Gari za wagonjwa kuwekewa mfumo wa taksi mtandao

Mbunge wa Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani Sylvestry Koka (kulia) akimkabidhi fungua za magari matatu yaliyonunuliwa na Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Charles Lawisso leo Mjini humo. Picha na Sanjito Msafiri
Muktasari:
- Serikali imekuja na mfumo mpya wa kuyaunganisha magari ya kubeba wagonjwa kutoa huduma hiyo kwa mfumo wa taksi mtandao.
Kibaha. Serikali imesema iko katika hatua za mwisho kuyaunganisha magari ya kubebea wagonjwa kutoa huduma kwa mfumo wa taksi mtandao.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma hiyo, pindi inapohitajika kumsafirisha mgonjwa kutoka eneo moja la kutolea huduma kwenda linguine kwa matibabu zaidi.
"Magari ya wagonjwa yataunganishwa kwenye mfumo na kuwezesha kutoa huduma kama ilivyo kwa magari ya kukodishwa ya taksi mtandao. Kama gari limemuwahisha mgonjwa na kituo kikabaki hakina gari, na kukawa na mgonjwa mwingine anahitaji huduma hiyo, kitakachokuwa kinafanyika ni kuingia kwenye mfumo na kuita gari lingine lililo jirani na mara moja litafika kutoa huduma," amesema mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka.
Koka ambaye alikuwa akizungumza leo Ijumaa Desemba 8, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi magari matatu kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, huku magari mawili kati ya hayo, yatatumika kwa ajili ya shughuli za idara ya elimu.
"Hizi gari za wagonjwa zimewekwa huduma zote za tiba kwa mgonjwa pindi anapoingia ndani, hivyo wakati anapelekwa hospitali ya ngazi ya juu, anakuwa anendelea kupata matibabu, hali ambayo itasaidia kupunguza vifo vya wajawazito," amesema.
Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Charles Lawisso amesema kuwa magari hayo yaliyonunuliwa na Serikali yatarahisisha utoaji wa huduma na utendaji kazi.
"Tulikuwa na gari bovu la kubebea wagonjwa jambo ambalo lilikuwa hatari sana. Sasa tutawahudumia wagonjwa wetu kwa kujiamini zaidi wakati wowote na pia shughuli za utendaji kazi katika idara ya elimu nazo zitarahisishwa, kwani usafiri ni jambo muhimu," amesema.
Diwani wa Kata ya Mkuza, Upendo Ngonyani amesema kuwa kabla ya kupatikana kwa gari la kubebea wagonjwa wajawazito walikuwa wanapata shida.