19, 2026, Mwalunenge alisema makundi ya bodaboda, bajaji na machinga si maskini kama wengi wanavyodhani, bali yana mchango mkubwa katika uchumi na uwezo wa kujijengea nguvu za kifedha.

Alitolea mfano Jimbo la Mbeya Mjini lenye zaidi ya waendesha bodaboda na bajaji 10,000, akisema kama kila mmoja angechangia Sh1,000 kwa siku, wangekusanya takribani Sh10 milioni kwa siku na zaidi ya Sh100 milioni kwa mwezi.

Mbunge huyo aliishauri Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, kuyaingiza makundi hayo katika mifumo rasmi ya kiuchumi ili yaweze kujikusanyia fedha, kujikopesha na kujikatia bima badala ya kutegemea fedha za halmashauri zinazotokana na mapato ya ndani.

Aidha, alisema makundi hayo yakirasimishwa na kutambuliwa rasmi katika sekta ya uchumi, yataweza kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo kampuni za ujenzi na shughuli nyingine za uwekezaji kama vile ujenzi wa barabara.

Hata hivyo, kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa mitandaoni. Baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji walimtuhumu kutaka kulibebesha kundi hilo jukumu la kujenga barabara, licha ya wao kulipa tozo mbalimbali kupitia mafuta wanayotumia.


Akaliwa kooni

Juni 20, 2026, Mwalunenge aliitisha mkutano na waendesha bodaboda na bajaji wa Mbeya Mjini kwa lengo la kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake. Katika mkutano huo, baadhi ya waendesha bodaboda walionekana kususia na kuondoka ukumbini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwalunenge alisema kauli yake imepotoshwa na kupewa tafsiri tofauti na alivyokusudia.

“Nilichosema ni kwamba bodaboda, machinga, bajaji na mamalishe wana uwezo wa kujitengenezea fedha zao wenyewe na kuwa matajiri. Serikali isiyadharau makundi haya, bali iyarasimishe, yatambulike na yaheshimike kwa kazi wanazofanya,” alisema.

Alisisitiza kuwa hakumaanisha bodaboda wachangishwe fedha kwa ajili ya kujenga barabara, akieleza kuwa jukumu hilo ni la Serikali.

“Mtu anatoka kwa masilahi yake na kusambaza taarifa kwamba bodaboda wachangie Sh1,000 kujenga barabara. Kazi ya kujenga barabara ni ya Serikali, ambayo hujenga barabara kwa kutumia mapato yanayotokana na sekta mbalimbali, ikiwemo mafuta mnayonunua,” alisema.

Mwalunenge alisema hoja yake ilikuwa kuhamasisha makundi hayo kutumia nguvu yao ya kiuchumi kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo.

“Nilimaanisha bodaboda wanaweza kuanzisha kampuni ya ujenzi, kununua mitambo na hata kushindania zabuni za Serikali za ujenzi wa barabara. Ninyi ni matajiri, lakini msiwe matajiri wa kufikiria kuendesha bodaboda maisha yenu yote. Mnaweza kuwekeza katika mashamba makubwa na miradi mingine ya maendeleo,” alisema.

Mbunge huyo aliongeza dhamira yake siku zote imekuwa kuwawezesha vijana wa bodaboda, bajaji na machinga kuinuka kiuchumi kupitia mitaji na mifumo ya kujitegemea.

“Tangu kampeni zangu nimekuwa nikitaka bodaboda, machinga na bajaji watajirike. Nataka niwatafutie mitaji, lakini pia waanze kujijengea uwezo kwa kujikusanyia fedha zao wenyewe. Kauli hizi zisiwaondoe kwenye reli vijana wangu wa bodaboda wa Mbeya,” alisema.

Pia alidai kuna watu wanaofurahia kuona makundi hayo yakiendelea kuwa katika hali ngumu za maisha na hupinga juhudi zozote zinazolenga kuyawezesha kiuchumi.

Alisema lengo lake siku zote limekuwa kuwawezesha vijana wa bodaboda, machinga na bajaji kujikwamua kiuchumi kwa kuwatafutia mitaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuanza na juhudi za kujichangisha wenyewe.

“Kuanzia kipindi cha kampeni hadi leo, nimekuwa nikitamani kuona bodaboda, machinga na bajaji wakitajirika. Kauli hizi za upotoshaji zisiwaondoe kwenye malengo yenu. Jambo ambalo Mungu amepanga lifanikiwe, litafanikiwa, kwani hila haijawahi kushinda,” alisema

Jana, akiwa Songea katika mkutano wa hadhara, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche alikosoa pendekezo la mbunge huyo la kutaka waendesha bodaboda na wamachinga wachangie Sh1,000 kila siku kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

“Mimi nilikuwa nikiangalia kwenye runinga nikamsikia mtu anayeitwa mbunge wa Mbeya Mjini akipendekeza kuwa bodaboda na machinga si maskini, hivyo kila siku wanapaswa kuchangia Sh1,000 kwa ajili ya kujenga barabara. Fikiria mtu analala na kuamka akiwa na hoja ya namna hiyo,” alisema Heche.

Heche alisema hoja hiyo haina msingi na haiwezi kutetewa kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni. Alidai kuwa ni muendelezo wa kuwanyanyasa Watanzania bila kuzingatia ugumu wa maisha wanaopitia.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Janeth Rithe, amesema si sahihi kupendekeza wamachinga na waendesha bodaboda wakatwe Sh1,000 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Rithe amesema katika kila lita moja ya mafuta kuna tozo ya Sh1,500 ambayo waendesha bodaboda tayari wanaichangia. Alishangazwa na pendekezo la kuongeza mchango mwingine kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Rithe, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu, amesema wamachinga na bodaboda ni makundi muhimu katika kuchangia maendeleo ya nchi, lakini wengi wao ni watu wa kipato cha chini.

“Hawa wamachinga ni kundi maalumu katika maendeleo, na bodaboda pia ni kundi muhimu katika kuchangia maendeleo. Ni watu wenye kipato cha chini, lakini tunaona kuna jitihada za kuwakandamiza na kuwanyonya badala ya kuwasaidia kuboresha maisha yao,” amesema.

Amesema hawawezi kuendelea kukaa kimya huku wananchi wakinyanyaswa, akidai kuwa kuna fedha nyingi zinazopotea bila uwajibikaji wa kutosha.Badala ya kuhoji matumizi ya fedha hizo, baadhi ya wawakilishi wanatoa mapendekezo yanayoongeza mzigo kwa wananchi maskini.