Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fursa za Kiswahili zatangazwa, matembezi ya mtaa kwa mtaa Dar

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Taifa (Bakita), Consolata Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Wataalamu wa lugha ya Kiswahili wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kuzitumia fursa zinazojitokeza kutokana na kukua kwa lugha hiyo, huku wakisisitizwa kujifunza lugha mbalimbali za kimataifa ile kujiweka katika nafasi nzuri ya kuzipata fursa hizo.

Dar es Salaam. Wadau wa lugha ya Kiswahili wamehimizwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza kutokana na kukua na kuenea kwa lugha hiyo katika maeneo mbalimbali duniani.

Firsa hizo ni pamoja na ufundishaji wa lugha hiyo katika nchi mbalimbali, tafsiri na ukalimani wa taarifa mbalimbali pamoja na uandishi wa vitabu kwa lugha hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mariana Msengi, mfasiri na mwalimu wa lugha ya Kiswahili nchini Urusi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Julai 2, 2024 kuhusu fursa za kujifunza zilizojitokeza kuelekea maadhimisho ya Kiswahili duniani ambayo huadhimishwa Julai 7 ya kila mwaka.

Msengi amesema ili kupata fursa hizo kwa wingi pamoja na kujifunza na kujua vyema Kiswahili na tamaduni zake, ni vyema pia kujifunza lugha na tamaduni nyingine.

“Kitu cha msingi ni kujua mbali na kuwa mahiri katika lugha hiyo, vilevile ni muhimu kujifunza lugha za mataifa mbalimbali, hasa Kingereza pamoja na kuelewa vyema tamaduni zao,” amesema.

Amesema kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Elimu ya Urusi kwa kushirikiana na Chuo cha Teknolojia cha Mendeleev cha nchini humo, wametoa fursa ya vijana 10 wa Kitanzania kwenda nchini Urusi kujifunza lugha pamoja na utamaduni wa nchi hizo.

Awali, akizungumzia kuhusu matukio kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Taifa (Bakita) Consolata Mushi, amesema wanatarajia  kufanya matembezi ya mtaa kwa mtaa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, yakilenga kuitangaza siku hiyo pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha hiyo.

Matembezi hayo yanayotarajiwa kufanyika Ijumaa ya Julai 5, 2024 yatahusisha wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali, wananchi pamoja na wadau wa lugha hiyo, huku yakitarajiwa kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Amesema matembezi hayo yanatarajiwa kuanzia Biafra, Kinondoni na kupita katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Mwananyamala, Makumbusho na kuhitimishwa katika eneo la Posta- Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

"Lengo la matembezi hayo ni kupita katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kuitangaza vyema Siku ya Kiswahili pamoja na kuhamasisha matumizi ya lugha hiyo kwa usanifu," amesema.

Awali, Mushi amesema kabla ya matembezi hayo Julai 3, 2024 kutafanyika mjadala wa kitaaluma utakaojadili mambo mbalimbali kuhusu lugha hiyo, ikiwemo chimbuko, mustakabali, changamoto pamoja na fursa zinazopatikana kupitia kukua na kuenea kwake.

Pia wanazuoni watakajadili uzoefu wa nchi za nje katika ufundishaji wa Kiswahili.

"Watu kutoka nchi za nje wataeleza jinsi wanavyojifunza Kiswahili katika nchi zao. Hafla hiyo itafanyika kwenye ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam," amesema.

Amesema maadhimisho ya siku hiyo yatafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

"Katika siku hiyo zitatolewa tuzo mbalimbali, ikiwemo ile ya Mwalimu Julius Nyerere katika Kiswahili kwa kutambua mchango wake wa kukiendeleza, atakayetunukiwa tuzo hii ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni (Unesco) na itatolewa nchini Ufaransa," amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na uchapaji pamoja na usambazaji wa vitabu, Ape Network, Hermes Damian amesema katika jitihada za kukuza lugha hiyo pamoja na kuhamasisha usomaji wa vitabu, wanatarajia kuja na mkakati wa kusambaza vitabu vilivyoandikwa katika lugha ya Kiswahili kwenye taasisi mbalimbali za umma pamoja na binafsi.

Tangu Unesco kutangaza rasmi kuwa Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, mwaka huu yanaadhimishwa kwa mara ya tatu yakiongozwa na kaulimbiu isemayo 'Fursa za maendeleo ya kugha ya Kiswahili.'