Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gavana ataka wanaoshikilia Dola kukaa chonjo

Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba

Muktasari:

 Serikali imesema itaendelea kuongeza mzunguko wa Dola kwa kadri inavyozipata na kuziingiza kwenye uchumi ili kuziba nakisi iliyopo.

Unguja. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa angalizo kwa wafanyabiashara wanaoendelea kushikilia Dola za Marekani ikisema watapata hasara siku za usoni kwa sababu ya mwenendo wa uchumi wa nchi na dunia unaoshuhudiwa.

Akizungumza leo Machi 22, 2024 katika mkutano na wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii Zanzibar uliofanyika ofisi za BoT Unguja, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba amesema baadhi ya changamoto zilizosababisha uhaba wa Dola sasa zimeanza kupatiwa ufumbuzi.

“Mlipuko wa Uviko-19 na njia zake za kukabiliana nao ulisababisha athari kubwa, watu walisitisha safari lakini sasa tunaona hata watalii nchini wanaongezeka. Vita vya Ukraine na Russia navyo vilileta athari kubwa za mnyororo wa usambazaji lakini changamoto zake zilizoibuliwa zimefanyiwa kazi na sasa mambo yanaenda vizuri,” amesema.

Gavana Tutuba amesema kutokana na mipango iliyowekwa na Serikali baadhi ya bidhaa muhimu hivi sasa zinapatikana nchini jambo ambalo linapunguza msukumo wa kutafuta Dola kwa ajili ya uingizaji wa bidhaa hizo, akitoa mfano wa mbolea, mafuta ya kupikia na vifaa vya ujenzi.

“Pamoja na upatikanaji wa bidhaa hizo muhimu, kukamilika kwa baadhi ya miradi ya maendeleo pia kunapunguza mahitaji ya Dola. Kwa mfano, kukamilika kwa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere kunaondoa utegemezi wa jenereta na vitu vingine ambavyo ni chanzo cha nishati ya umeme,” amesema.

Amesema uhaba wa Dola ulikuwa na uhusiano mkubwa na sera za fedha za Marekani na Uingereza zilizowekwa ili kudhibiti mfumuko wa bei katika mataifa hayo na sasa hali inaanza kuimarika, huku kukiwa na matumaini kuwa sera hizo zitalegezwa.

“Mara nyingi sera za namna ile haziwezi kudumu kwa muda mrefu, imepita miaka miwili sasa uzoefu unaonyesha kuna uwezekano wa kulegeza sasa, kwani mfumuko wa bei katika mataifa hayo upo katika hali nzuri, na kuendelea sera hiyo kuna athari zake kwa uchumi wao,” amesema.

Gavana Tutuba amesema Serikali itaendelea kuongeza mzunguko wa Dola kwa kadri wanavyozipata na kuziingiza kwenye uchumi ili kuziba nakisi iliyopo, hatua ambayo inafanya hata thamani yake inayotokana na uhaba kupungua.

Amesema kwa wiki iliyopita pekee BoT iliuza Dola za Marekani 100 milioni (Sh255.2 bilioni).

“Tunaamini hata wale waliozishikilia kwenye black market (soko haramu) siku zijazo wataendelea kupata hasara kwa sababu uchumi unaendelea kufunguka, zile hatari na vihatarishi vilivyokuwapo kwenye uchumi wa dunia vinaendelea kupungua,” amesema.

Akiwahamasisha wenye hoteli kuchangamkia fursa ya kuendesha maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, Tutuba amesema kuna taarifa kuwa fedha nyingine zilizokuwa zikitoka kwenye hoteli zinaenda kwenye soko haramu.

Tutuba amesema kulingana na sera zilivyo sasa za ndani ya nchi, wataendelea kusimamia fedha za kigeni ziendelee kupatikana na kukuza biashara halali inayofanywa nchini na kwa wale ambao wanaendelea kufanya biashara haramu wataendelea kuwafuatilia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Gavana Tutuba amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto hizo, kwani imeendelea kukua kwa asilimia 5.2 na malengo ya mwaka huu ya asilimia 5.3 yanaweza kufikiwa.

Amesema kiwango cha kuimarika kwa uchumi kina mchango mkubwa kuwezesha kuimarika kwa Shilingi.

“Tunafahamu thamani ya Shilingi imetetereka kwa asilimia nane ikilinganishwa na mwaka jana kutokana na kuadimika kwa Dola,” amesema.

Amesema uwiano kati ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi na bidhaa zinazoingizwa imepungua kutoka Dola za Marekani 5.3 bilioni mwaka 2022 na mpaka kufikia Desemba 2023 ilikuwa Dola za Marekani 2.7 bilioni.

“Kwa hiyo utaona kwamba namna tunavyopunguza kuagiza nje tunaendelea kupunguza hiyo nakisi,” amesema.

Hiyo ni kutokana na bajeti ya Serikali ya mwaka jana, ilifungua dirisha la kuongeza mauzo nje ili kuongeza fedha nyingi za kigeni lakini kulikuwa na namna ya kupunguza uingizaji wa bidhaa kwa kuzalisha nyingi ndani ya nchi.

“Hizo zimechangia zaidi kupunguza tofauti kati ya uingizaji na uagizaji wa bidhaa,” amesema.

Amesema kwenye uchumi kuna mifumo mingi wanaendelea kuisimamia ikiwemo kudhibiti riba baada ya kutangaza sera ya fedha Januari.

Kwa sasa riba elekezi ni wastani wa asilimia 5.5. Ukomo wa juu ni asilimia 7.5 na wa chini ni asilimia 3.5.

“Hii inatoa viashiria kwamba bado Shilingi yetu ni himilivu,” amesema.

Hoteli kuanzisha maduka ya fedha

Katika kurahisisha biashara, Oktoba, 2023 Serikali iliamua kufanya mabadiliko kwenye sheria na kanuni ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kuweka dirisha jipya la kuwezesha hoteli zote za kitalii kuanzia nyota tatu hadi tano waanze kuendesha maduka ya kubadilisha fedha kwenye hoteli zao.

“Tumeona watalii wengi wanakuja nchini tunapata fedha za kigeni na kuangalia namna ya kurahisisha ili fedha hizo wanazopata wasipeleke kwenye soko haramu la fedha badala yake wazibadilishe kwenye mfumo rasmi,” amesema.

Amesema baada ya kufanya utafiti walibaini fedha nyingine zinazoenda kwenye mifumo haramu zinatoka kwa watu wa hoteli.

Kifungu cha 26 cha sheria ya Benki Kuu kimetamka wazi kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo itakuwa fedha pekee inayotumika kwenye miamala yote inayofanyika ndani ya nchi.

Gavana Tutuba amesema baada ya Julai Mosi, 2024 wanataka kuona hoteli zote zimejisajili zikiwa na maduka ya ndani ya hoteli wakipokea wateja kama wana fedha za kigeni wanawabadilishia, hatua hiyo itasaidia wamiliki wa hoteli kutoa taarifa na takwimu sahihi za miamala waliopokea za fedha za kigeni.

Amesema wakati mwingine wageni hufika mwisho wa juma au usiku kwenye hoteli maduka ya kubadilisha fedha yakiwa yamefungwa, hivyo kuwapatia usumbufu wageni hao.

Wiki moja iliyopita Tutuba akizungumza na wenye hoteli Tanzania Bara kuhusu fursa ya kufungua maduka ya kubadilishia fedha, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAP), Edward Kennedy alisema dhamira ya BoT ni nzuri, lakini hadi hoteli kuwa na leseni hizo ni mlolongo mwingine mrefu.

"BoT ingekaa na wadau kwanza ili kuidadavua hiyo kanuni, na kuona je itakuwa rahisi kiasi gani kwa pande zote? Je, BoT itakusanya kiasi gani na mimi mwenye hoteli itaniongezea kiasi gani au itanipunguzia kiasi gani?" alisema Kennedy.

Baadhi ya wadau visiwani Zanzibar wamesema licha ya sheria kuwalazamisha kufanya miamala kwa Shilingi lakini ipo miongozo pia ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) inayowataka kulipa kwa Dola.

Ali Haji, mwakilishi kutoka moja ya hoteli kisiwani hapa, amesema sheria hizo zinakanganya, hivyo ipo haja kuangalia jambo hilo.

Kamishana wa Sera za Fedha na Kodi wa ZRA, Hajali Ali amekiri kuwapo malipo kwa baadhi ya hoteli yanayofanyika kwa Dola.

Amesema ni namna ya kukaa na kuangalia jinsi ya kwenda kulifanyia kazi.

Gavana Tutuba amesema wamepoka changamoto hiyo, hivyo wataangalia jinsi ya kulimaliza kwani sheria inataka hivyo.

Amesema katika mataifa yote miamala ya fedha hufanyika kwa sarafu ya fedha ya Taifa husika.